Dar es Salaam. Sio swali tena kuhusu Chadema itashiriki au haitoshiriki uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu, kinachowatafakarisha wadau wa siasa kwa sasa ni mustakabali na hatima ya chama hicho katika mazingira ya kutoshiriki uchaguzi.
Tafakuri hizo zinakuja baada ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuweka wazi kuwa chama hicho hakitaruhusiwa kushiriki uchaguzi wowote kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, baada ya kutosaini kanuni za maadili ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani.
“Chama cha Chadema ambacho hakikusaini kanuni za maadili ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani wa mwaka 2025, hakitashiriki uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu na chaguzi ndogo zitakazofuata kwa muda wa miaka mitano,” alisema Mkurugenzi wa INEC, Ramadhani Kailima.
Baadhi ya wadau wa siasa wanaiona hatua hiyo kama ufunguo wa mlango wa kuzimu kwa chama hicho kikuu cha upinzani, lakini wapo wanaoonyesha matumaini ya uhai wa Chadema hata kisiposhiriki uchaguzi.
Wanachokiona wadau, ndicho kinachoonekana na makundi mawili ya makada ndani ya chama hicho; wengine wakisema ndiyo mwisho wa ufalme wa Chadema katika upinzani na wapo wanaosema kilichofanyika ni ithibati ya msimamo walioujenga tangu awali.
Katikati ya mazingira hayo, kwa chama cha ACT Wazalendo ni kama vita vya panzi furaha kwa kunguru; chenyewe kimeweka wazi milango yake kuwapokea wataokimbia kwa kukosa nafasi za kugombea kutoka Chadema na kwingineko, kama ilivyoelezwa na Makamu Mwenyekiti wake Bara, Issihaka Mchinjita.
Hata hivyo, uamuzi wa wanachama wasiokubaliana na msimamo wa Chadema kutoshiriki uchaguzi, maarufu G55, kwa mujibu wa Katibu wao, Edward Kinabo utatolewa hivi karibuni baada ya vikao vya mashauriano.
Chadema itavuna, kupoteza nini?
Chama cha Wananchi (CUF) kinaujua uchungu na madhara kwa chama cha siasa kutoshiriki uchaguzi, kwa kuwa kiliwahi kususia uchaguzi wa marudio wa Zanzibar Machi 2016.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Husna Abdalla, amesema uamuzi huo ulikisababishia chama hicho kukosa haki ya kusimamisha wagombea.
Hilo liliambatana na kuwavunja moyo wanachama, ambao alisema waliamini chama chao ndicho kingewapa viongozi bora na sahihi kupitia uchaguzi.
“Ilivyotokea tumesusa, wanachama wakapoteza matumaini wakaona hawana nafasi tena ya kupata viongozi wanaowataka kutoka ndani ya chama chetu. Tukawavunja moyo,” ameeleza Husna.
Sambamba na hilo, amesema chama hicho kilikosa ruzuku inayopatikana kwa makadirio ya idadi ya kura za urais ambazo chama husika kimezipata katika uchaguzi.
“Tulipoteza ruzuku. Kile ambacho tuliweza kukifanya tulipokuwa na ruzuku, tukashindwa kukifanya. Taratibu tukawa tunapoteza nguvu,” amesema.
Katika mazingira hayo, amesema kuna hatari ya kupoteza wanachama wengi, kama ilivyokuwa kwao wakati huo, kwa sababu wanatafuta matumaini nje ya taasisi waliyopo.
“Kwa sababu kila mtu anaingia kwenye siasa akiwa na lengo la kuwania nafasi fulani. Wapo wanaoamini akishinda atafanikiwa au mwingine akishinda naye atafanikiwa. Akiona hakuna nafasi ya kushindana ndani ya chama hicho wanaondoka,” amesema.
Maumivu mengine, Husna amesema, ni kuipa nafasi CCM ya kubaki yenyewe katika vyombo vya uamuzi na hivyo kutumia mwanya huo kupitisha sheria, kanuni na taratibu zinazolinda maslahi yake.
“Hatua ile ukawa mwanya wa kupitishwa kwa sheria nyingi za ovyo, na sisi (CUF) tulibaki kusemea nje, tukikosa mamlaka ya kusema na kusikilizwa kwa kuwa hatukuwa sehemu ya Bunge,” ameeleza.
