Unguja. Waziri wa Afya Zanzibar, Ahmed Nassor Mazrui amesema utafiti uliofanywa na wizara hiyo kwa kushirikiana na taasisi nyingine, kuhusu viashiria hatarishi na ufuatiliaji wa hali ya magonjwa yasiyoambukiza nchini, umebainisha kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanya ili kufikia malengo ya maendeleo endelevu ifikapo mwaka 2030.
Licha ya hali hiyo, amesema bado kuna changamoto ya watu kutozingatia matibabu ya magonjwa hayo, ambapo takwimu zinaonesha kuwa ni mtu mmoja tu kati ya kila watu watano wenye shinikizo la damu anayetumia dawa, na kati yao ni asilimia 3.2 ndio wamefanikiwa kudhibiti ugonjwa huo.
Waziri Mazrui ametoa kauli hiyo leo Jumapili, Aprili 13, 2025, wakati akifunga mkutano wa tatu wa kimataifa wa moyo Tanzania (Cardio Tan 2025), ulioandaliwa na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na kuwaleta pamoja wataalamu wa moyo kutoka mataifa ya bara la Ulaya, Asia, Amerika na Afrika.
Ametumia fursa hiyo kuwataka washirika wote kuendelea kushirikiana kwa karibu katika kuendeleza tafiti, kuboresha matibabu na kutoa elimu katika jamii.
“Nitoe wito kwa washiriki wote kuendelea kushirikiana kwa karibu katika kuendeleza tafiti, kuboresha matibabu, na kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kuzuia magonjwa ya moyo,” amesema na kuongeza kuwa:
“Ni lazima tujenge uelewa wa watu kuhusu tabia bora za kiafya, ikiwemo kula vyakula bora, kufanya mazoezi na kuepuka matumizi ya pombe na sigara. Jamii zetu zinahitaji kupatiwa uelewa huu ili kuweza kupunguza idadi ya wagonjwa wa moyo.”
Waziri Mazrui amesema idadi ya wagonjwa ambao hawapo kwenye dawa na wanaoweza kudhibiti ugonjwa ndiyo wamekuwa tishio, kwa sababu wengi hufika hospitalini wakiwa katika hali mbaya na kutumia gharama kubwa za matibabu.
Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti huo, theluthi moja ya watu wamekuwa na tabia ya kubweteka, na kwa wanawake kumekuwa na ongezeko kubwa la kutofanya mazoezi miongoni mwao.
Amesema utafiti unaonesha mwanamke mmoja kati ya wawili ameripotiwa kuwa na tabia bwete, ikilinganishwa na mwanaume mmoja kati ya kila watano.
“Taarifa pia inaonesha ongezeko la idadi ya watu wenye hali ya unene na unene uliokithiri kutoka asilimia 26 mwaka 2012 hadi kufikia asilimia 30.8 mwaka 2023,” amesema Mazrui.
Katika utafiti huo pia inaonesha asilimia 7.6 tu ya watu ndio hutumia kiwango stahiki cha matunda na mbogamboga, asilimia 20 wameripotiwa kuwa na tabia ya kutumia chumvi kwa wingi, na asilimia 10.9 hutumia vyakula vilivyosindikwa viwandani, hivyo kusababisha maradhi hayo hususani maradhi ya moyo.
Pamoja na uwepo wa viashiria hivyo hatarishi, amesema bado utafiti unaonesha kupungua kwa matatizo ya kisukari kutoka asilimia 9.1 hadi asilimia 2.8 kwa mwaka 2023, huku tatizo la ugonjwa wa shinikizo la damu pia likipungua kutoka asilimia 26.0 mwaka 2012 hadi asilimia 22.
Kadhalika, kiasi cha matumizi ya pombe kimeshuka kutoka asilimia 29 hadi asilimia 20 kwa mwaka 2023; matumizi ya sigara yamepungua kutoka asilimia 14.1 mwaka 2012 hadi asilimia 10.0 mwaka 2023.
Akizungumza kuhusu mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk Peter Kisenge amesema umekuwa na mafanikio makubwa kwani wapo madaktari wa Tanzania waliopata fursa za kwenda kwenye mafunzo Marekani.
Amesema wamekutanisha wataalamu 424 kutoka nchi zaidi ya 25, ambao kati yao wageni kutoka mataifa mbalimbali ni 107 na washiriki wa ndani ni 317.
Amesema katika kutekeleza kaulimbiu isemayo ‘Kuimarisha huduma za moyo barani Afrika kupitia jitihada za pamoja’, wamekutanishwa wakuu wa taasisi za moyo kutoka taasisi za kimataifa na kufanikiwa kujadili mambo muhimu ya kukabiliana na changamoto za moyo.
“Ni pamoja na jinsi taasisi za moyo zinavyoweza kuimarisha huduma za matibabu ya magonjwa ya moyo kupitia njia ya ushirikiano.
“Tumekaa na viongozi mbalimbali tukakubaliana namna tunavyoweza kushirikiana kuimarisha huduma za matibabu ya magonjwa ya moyo kupitia njia ya ushirikiano,” amesema.
Kwa mujibu wa Dk Kisenge, mbali na kuboresha huduma za matibabu ya moyo, kupitia mkutano huo wamefanikiwa kutekeleza tiba utalii nchini, kwani Afrika na dunia nzima wameona na kujenga imani juu ya uwezo wa nchi katika huduma za afya, hususani moyo.