MSHAMBULIAJI wa Mashujaa, Jaffar Kibaya anayemiliki mabao matatu hadi sasa katika Ligi Kuu, ametoa hamasa kwa mastaa wenzake hususani wanaocheza eneo la ushambuliaji kutumia kwa makini nafasi wanazozipata ili kuisaidia timu hiyo imalize kibabe mechi zilizobaki ili wasalie kwa msimu ujao.
Kibaya aliyeanza kupata nafasi kikosini tangu Mashujaa imuajiri kocha Salum Mayanga aliyewahi kufanya naye kazi Mtibwa Sugar, ameahidi kuendeleza moto alioanza nao ikiwamo kufunga katika mechi mbili mfululizo katika nafasi anayocheza pia straika mkongwe, Danny Lyanga aliyetokea JKT TZ.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kibaya alisema eneo la ushambuliaji la timu hiyo, halina makali kutokana na kufunga mabao 25 tu kupitia mechi 25, huku yenyewe ikifungwa 28 na kwa sasa imeweka mikakati mipya chini ya Mayanga aliyetua hapo akitokea Mbeya City iliyopo Ligi ya Championship.
“Tangu ujio wa Mayanga, timu imekuwa ikiongeza kasi kwa kufuata matakwa ya kocha hasa eneo la ushambuliaji analolifanyia kazi zaidi mara kwa mara na kutusisitiza kutumia kila nafasi tunazozipata na ukiangalia katika mechi mbili za hivi karibuni idadi ya mabao ya kufunga inaongezeka,” alisema Kibaya na kuongeza;
“Tukiwa na Mayanga tumepoteza mbele ya Pamba Jiji kwa bao 1-0, tumeshinda 3-0 dhidi ya Fountain Gate na Tabora United na kati ya mechi hizo nimehusika kufunga bao moja moja hii ni kutokana na kuaminiwa na mimi kutaka kuonyesha.
“Naamini kama mwalimu atazidi kunipa nafasi zaidi, nitakuwa nafunga au kutengeneza nafasi nyingi za mabao ambayo yatatupa pointi ambazo sisi tunazihitaji kwa ajili ya kujihakikishia nafasi ya kucheza ligi msimu ujao.”
Kibaya aliyeibuka Nyota wa Mchezo dhidi ya Fountain Gate, alisema kama wachezaji wanahitaji kufanya vizuri katika mechi zilizobaki kwa kuwa imara eneo la ushambuliaji ili kujiweka pazuri dhidi ya vita kubwa iliyopo ya kushuka daraja kwani bado Mashujaa haipo eneo zuri kwa pointi ilizonazo.
Mashujaa ipo Ligi Kuu kwa msimu wa pili baada ya kupanda msimu uliopita.