Mwandishi mwandamizi wa habari, Absalom Kibanda, amesema pamoja na doa kwa demokrasia ya nchi, uamuzi wa Chadema kutoshiriki uchaguzi una athari hasi kwa chama hicho zaidi.
Amejenga hoja hiyo akirejea kilichotokea kwa CUF iliposusia uchaguzi wa marudio mwaka 2016; hakikupata kilichodhamiria, zaidi ya kupoteza mvuto kwa umma.
Kwa mujibu wa Kibanda, kama Chadema itaendelea kushikilia msimamo wake huo, kitaathirika zaidi ya kupata matokeo ya kile inachokilalamikia.
“Kilichotokea ni bahati mbaya kwa mustakabali wa demokrasia nchini, hasa kwa chama ambacho tangu mwaka 2010 kilikuwa kinara wa upinzani,” amesema.
Hata hivyo, amesema hatima ya taasisi huamuliwa na uongozi wake, na kwa sasa viongozi wa chama hicho wameamua kusimamia msimamo wa kutoshiriki uchaguzi, hivyo wanaamua hatima ya Chadema.
Lakini, amesema mwenendo wa kilio cha demokrasia kwa sasa umeonekana kote duniani, hali inayochangia kupungua kwa idadi ya wapiga kura.
Amesema kutokana na hali ilivyo, INEC itakuwa na jukumu zito la kuwashawishi wananchi kushiriki kupiga kura.
Kitaumia lakini hakitapotea
Kwa mtazamo wa Katibu Mkuu wa Shura ya Maimamu, Sheikh Issa Ponda, haoni Chadema ikipotea endapo hakitashiriki uchaguzi, kwa kuwa kinadai mambo ya msingi.
“Tulijua haya mapema kwa sababu Serikali ilishaweka msimamo wa kutobadili Katiba wala sheria na Chadema waliweka msimamo wao. Wanachokipigania ni mambo ya msingi; wanaweza kuumia lakini ndiyo faida ya kupigania haki,” amesema.
Amesema kinachopiganiwa na Chadema sasa huenda kisinufaishe chama hicho kwa sasa, lakini baadaye kitawanufaisha wengine.
Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche, akizungumzia madai ya chama hicho kufa kama hakitashiriki uchaguzi, alisema wataendelea kusimamia ukweli hata kama chama kikifa.
“Wanatutishia kwamba Chadema itakufa isiposhiriki uchaguzi, Chadema itakufa hii… na ife kama itasimamia jambo la kweli na watu wasijue kama inasimamia ukweli… na ife kuliko iwepo na kusimamia uongo.
“Kuliko tuwe na chama kinachosimamia uongo, tupo tayari wengine kuacha siasa—kama viongozi wetu mnataka mimi na (Tundu) Lissu tusimamie uongo,” amesema Heche katika moja ya mikutano ya hadhara anayoendelea nayo mikoani.
Mwanazuoni wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Sabatho Nyamsenda, anaona uamuzi wa Chadema na mambo inayolalamikia yanapaswa kuitafakarisha INEC.
Hatua ya chama hicho kususia kusaini kanuni za maadili, anaihusisha na utekelezaji wa ajenda ya chama hicho ya No Reforms, No Election.
“Taasisi (INEC) unapoweka masharti ya kuondoa watu kutoshiriki uchaguzi na wewe ndiyo unazisimamia hizo taasisi, unaonyesha tayari una upande wako. Unafunga milango ya yale yanayolalamikiwa kutoshughulikiwa hata kwa muda mchache uliopo,” amesema.
Kwa mantiki hiyo, amesema hoja zinazopigiwa kelele na Chadema, ikiwemo madai kwamba CCM inatumia dola kubaki madarakani na kutokuwepo kwa uwanja sawa katika uchaguzi zina mashiko, na hata tafiti mbalimbali za wanazuoni zinathibitisha hivyo.
Kwa mtazamo wa viongozi wa kiroho, kuna umuhimu wa kutumika busara kuangalia yanayopaswa kufanyika ili kuwe na uchaguzi huru na haki.
