Dube: Kuna jambo linakuja | Mwanaspoti

TANGU mshambuliaji Prince Dube aanze kucheza Ligi Kuu Bara 2020/21, amesema huu wa sasa ndio anaamini kwamba una tofauti katika maisha yake ya soka, huku akidai kuna kitu cha zaidi kinakuja.

Dube amefafanua kauli yake kwamba ilikuwa kawaida kuumia kila msimu tofauti na sasa ambapo anafurahia kucheza mechi nyingi bila majeraha.

Mshambuliaji huyo aliyetua Yanga msimu huu akitokea Azam katika ligi amehusika na mabao 20 kati ya 64 yaliyofungwa na timu hiyo kupitia nyota 13 tofauti.

Dube ambaye huu ni msimu wa tano katika Ligi Kuu Bara hadi sasa ndiye mchezaji kwenye ligi hiyo aliyehusika na mabao mengi msimu huu akifunga 12 na asisti nane.

Akizungumza na Mwanaspoti, mchezaji huyo alisema ana deni la mabao mawili kufikia rekodi yake ya msimu wa kwanza Tanzania akiitumikia Azam FC, huku matamanio yake ni kuona anacheza mechi zilizobaki na kuisaidia Yanga kubeba ubingwa na yeye kuweka rekodi mpya ya mabao.

“Nakiri kuwa huu ndio msimu wangu bora nimefunga mabao 12 nikiwatengenezea wenzangu mabao nane. Ukiondoa hilo nimeweza kuwa imara bila kuumia. Namshukuru sana Mungu na natamani kuona namaliza msimu bila ya kupata shida yoyote.

“Bado nina nafasi ya kufanya mambo mazuri na nitafanya hivyo kila nitakapopata nafasi. Namuomba Mungu nimalize msimu nikicheza mechi zote na kuipa timu yangu matokeo mazuri bila kujali nitafunga au nitatengeneza nafasi.”

Akimzungumzia mchezaji huyo, kocha wa Yanga, Miloud Hamdi alisema anavutiwa na upambanaji wa Dube eneo la ushambuliaji akidai kuwa sio mchezaji mchoyo ndio maana amekuwa na mafanikio makubwa.

“Dube ni mpambanaji amekuwa bora licha ya kukosa nafasi nyingi sio mtu wa kukata tamaa. Anapambana kuhakikisha timu inapata matokeo mazuri. Asipofunga, basi atatengeneza nafasi ya kufunga kama alivyofanya kwenye mchezo dhidi ya Azam FC.

“Mshambuliaji kazi yake ni kufunga na ni mchoyo, lakini hilo ni tofauti kwa Dube. Naamini anachofanya kitampa namba nyingi kwenye kufunga na hata kutengeneza nafasi, lakini nawapongeza wachezaji wote kuipambania timu.”

Msimu wa kwanza Azam 2020/21 alifunga mabao 14 Azam FC.

Akiwa na Azam alicheza misimu minne akifunga mabao 34 kwenye mechi 54. Msimu wa 2021-21 alifunga mara moja kutokana na kusumbuliwa na majeraha. Msimu wa 2022-23 alifunga mabao 12 na wa mwisho kuitumikia Azam  2023-24 aliifungia mabao saba.

Related Posts