Wachezea misitu, wanyooshewa kidole | Mwananchi

Dar es Salaam. Wakati takwimu zikionesha takriban hekta 460,000 za misitu zinapotea nchini kwa mwaka, wanaojihusisha na shughuli za uharibifu ikiwemo kukata miti wameonywa na kutakiwa kuacha tabia hiyo mara moja.

Kupotea huko kunasababishwa na shughuli za kibinadamu ikiwemo uchomaji moto, ukataji miti kwa ajili ya kuchoma mkaa na mbao zinazofanywa na wenye nia ovu na mazingira.

Akizungumza wakati wa shughuli ya upandaji miti takriban 3,000 katika eneo la Pugu Mwambisi Dar es Salaam lililofanywa na Shirika la Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF), Msaidizi wa Misitu kutoka Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), Ramadhan Mnaguzi amesema shughuli za uharibifu hazipaswi kufumbiwa macho.

“Wadau wa mazingira kama hawa wakishapanda miti ili kurejesha eneo la misitu lililoharibika, katika kutunza sisi tunafanya doria wale wanaofanya uharibifu tunawakamata tunawapeleka katika vyombo vya sheria,” amesema.

Amesema wanaoingia kwenye hifadhi bila taarifa maalumu wanawafuatilia na kuwakamata, lengo ikiwa ni kuokoa misitu inayopotea kutokana na shughuli za kibinadamu.

“Tunapambana na uchomaji wa moto hasa katika kipindi cha Agosti majani yanapokuwa yamekauka. Tunapambana nao kwa kuwapa elimu na tunaowabaini tunawakamata,” amesema Mnaguzi.

Aidha amewataka wote wanaojihusisha na shughuli hizo kuacha kwani zinaharibu misitu, huku madhara yake yakiwa ni makubwa.

Meneja Mradi wa uhongoaji wa misitu Ukanda wa Usambala Mashariki (WWF), Dk Thomas Sawe amesema kupitia kampeni ya ‘Ishi Kijani-Ishi Kijanja’ ina lengo la kushirikisha vijana katika kuhongoa maeneo yaliyoharibiwa kutokana na shughuli za kibinadamu.

“WWF inatekeleza malengo ya nchi ya kuhongoa maeneo yaliyoharibika ambayo ni ardhi hekta 5.2 milioni na katika malengo haya WWF inasaidia Serikali ardhi yenye ukubwa wa hekta 2.6 milioni,” amesema.

 “Tafiti zinasema kiasi kikubwa cha eneo duniani kimefanyiwa uharibifu kutokana na shughuli za kibinadamu. Katika ngazi za mabara kuna malengo ya kurejesha maeneo hayo yaliyoharibika, na sisi ndicho tunachokifanya,” amesema.

Amesema shughuli za kilimo kisicho endelevu, uchomaji moto, ufugaji holela, ukataji miti kwa ajili ya mbao, mkaa, nguzo na kukosekana kwa utashi na ushirikishwaji katika utunzaji wa maeneo ya misitu vinasababisha uharibifu mkubwa.

Amesema wanachokifanya wanaisaidia Serikali kurejesha maeneo yaliyoharibiwa na kuhifadhi yaliyopo. Ameongeza kwamba miti waliyoipanda wanaifuatilia ikue kama inavyotakiwa.

“Tunashirikiana na TFS wametupa eneo hili tumepanda miti 3,000 lengo ni kutunza maeneo ya misitu. Tafiti zinaonesha mikoa ya kusini ndio inaongoza kwa upotevu mkubwa wa maeneo ya misitu.

Mmoja ya wapandaji miti, Gillia Lyimo amesema kama kijana wanashirikiana na wadau ili kuokoa uoto wa asili na misitu inayopotea. Amesema watu wote wanapaswa kulinda mazingira na kuhakikisha yanakuwa sawa.

Naye, Hussein Jaffar mkazi wa Kisarawe, amesema nguvu inahitajika kutunza miti.

Related Posts