Hatari inayowakabili wanaume wenye matiti makubwa

Wanaume wenye matiti ambayo yametanuka (gynecomastia), wapo katika hatari ya kufa kabla ya kufika umri wa miaka 75, wanasayansi wamebaini.

Watafiti wamefichua kuwa wanaume ambao wana maradhi kama saratani, matatizo kwenye mapafu ambayo hayajagunduliwa na magonjwa mengine sugu,  wapo katika hatari zaidi kufa ikiwa  wana matiti ambayo yametanuka.

Mwanaume kuwa na matiti makubwa, husababishwa na kutosawazishwa kwa homoni muhimu ndani ya mwili. Hali hii inawaathiri theluthi mbili ya wanaume wote duniani japo pia hali hiyo inaweza ikawa inatokana na sababu za kiumri.

Watafiti kutoka Denmark kwenye jarida la BMJ Open wamebaini kuwa tatizo la matiti kuwa makubwa kwa wanaume hukolea sana hasa wakiingia uzeeni.

Huku homoni za kiume nazo zikipungua uzeeni, wanaume wengi huanza kuongeza uzani ambao huhatarisha hali  ya matiti kuongezeka ukubwa.

Katika utafiti huo, ilibainika kuwa wanaume ambao wana matatizo ya afya mapema wakati wa uhai wao kabla ya kutinga uzeeni, wapo kwenye hatari ya kupatwa na tatizo la matiti kutanuka.

Wakati wa utafiti huo, ilibainika kuwa wale ambao wana matiti makubwa wako kwenye hatari ya kufa kabla ya kufika miaka 75 kwa sababu kinga ya mwili wao hudhoofishwa na magonjwa yanayowasibu.

Kuepuka hali hiyo, wanapendekeza kuwa wale ambao wana matatizo mbalimbali ya afya wawe wakifuatilia hali yao na kupokea matibabu mapema.

Hii ni kwa sababu kutanuka kwa matiti huhusishwa sana na matatizo ya baadaye ya afya hasa uzee unapoingia.

“Wanaume wenye matiti yaliyotanuka wapo katika hatari ya kufa kwa asilimia 37. Hoja hapa ni kuwa lazima wawe wanatatizwa na magonjwa mengine yanayolemaza kingamwili yao. Hii ndiyo maana kila mmoja anastahili kupitia uchunguzi wa ndani wa afya kila mara kufahamu magonjwa yanayomwandama na kupokea matibabu,” wamesema watafiti hao.

Habari hii kwa hisani ya Taifa Leo

Related Posts