Dk Biteko amlilia Nyamo-Hanga, dereva wake

Dar es Salaam. Kifo ni fumbo la imani. Ni kauli ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko alipozungumza na Mwananchi kuhusiana na kifo cha Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Gissima Nyamo-Hanga pamoja na dereva wake, Muhajiri Haule.

Nyamo-Hanga na Haule wamefariki dunia usiku wa kuamkia leo Jumapili Aprili 13, 2025 katika ajali iliyotokea wilayani Bunda mkoani Mara.

Dk Biteko amesema shirika limepoteza mtendaji mahiri kwa sababu hakuwa mtu wa kukaa ofisini, mara zote alikuwa akifanya kazi zake nje ya ofisini kwa lengo la kutekeleza jukumu alilopewa la kuhakikisha Watanzania wanapata umeme wa uhakika linatekelezwa.

“Kifo ni fumbo, jana tu alikuwa hapa Dodoma kwenye vikao vya bodi vilivyokuwa vinajadili namna ya kuimarisha hali ya upatikanaji wa umeme, kwa kweli tumepoteza mtu rahim sana,” amesema Dk Biteko.

Naibu waziri mkuu amesema miongoni mwa wakurugenzi watendaji waliokuwa wakisimamia vema utendaji wa kazi kwa wafanyakazi sambamba na kujenga timu nzuri, hatoacha kumtaja mkurugenzi mtendaji huyo.

“Hakuwa mbanafsi, alikuwa mnyenyekevu kwa kila mtu, alikuwa anatamani kila Mtanzania apate umeme bila kero, lakini sasa tunafanyaje! Ni mapenzi ya Mungu,” amesema Dk Biteko.

Ametoa pole kwa familia, watumishi wa Tanesco pamoja na ndugu, jamaa na marafiki wote wa marehemu na dereva wake.

Dk Biteko amesema anamuomba Mwenyezi Mungu azijalie subira na uvumilivu familia katika kipindi hiki kigumu huku akisema; “Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu Nyamo-Hanga na Haule mahali pema peponi, Amina.”

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara,  Pius Lutumo akizungumza na Mwananchi kwa simu mapema asubuhi leo, amesema gari alilokuwamo Nyamo-hanga lililokuwa likitokea Mwanza kwenda Bunda, liligongana uso kwa uso na lori.

Amesema chanzo cha tukio hilo ni dereva wa gari lililokuwa limembeba Nyamo-Hanga aina ya Toyota Landcruser kumkwepa mwendesha baiskeli kisha kupoteza  mwelekeo na kugongana uso kwa uso na lori lililokuwa mbele yao.

“Tukio limetokea Bunda saa 7.30 usiku baada ya dereva wa gari dogo kumkwepa mwendesha baiskeli na kugongana uso kwa uso na lori na kusababisha vifo vya dereva (bila kumtaja jina)na bosi wake,” amesema.

Kumbukumbu inaonyesha Nyamo-Hanga aliteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kushika wadhifa huo Septemba 23, 2023 akichukua nafasi ya Maharage Chande, kabla ya uteuzi huo alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Umeme Vijijini (Rea).

Related Posts