Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco afariki dunia

Mara. Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Usambazaji Umeme Tanzania (Tanesco), Gissima Nyamo-Hanga amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Aprili 13, 2025 katika ajali iliyotokea wilayani Bunda mkoani Mara.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, ambapo amefafanua kuwa  limetokea kati ya saa 6 hadi 7 usiku wa kuamkia leo.

“Ni kweli tukio lipo na amefariki dunia ila wasiliana na RPC atakuwa na taarifa kwa kina,” amesema  Mtambi

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo huku akiahidi kutoa taarifa baadaye kidogo.

“Ndio nimefika eneo la tukio naomba muwe na subira nitakupa taarifa baadaye,”amesema Kamanda Lutumo.

Meneja wa Tanesco Mkoa wa Mara, Nickson Babu amesema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Bunda huku wakisubiri taarifa zaidi kuhusu taratibu nyingine.

Endelea Kufuatilia Mwananchi kwa taarifa zaidi

Related Posts