Kisarawe. Tanzania iko mbio kuacha kuagiza vipulizi na baruti kutoka nje ya nchi. Kila mwaka Tanzania inaagiza vilipuzi milioni 10 na tani 26,000 za baruti kutoka nje.
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema nchi iko mbioni kuachana na uagizaji wa bidhaa hiyo kutoka nje ya nchi.
Amesema Kiwanda cha Solar Nitrochemicals Limited kilichozinduliwa leo Jumapili, Aprili 13, 2025 kitakuwa na uwezo wa kuzalisha bidhaa hiyo zaidi ya mahitaji.
Akizindua kiwanda hicho kilichogharimu Sh19 bilioni, Waziri Mavunde amesema kitazalisha tani 22,000 za baruti na vilipuzi milioni 15 kwa mwaka.

“Tunaelekea kuacha kuagiza vipulizi na baruti kutoka nje,” amesema Mavunde wakati wa uzinduzi wa kiwanda hicho kilichopo eneo la Visegese, Kisarawe mkoani Pwani.
Amesema kiwanda hicho ni cha kwanza kuzalisha kiwango kikubwa cha baruti na vipulizi nchini na kwamba, uzalishaji huo utaogeza pato la Taifa kupitia sekta ya madini.
“Mwaka 2022/23 sekta ya madini ilichangia kwa asilimia 7.2, mwaka 2024 ilichangia kwa asilimia 9.0 na mwaka huu malengo ni kufika asilimia 10,” amesema.
Amesema sekta ya madini inategemea baruti na vilipuzi, hivyo uwepo wa kiwanda hicho nchini utasaidia upatikanaji wa bidhaa hiyo kwa urahisi.
“Uzalishaji wa baruti kwenye kiwanda hiki ni asilimia 95 ya mahitaji,” amesema Mavunde.
Amesema kupitia kiwanda hicho, Tanzania pia itaanza kuuza vipulizi na baruti kutoka nje ya nchi, hivyo kuingiza fedha za kigeni na kuongeza ajira na kukuza sekta ya viwanda.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Solar Nitrochemicals Limited, Milind Deshmukh amesema kiwanda hicho kimetoa ajira 300 za moja kwa moja.
Amesema matarajio ni kutoa ajira zaidi huku Mavunde akishauri katika mnyororo wa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, wananchi wa Kisarawe wapewe kipaumbele.
Mkurugenzi mkazi wa kiwanda hicho, Kishor Bhomale amesema uwekezaji huo umezingatia miaka mingi ijayo.

Amesema uzalishaji wa vipulizi na baruti kiwandani hapo utakuwa na tija kwa nchi, kwa kuwa utapunguza gharama na kuleta unafuu wa bidhaa kufika sokoni.
“Pia, Tanzania itakuwa ni kitovu cha kufikia masoko ya baruti na vipulizi kwa nchi jirani,” amesema.
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Tito Magoti amesema wilaya hiyo ni ya viwanda akibainisha changamoto waliyonayo ni barabara na maji, akimuomba Mavunde kufikisha changamoto hiyo kwa Waziri wa Maji, Juma Aweso na Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega.
Hata hivyo, Mavunde amesema kupitia mbunge wa Kisarawe, Dk Suleiman Jaffo ambaye ni Waziri wa Viwanda na Biashara watalifikisha jambo hilo kwa mawaziri wa ujenzi na maji.