KOCHA wa Biashara United, Omary Madenge amesema sare ya bao 1-1, iliyoipata kikosi hicho Aprili 9, dhidi ya Mbeya City kwenye Uwanja wa Karume Mara, imewaongezea morali ya kupambana ili kuinusuru timu hiyo isishuke daraja.
Madenge aliyekuwa Mkurugenzi wa Ufundi katika timu hiyo kabla ya kuifundisha baada ya kuondoka kwa Kocha Mussa Rashid aliyejiunga na Polisi Tanzania, alisema michezo minne iliyobakia inawapa matumaini makubwa ya kukinusuru kikosi hicho.
“Pointi moja tuliyoipata kwa Mbeya City kwetu ni kubwa sana kwa sababu ukiangalia tulianza kufungwa na wachezaji wetu wakapambana hadi tukasawazisha, naamini bado tuna nafasi kubwa ya kubakia ikiwa tutachanga vyema karata zetu,” alisema.
Katika michezo minne iliyobakia ya timu hiyo, miwili ni ya nyumbani dhidi ya Geita Gold Mei Mosi na ule wa mwisho wa msimu na Polisi Tanzania Mei 10, huku ya ugenini ni mbele ya Cosmopolitan Aprili 18, kisha Green Warriors, Aprili 26.
Timu hiyo iliyoshuka daraja msimu wa 2021-2022, inapambana kuepuka janga la kushuka daraja kwani katika michezo yake 26, iliyocheza imeshinda sita, sare mitano na kupoteza 15, ikifunga mabao 20 na kuruhusu 42, ikiwa mkiani na pointi nane.
Hali ya timu hiyo ilianza kuonekana tangu mwanzoni baada ya kuandamwa na ukata ulioifanya kushindwa kufika katika mchezo wa ugenini dhidi ya Mbeya City uliotakiwa kuchezwa Desemba 3, 2024, hivyo kukatwa pointi 15 na Bodi ya Ligi Kuu (TPLB).