Ukiniuliza mimi nitakwambia natamani mtoto wangu awe mwanasayansi wa kwanza wa Kitanzania kugundua sayari nyingine ambayo binadamu tunaweza kuhamia na kuishi kama.
Au aanzishe kampuni ambayo itatengeneza roketi na kuratibu usafirishaji wa binadamu kutoka hapa kwenda huko. Na kupitia yote hayo, ashinde ‘Nobel prize’ na tuzo nyingine kubwa kubwa za sayansi, uvumbuzi na biashara.
Kupitia biashara yake hiyo, akusanye pesa nyingi zitakazomfanya awe tajiri mkubwa zaidi duniani. Na aandike historia ya kuwa na pesa nyingi kiasi kwamba hata watu tisa wanaomfuatia kwenye orodha ya matajiri wakikusanya utajiri wao wote, wasimfikie hata nusu.
Pia, awe mwanamuziki mkubwa wa kwanza duniani ambaye anafanya onyesho kwenye viwanja vikubwa na kwa kiingilio kikubwa kuwahi kutokea na bado awe anajaza uwanja. Na licha ya tiketi za onyesho kuuzwa kwa bei kubwa kiasi hicho bado ziwe zinaisha ndani ya dakika tano tangu kuanza kuuzwa.
Nani kati yetu asiyetamani kuwa na mtoto wa aina hiyo? Hakuna. Kila mtu kati yetu anatamani mwanawe awe Bakhresa ajaye, awe Cristiano Ronaldo wa kizazi kipya, kila mtu anatamani mtoto wake awe mtoto mwenye mafanikio makubwa.
Sio mbaya kabisa kutamani yote hayo kwa mtoto wako lakini wazazi tunakosea sana namna tunavyofikisha ujumbe kwa watoto wetu kuhusu matarajio yetu juu yao. Mara nyingi tumekuwa watu wa kuwalinganisha sana na watoto wengine kama sio kutumia lugha kali na zenye kuvunja moyo.
Kwa sababu mtoto wako anafanya vibaya kitaaluma darasani, lugha pekee unayoitumia ni ‘wewe huna akili’, ‘mbona mtoto wa fulani anafanya hivi, wewe unashindwa nini?’
Ni rahisi sana kutumia lugha hizo lakini ukweli ni kwamba zinaua mioyo ya watoto wetu badala ya kuwajenga.
Na hili wala halikutakiwa kuandikwa kwenye magazeti, ni jambo ambalo pengine kila mtu mzima mwenye akili timamu alitakiwa awe na uelewa na ufahamu kwamba binadamu tunafoautiana sana. Kila mtu ana upungufu wake kama ambavyo kila mtu amejaaliwa uwezo wake.
Unahangaika kumlinganisha mtoto wako na watoto wengine, kwa mfano, unataka awe vizuri kwenye hesabu kama hao wengine, lakini ukweli ni kwamba, sio kila mtu duniani atakuwa ni mzuri wa hesabu.
Kila mtu ana kitu chake anachokiweza. Kwahiyo badala ya kutaka mwanao awe unavyotamani, ni bora ungepambana kutamani kujua uwezo wa mwanao na kumjenga afanikiwe upande huo.
Halafu, kama kulinganisha ingekuwa inafanya kazi mbona kwako imeshindwa kukusaidia? Maana hauna pesa kumzidi Elon Musk, hauchezi mpira kumzidi Messi, sio maarufu kumzidi Michael Jackson, wala sio namba moja kwenye unachokifanya.
Kwahiyo, mtu wa kwanza aliyetakiwa kufahamu kwamba kulinganisha haisadii ni wewe.