LATRA YAWEKA REKODI MPYA YAJIVUNIA MAKUBWA AWAMU YA SITA, YATOA LESENI LUKUKI

 *****

MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imesema kuwa, katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan kuanzia mwezi Februari, 2021 hadi mwezi Machi 2025 imetoa leseni 108,658 za usafirishaji.

Hayo yamesemwa leo Aprili 14,2025 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA),CPA Habibu Suluo katika kikao kazi na wahariri, waandishi wa habari nchini,chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).

“Kwa mujibu wa Kifungu cha 5(1)(b) cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini,Sura ya 413, LATRA ina wajibu wa kutoa, kuhuisha, kusitisha na, au kufuta leseni za usafirishaji.”

CPA Suluo amesema,leseni za usafirishaji zilizotolewa kwa vyombo vya usafiri wa abiria, mizigo na vyombo vya usafiri wa kukodi ziliongezeka kutoka 226,201 mwaka 2020/21 (Februari, 2021) hadi 334,859 mwaka 2024/25 (Machi, 2025).

“Ikwa ni ongezeko la leseni 108,658, sawa na ongezeko la asilimia 48. Hili ongezeko ni sawa na wastani wa ongezeko la asilimia 12 kila mwaka katika kipindi cha miaka minne.”

Wakati huo huo, CPA Saluo amesema,LATRA imeendelea kuboresha usafiri wa umma katika miji na majiji makubwa hapa nchini.

Pia, amesema LATRA imeanzisha njia mpya 1,007 za daladala mkoani Dar es Salaam ili kufika maeneo yasiyofikika na kurefusha baadhi ya njia kwa lengo la kumpunguzia gharama mwananchi.

CPA Suluo amesema,njia za usafiri wa mabasi ya mijini zilizorefushwa kwa upande wa Dar es Salaam ni Mbezi Luis-Kisarawe kupitia barabara ya Malamba Mawili, Banana.

Nyingine ni Toangoma-Pugu Stesheni kupitia barabara ya Kilwa, Nyerere ikiwemo Kivukoni-Bunju Sokoni kupitia Barabara ya Bagamoyo.

Ametaja njia nyingine kuwa ni Gerezani-Bunju Sokoni kupitia Barabara ya Bagamoyo, Buyuni Sokoni-Stendi Kuu ya Magufuli kupitia Kinyerezi.

Vilevile Bunju Sokoni-Stendi Kuu ya Magufuli kupitia Madale,Mbande Kisewe-Gerezani kupitia Barabara ya Kilungule, Chang’ombe, Usalama,Mvuti-Machinga Complex na Tabata Segerea.

CPA Suluo amesema, njia nyingine ni Ngobedi B-Machinga Complex kupitia Nyota Njema, na Kitonga-Gerezani kupitia barabara ya Kilwa.

Katika hatua nyingine, CPA Saluo amesema, kwa Arusha mamlaka imefanya mabadiliko ya njia za daladala kwa kuzifanya baadhi ya njia kuwa za mzunguko kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa huduma kwenye baadhi ya maeneo ambayo hayakuwa na huduma.

“Mfano ni njia inayoanzia Kwa Mrombo kupitia Impala, Philips, Sanawari, Chuo cha Ufundi Arusha hadi ‘Fire’ na kurudi kwa Mrombo.”

Akizungumzia kwa upande wa Jiji la Dodoma ambayo ni makao makuu ya nchi,CPA Saluo amesema,zimeanzishwa njia mpya kwa ajili yakuyafikia maeneo mapya ya makazi mapya kutokana na kukua kwa kasi kwa jiji hilo.

“Mfano wa njia hizo ni Machinga Complex-Njedengwa, Machinga Complex-Mpamaa, Machinga Complex-Chidachi, Machinga Complex-Nzuguni, Machinga Complex-Swaswa na Vyeyula-llazo.”

CPA Suluo amesema,hatua ya kuhamishia daladala kituo cha Machinga Complex imesaidia kuwepo kwa njia za mzunguko katikati ya Jiji la Dodoma na hivyo kuongeza upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

Amesema,mzunguko huo ni kuanzia barabara ya Hospitali kupitia Majengo Sokoni hadi Machinga Complex kisha kupitia Uwanja wa Ndege na kurudi mjini.

Katika Jiji la Mwanza,CPA Saluo amesema, zimeanzishwa njia ndefu kwa ajili ya kuyafikia maeneo mapya ya makazi na kukua kwa kasi kwa Jiji la Mwanza.

“Mfano wa njia hizo ni kutoka Usagara-Kisesa kupitia Buzuruga,llalila-Misungwi kupitia Buzuruga,Nyashishi-TX kupitia Kiseke-PPF, Nyashishi -Kisesa Kona ya Kayenze kupitia Meccov) Nyashishi -llalila kupitia Buzuruga, Mwanza mjini-lgombe, Mwaloni-Kona ya Kayenze na Mwaloni-Kabusungu.”

Related Posts