Katika ulimwengu wa leo ambao umejaa vishawishi, mashinikizo na changamoto nyingi, hakuna zawadi bora ambayo mzazi anaweza kumpatia mtoto wake zaidi ya kumjengea msingi wa hekima na busara.
Tunaambiwa kuwa hili ni jukumu lisiloisha na linahitaji subira, mawasiliano ya mara kwa mara na mfano wa kuigwa baina ya mzazi na mwanawe.
Na tunaambiwa kwa kuwafundisha watoto kuwa na hekima na busara, mzazi atakuwa anajenga kizazi chenye maadili, chenye maono na chenye uwezo wa kujenga jamii bora kwa siku zijazo.
Katika malezi ya watoto, kuna maadili na tabia ambazo ni muhimu zaidi ya elimu ya darasani au mafanikio ya kitaaluma.
Na miongoni mwa maadili hayo yanayozungumzwa ndiyo pamoja na kumfunza mtoto awe na hekima na busara ambazo ni nguzo kuu zitakazomsaidia mbele ya safari kuja kufanya uamuzi sahihi, kuishi kwa amani na jamii atakayokuja kuchangamana nayo.
Lakini pia kuenenda katika njia ya heshima na maadili mema ndiyo sahihi zaidi.
Lakini katika jamii nyingi, hususan zile za Kiafrika, wazazi wanachukuliwa kuwa walimu wa kwanza kwa watoto wao.
Hivyo basi, ni jukumu lao kubwa kuwafundisha watoto umuhimu wa kuwa watu wenye hekima na busara.
Naandika hivyo kwa hata mimi nilifunzwa na wazazi wangu kuwa hekima ni uwezo wa kutumia maarifa na uzoefu katika kufanya uamuzi wenye mantiki na manufaa kwa muda mrefu.
Lakini pia inasaidia kuona mbali na kutathmini matokeo ya uamuzi kabla ya kuufanya na busara kwa upande mwingine, ni uwezo wa kuchambua mambo kwa makini na kuchukua hatua inayofaa kwa wakati unaofaa.
Na tukumbuke kuwa hekima na busara huenda pamoja na kwa pamoja, zinamwezesha mtu kuishi kwa amani na watu wengine huku akijiheshimu mwenyewe.
Hivyo mzazi ukimfundisha haya yote mwanao akingali bado mdogo, ni wazi atakuwa katika mstari sahihi wa maisha.
Tukumbuke kuwa watoto wanapokua, hukutana na changamoto nyingi katika maisha yao, kuanzia uhusiano na wenzao, changamoto za masomo, hadi uamuzi kuhusu maisha yao ya baadaye.
Kama atakuwa hana msingi wa hekima na busara, kuna hatari ya wao kushindwa kuchagua njia sahihi.
Hivyo, wazazi kwa uzoefu wao wa maisha, wanayo nafasi bora ya kuwafundisha watoto namna ya kukabili changamoto hizi kwa ustadi na busara.
Kwa mfano, mtoto anapojifunza kutoka kwa mzazi kwamba si kila kitu kinahitaji majibu ya haraka au kwa hasira, huanza kuendeleza uwezo wa kuhimili hisia na kuchambua hali kabla ya kuchukua hatua.
Vilevile, mtoto anapofundishwa kujifunza kutokana na makosa yake badala ya kukata tamaa, anakua na hekima ya kweli inayotokana na uzoefu.
Kwa hivyo, ni vema ukamridhisha mtoto mbinu sahihi itakayomwezesha kuwa mtu mwenye busara na hekima.
Kwa mfano, watoto hujifunza zaidi kwa kuangalia tabia za wazazi wao. Wazazi wanapokuwa watu wenye uamuzi wa busara, wanaoweza kusikiliza na kujibu kwa utulivu, watoto wao pia hujifunza kuwa hivyo.
Na katika hili pia mazungumzo ya kila siku kuhusu maisha, changamoto na uamuzi huwasaidia watoto kuelewa namna ya kukabiliana na hali mbalimbali.
Na kwa njia ya mazungumzo ya mara kwa mara, kutasaidia wazazi kupanda mbegu za hekima katika akili na mioyo ya watoto wao.
Tukumbuke kuwa watoto wanapopewa nafasi ya kushiriki katika uamuzi mdogo nyumbani, wanajifunza pia namna ya kufikiria kwa kina na kutathmini matokeo ya chaguo walilofanya. Hii huimarisha uwezo wao wa kufikiri kwa hekima.
Wataalamu wa malezi wanasema kuna umuhimu pia wa kuwafundisha umuhimu wa kujifunza kutokana na makosa.
Mzazi badala ya kuwaadhibu kwa kila kosa, unaweza kutumia makosa kama fursa ya kuwafundisha.
Hii huwasaidia watoto kuwa watu wanaojitafakari na kujifunza, badala ya kukata tamaa. Mtoto mwenye hekima na busara huwa na uwezo mkubwa wa kujizuia kufanya uamuzi wa haraka bila kufikiria.
Na anaweza kuwasiliana vizuri na watu na anaweza akawa mtu wa kuheshimu maoni ya wengine pia.
Mtoto wa aina hii anayo nafasi nzuri ya kufanikiwa katika maisha kwa sababu anaweza kushughulikia matatizo kwa ustadi na si kwa jazba.
Tukumbuke pia kuwa hekima na busara pia husaidia watoto kuepuka vishawishi vinavyoweza kuwaangamiza, hasa katika umri wa ujana.