“Kama nikipata nafasi ya kuzungumza na viongozi wenzangu wa dini, jambo kubwa nitakalowaambia ni watumie nafasi zao kusaidiana na wanasiasa kuwaunganisha Watanzania kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu,” amesema Askofu Mkuu wa Kanisa la Mennonite Tanzania, Nelson Kisare.
Amesisitiza mazungumzo yachukue nafasi ya bunduki na mabomu ya machozi, huku kodi za wananchi zisitumike kununua mabomu ya kupiga wananchi, badala yake, haki itawale matendo, mawazo na nia.
Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima, amesema kabla ya kuangalia mustakabali wa Chadema na demokrasia, ni vema kujiuliza uchaguzi wa Tanzania una sura gani.
“Tumefanya chaguzi tangu mwaka 1995. Kabla hatujaangalia ndani ya vyama, hebu tujiulize uchaguzi wa Tanzania una sura gani. Mimi naishia hapo, siwezi kusema zaidi,” amesema.
Katibu Mkuu wa Baraza la Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Nuhu Mruma, amesema kwa mtazamo wake, mabadiliko hayawezi kufanywa siku moja; yanahitaji mchakato.
Kwa mujibu wake, ulipoisha uchaguzi wa mwaka 2020, ndio uliokuwa wakati sahihi wa kufanya mabadiliko, lakini kwa sasa muda uliobaki hautoshi.
“Kwa sasa tumechelewa, bora tuendelee na uchaguzi, kisha baadaye ndiyo tuje na hayo mabadiliko,” amesema Sheikh Mruma.
ACT mguu sawa kupokea wanachama
Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Bara, Issihaka Mchinjita, amesema milango ya ACT Wazalendo ipo wazi kuwapokea wanachama wapya washirikiane nao kulinda demokrasia.
“Tunajua kuna changamoto za mifumo ya chaguzi zetu, lakini ni vema kupambana nayo. Na moja ya jukwaa muhimu la mapambano ni uchaguzi. Tunawakaribisha wote,” amesema.
Mchinjita amesema wamejipanga vyema na kuna mifumo imara ndani ya ACT-Wazalendo kuhakikisha ujio wa mwanachama mpya hauathiri mshikamano uliopo.
Ameeleza kuwa, iwapo watajiunga na chama hicho, watapewa nafasi sawa na waliokuwepo kushiriki kuwania nafasi mbalimbali za ndoto zao, kwa kupitia michakato halali na stahiki.
“Kwa sasa wanachama wanatia nia na kutoa taarifa, utafika wakati watatakiwa kuchukua fomu. Kama wanachama wapya watakuwepo, nao watapewa fursa sawa na kuingia kwenye mchujo,” amesema Mchinjita.
Amesisitiza kuwa ndani ya chama hicho hakuna mwanachama mwenye haki na mamlaka ya kuwa mgombea mwenyewe, hivyo kila mtu atapewa nafasi.
Kwa kuwa chama hicho kitashiriki uchaguzi, amesema wanachama wapya na wenye nia ya kugombea wajiunge ili kupata nafasi hizo.
“Utakapofanyika uamuzi, na akiwa mwanachama, ataingia katika kura za maoni na kupewa nafasi kama mwanachama mwingine,” ameeleza.
Sharti kwa chama cha siasa kusaini Kanuni za Maadili linatajwa katika Ibara ya 162(1)(a), kinachoeleza kuwa Tume itaandaa na kuchapisha katika Gazeti la Serikali Kanuni za Maadili ya Uchaguzi.
Kwa mujibu wa ibara hiyo, kanuni hizo zitaainisha maadili ya vyama vya siasa, Serikali na Tume wakati wa kampeni za uchaguzi na utaratibu wa utekelezaji wake.
Kifungu cha 162(2)(a) hadi (c) vinataja wahusika wa kusaini kanuni hizo ambao ni Serikali, INEC, chama cha siasa na wagombea, huku kipengele (3) kikieleza kuwa atakayekiuka ataadhibiwa kwa masharti ya kanuni husika.
“Mtu ambaye atakiuka masharti ya kanuni za maadili ya Uchaguzi ataadhibiwa kwa mujibu wa kanuni hizo,” kinaeleza kipengele cha (3) cha ibara hiyo.
