UONGOZI wa Transit Camp umefikia makubaliano na aliyekuwa Kocha wa Kipanga FC ya visiwani Zanzibar, Ramadhan Ahmada Idd, kukiongoza kikosi hicho kwa michezo iliyosalia, akichukua nafasi ya Stephen Matata aliyeondoka kikosini.
Akizungumza na Mwanaspoti jijini Dar es Salaam, Ahmada alikiri kufikia makubaliano na uongozi wa timu hiyo, huku akiomba sapoti kubwa kutoka kwa mashabiki wa kikosi hicho, ili kwa pamoja wakinusuru na janga la kushuka daraja msimu huu.
“Nashukuru kwa imani kubwa niliyopewa hapa, ni changamoto sana kwangu kwa sababu nimeipokea timu ikiwa katika hali mbaya na napaswa nipambanie kuinusuru isishuke daraja, kitu kitakachotusaidia ni umoja na wachezaji kikosini,” alisema Ahmada.
Ahmada anakuwa ni kocha wa tatu msimu huu kuiongoza timu hiyo, baada ya awali kuanza na Ally Ally, kisha Stephen Matata, aliyeondoka kutokana na mwenendo mbovu na aliiongoza katika michezo saba tangu ateuliwe Januari 13, 2025.
Kocha huyo wa zamani wa Sharp Boys inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza visiwani Zanzibar, ana jukumu la kuinusuru na janga la kushuka daraja, baada ya kushinda michezo miwili, sare mitano na kupoteza 18, ikiwa nafasi ya 15 na pointi 11.