YANGA inajiandaa kushuka uwanjani Jumanne hii kuvaana na Stand United, huku kocha wa timu hiyo akifichua kuwa, kukosekana kwa kiungo wa kati Khalid Aucho, kwa muda wa wiki tatu ndani ya kikosi hicho kunampasua kichwa, ingawa amejipanga na jeshi lake kumalizia mechi zilizosalia kwa kishindo.
Aucho anayeitumikia Yanga kwa msimu wa tatu sasa, amekuwa mhimili wa timu hiyo chini ya makocha wanne tofauti, kuanzia Naserddine Nabi, Miguel Gamondi, Sead Ramovic na sasa Miloud Hamdi na kwa sasa yupo nje ya uwanja kutokana na kuumia nyama za paja wakati wa mchezo dhidi ya Coastal Union.
Kocha Hamdi alisema kukosekana kwa Aucho kunampa wakati mgumu, licha ya kuwepo kwa wachezaji mbadala akiwamo Duke Abuya, Mudathir Yahya, Salum Abubakar, Aziz Andambwile, Jonas Mkude na Shekhan Ibrahim.
Mganda huyo anayecheza kiungo mkabaji huwezi kuona rekodi zake, kama mastaa wengine lakini kazi yake ya kutoa pasi zilizonyooka na kuwachosha wapinzani wasisogee jirani na lango la Yanga imekuwa kubwa ndani ya kikosi hicho na hicho ndicho Hamdi anachokiwaza anapomkosa.
Mwanaspoti iliandika kuwa, Aucho aliyekuwa katika majukumu ya timu ya Taifa Uganda Cranes, alipata majeraha mazoezini wakati wanajiandaa na mechi ya kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Guinea na kushindwa kuucheza mchezo huo.
Hata hivyo, alivyorudi nchini alitumika kwa dakika 45 kabla ya kuomba kutolewa kutokana na kilichoelezwa alijitonesha katika mechi hiyo ya Coastal ambapo Yanga ilishinda kwa bao 1-0, huku rekodi zikionyesha amecheza mechi 19 kati ya 25 akitumika kwa dakika 1502 akifunga bao moja.
Akizungumza na Mwanaspoti, kocha Hamdi alisema ameumizwa na taarifa za Aucho kwani ni mmoja wa askari tegemeo wa kikosi hicho na si rahisi kumkosa kikosini wiki tatu zijazo.
“Aucho ni mchezaji anayejituma, huhitaji kumuuliza kama yuko tayari kucheza kwa sababu wakati wote yuko tayari kuisaidia timu yake,” alisema Hamdi na kuongeza;
“Pia ni kiongozi anapokuwa uwanjani ni pigo kwetu.”