Wazabuni wazawa watengenezewa njia kunufaika fursa za sheria mpya

Bagamoyo. Wakati Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) ikija na mfumo wa kidijitali wa ununuzi wa umma (Nest), mamlaka hiyo imewasihi wazabuni wazawa na wafanyabiashara kote nchini kujisajili.

PPRA imesema wazawa wakijisajili watanufaika na fursa zinazotolewa kupitia maboresho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023.

Kwa mujibu wa PPRA, sheria hiyo mpya imetoa fursa pana kwa wazabuni kushiriki katika zabuni zenye thamani ya hadi Sh50 bilioni, huku makundi maalumu ya wanawake, vijana, wazee na watu wenye ulemavu wakipewa nafasi ya kushindania kazi za hadi Sh500 milioni.

Akizungumza mkoani Pwani wakati wa kufunga mafunzo ya siku nne juu ya uelewa wa sheria na kanuni za ununuzi wa umma, yaliyofanyika wilayani Bagamoyo, Meneja wa Kanda ya Pwani wa PPRA, Vicky Molel, amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wadau kutoka taasisi za umma kuhusu mabadiliko yaliyofanywa kwenye sheria hiyo.

“Sheria mpya imeweka misingi madhubuti ya uwazi, ushindani na usimamizi bora wa mikataba ya manunuzi. Tunawahimiza wazabuni wote, hususan wa ndani, kujisajili katika mfumo huo ili waweze kufaidika na fursa hizi kubwa,” amesema Molel.

Ameongeza kwamba sheria imeimarisha majukumu ya Bodi ya Zabuni na imeweka bayana wajibu wa watumiaji wa mwisho kwenye taasisi nunuzi, ikiwa ni pamoja na uwajibikaji wa moja kwa moja kwenye usimamizi wa mikataba.

“Kwa mfano, mtumiaji wa mwisho sasa ana jukumu la kufuatilia utekelezaji wa mkataba kwa karibu, jambo ambalo awali lilikuwa halipewi uzito mkubwa,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Meneja wa kujenga Uwezo na Huduma za Ushauri kutoka PPRA, Gilbert Kamde, amesema sheria imeweka utaratibu wa haki kwa wazabuni, wakiwemo wale wanaoweza kuwa na mashaka na mchakato wa utoaji wa zabuni.

“Sheria hii inatambua haki ya kila mzabuni. Endapo kuna kutoridhishwa na mchakato wa manunuzi, kuna utaratibu wa kukata rufaa kupitia Bodi ya Rufaa ya Zabuni za Umma (PPAA),” amesema Kamde.

Aidha, baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wameeleza namna yamewajengea uelewa mpya, huku wakisema kuwa mfumo umeleta mabadiliko makubwa katika uwazi na ufanisi wa manunuzi serikalini.

 “Kupitia mfumo huu, sasa tunaweza kufanya manunuzi moja kwa moja kwa uwazi zaidi, na tunaweza kufuatilia hatua kwa hatua mpaka utekelezaji wa mkataba,” amesema Grace Mshana, Ofisa Ununuzi kutoka moja ya taasisi za serikali.

Related Posts