DK Mpango: Kutofungamana na mataifa mengine kumetuweka salama

Dodoma. Serikali imesema mpango wa kutofungamana na upande wowote, umeendelea kuifanya Tanzania kutokuwa na uadui na mataifa mengine.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumapili Aprili 13, 2025 na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango alipohutubia kwenye kumbukumbu ya miaka 103 ya hayati Mwalimu Julius Nyerere ambaye aliyefariki dunia mwaka 1999.

Maadhimisho hayo yameratibiwa na Tasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Nyerere ambayo mwenyekiti wake ni Paul Kimiti na makamu wake, Peter Mavunde na kufanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

Dk Mpango amesema kutofungamana na upande wowote ni msimamo uliowekwa na hayati Nyerere enzi hizo na waliofuatia katika uongozi, waliendelea na msimamo.

“Baba wa Taifa aliweka msimamo wa kutokufungamana na upande wowote, falsafa hiyo imeendelea kulifanya Taifa letu liendelee kuwa salama na kutokuwa na uadui na nchi zingine duniani,” amesema Dk Mpango.

Akizungumzia taasisi zilizo chini ya mwamvuli wa mwalimu Nyerere, Dk Mpango amesema Serikali itakuwa karibu nao na itaendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi hizo ikiwamo ujenzi wa makao makuu ya Tasisi ya Mwalimu.

Makamu wa Rais ameiagiza Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Wizara ya Maliasili kufuatilia kwa karibu bajeti ambazo huwa zinatengwa kwa ajili ya ujenzi wa makambusho.

“Lakini niungane na Jaji Mkuu (Profesa Ibrahim Juma) kuwataka vijana muendelee kusoma zaidi vitabu ili muweze kumtambua Mwalimu Nyerere alikuwa nani katika nchi yetu,” amesema Dk Mpango.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Paul Kimiti ameiomba Serikali kuisaidia taasisi hiyo kuondokana na mtazamo kwamba imeundwa kwa ajili ya siasa bali ipo kwa ajili ya kuwapa elimu juu ya maisha ya mwalimu hasa vijana ambao hawakumuona.

Kimiti amesema kuna maeneo historia ya mwalimu inaanza kufutika, hivyo ameomba utaratibu wa kujenga makumbusho uchukuliwe kwa uzito na Serikali.

Mwakilishi wa familia ya hayati Nyerere, Edward Nyerere amesema familia itaendelea kuwashukuru na kuungana na Watanzania katika ushirikiano kutokana na namna ambavyo wameendelea kumuenzi kiongozi huyo ndani na nje ya nchi.

Edward ambaye ni mjukuu wa mwalimu, amesema Mama Maria na Makongoro wamemtuma kuwaambia kuwa familia inawashukuru kwa namna ambavyo wamekuwa karibu nao kwa miaka yote 26 tangu kifo hicho.

Kwa upande wake, Joseph Butiku amesema historia ya mwalimu Nyerere inapaswa kulindwa na kuenziwa lakini akasisitiza inapofanyika shughuli ya namna yoyote kuhusu Rais huyo wa awamu ya kwanza, ihusishe taasisi mama ya Mwalimu Nyerere ili kuepuka kupotosha historia.

Butiku amegusia suala la uchaguzi akisema ni tendo tukufu, akiwataka watakaochaguliwa wasaidie kuwaongoza watu kuishi na kupata maendeleo kwa kuwa ilikuwa ndiyo hoja kuu ya mwalimu.

Related Posts