Wakati kifungu cha 1.5(a) kinachoeleza wajibu wa kusaini, kuthibitisha na kuheshimu kanuni za maadili, kinaweka wazi kuwa chama cha siasa ambacho hakitasaini kitazuiliwa kushiriki kwenye kampeni za uchaguzi.
“Chama cha siasa ambacho hakitasaini kanuni hizi za maadili, kitazuiliwa kushiriki katika kampeni za uchaguzi,” kinaeleza kifungu hicho.
Hatua hiyo imewaibua wataalamu wa sheria, wanaosema kuwa sheria haijafafanua iwapo chama cha siasa hakitasaini kitakosa haki ya kushiriki uchaguzi.
“Sijui hawa wenzetu wanazisomaje hizi sheria. Je, ni utofauti wa vyuo? Hakuna sheria inayozuia chama kushiriki uchaguzi kwa kutosaini maadili ya uchaguzi; ni tafsiri mbovu ya kukosa logic (mantiki). Tuache kuharibu Taifa na kuchochea vurugu,” amesema Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi.
Hoja ya changamoto ya tafsiri ya sheria imeibuliwa pia na Wakili Edson Kilatu, aliyesema kuwa sheria haijaeleza adhabu au athari ya moja kwa moja kwa chama au mgombea asiyesaini.
“Haki ya kushiriki uchaguzi ni ya kikatiba na haiwezi kuondolewa kwa kutokuwepo saini ya kanuni,” amesema.
Amesema kifungu cha 162(2) kinaelekeza waliotia saini kuzingatia kanuni, lakini hakielezi kuhusu wasiosaini.
“Hii inaacha mwanya wa kisheria (lacuna) unaoweza kutumiwa na baadhi ya wadau,” amesema Wakili Kilatu.
Wakili Jebra Kambole amesema katika sheria hakuna kipengele kilichoweka ukomo wa muda wa chama au mgombea kusaini, hivyo vyama vina nafasi ya kusaini siku yoyote.
“Hakuna ukomo wa kusaini kanuni za maadili. Chama au mgombea atasaini muda wowote,” amesema.
Kwa mujibu wa Kambole, uchaguzi unasimamiwa na Katiba na siyo kanuni, hivyo hakuna uwezekano wa chama au mgombea kukosa haki ya kushiriki mchakato huo kwa sababu za kikanuni.
Jitihada za kuipata INEC kuzungumzia utata huo wa kisheria na kikanuni hazijazaa matunda, kwani si Mkurugenzi wake, Ramadhan Kailima, ama Mwenyekiti wake, Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele, waliopatikana.
Matokeo ya Chadema tangu 1995
Katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi, mwaka 1995, Chadema haikuwa na mgombea wa urais; walikuwepo wa ubunge na walishinda wanne kati ya nafasi 269.
Kama ilivyokuwa mwaka 1995, katika uchaguzi wa 2000, chama hicho hakikuwa na mgombea urais, lakini kilisimamisha wagombea ubunge na waliongezeka hadi kufikia watano.
Chadema ilianza kusimamisha wagombea katika nafasi ya urais kwenye Uchaguzi Mkuu 2005, ilipomsimamisha Freeman Mbowe, aliyepata kura 668,756 sawa na asilimia 5.88 ya kura zote.
Katika uchaguzi huo, ushindi wa wabunge kupitia chama hicho uliongezeka na kufikia 11 wa majimbo na viti maalumu.
Mwaka 2010, chama hicho kilimsimamisha Dk Willibrod Slaa, aliyepata kura milioni 2.27 sawa na asilimia 27.05 ya kura zote, huku kikijipatia viti 48 vya ubunge wa majimbo na viti maalumu.
Wastani wa kura za urais za Chadema uliendelea kupanda, hata katika uchaguzi wa mwaka 2015 ilipomsimamisha Edward Lowassa kupitia muungano wa vyama (Ukawa); ilipata kura milioni 6.07 sawa na asilimia 39.97 ya kura zote na wabunge 73 wa majimbo na viti maalumu.
Hali ikawa mbaya katika uchaguzi wa mwaka 2020, chini ya mgombea Tundu Lissu, aliyepata kura milioni 1.93 sawa na asilimia 13.04, huku ikiambulia wabunge 20, kati yao ni mmoja tu aliyeshinda jimboni.