Longido. Wananchi 37,752 wa kata za Sinya, Namanga na Kimokoua, wilayani Longido Mkoa wa Arusha, wanatarajia kuondokana na adha ya maji kufuatia ujenzi wa mradi wa maji wa zaidi ya Sh13.5 bilioni.
Mradi huo wa muda wa miaka miwili unatarajiwa kukamilika Juni 2027 unatekelezwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Jiji la Arusha (Auwsa).
Akizungumza wakati wa utiaji saini wa mradi huo wa Sinya-Namanga leo Jumatatu Aprili 14,2025 katika Kijiji cha Ildonyo, Kata ya Sinya, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amewaonya makandarasi wanaotekeleza miradi mbalimbali mkoani humo kutekeleza kwa wakati.
Amesema Serikali haitasita kuwachukulia hatua wanaokiuka mikataba.
Amesema maji ni miongoni mwa huduma muhimu katika jamii na ndiyo maana Serikali imeamua kutekeleza mradi huo ili kupunguza changamoto ya wananchi kutembea umbali mrefu kufuata maji.
“Maji ni uchumi uhai na siasa yakikosekana hali inakuwa tete niwatake mkandarasi ambaye atafanya kazi kwenye huu mkoa ambao unaongozwa na Makonda kwanza mfahamu sina aibu naheshimu makubaliano tumeambiwa mradi wa miaka miwili.
“Ili ujipatie heshima na upate kazi nyingine kwenye mkoa ufanye kazi ndani ya muda tutakuona ni tumaini letu, wananchi wamesubiri maji na kama ni kutiwa moyo wametiwa sana kama ni matumaini walipewa sana, makandarasi fanyeni kazi kwa wakati,”
“Kazi za kusukumana sio nzuri ukiwa mkandarasi kwenye huu mkoa tukakukumbusha wajibu wako ukianza kwenda kinyume tutakutafutia Kituo cha Polisi karibu ili ufanye kazi kwa wakati, utakuwa unakaa polisi asubuhi unaenda kwenye mradi sina mkataba, urafiki, ushirika na watu wanaopoteza heshima ya kazi niliyopewa,” ameongeza
Makonda amewataka wananchi wa Longido kutokuwa kikwazo cha kufanyika kwa mradi huo na kuwa wakiwa kikwazo lawama zitatupiwa Serikali.
Kuhusu uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani unaotarajiwa kufanyika mwaka huu, aliwataka wananchi kutokukubali kuchagua viongozi kwa sababu ya rushwa.
Awali akitoa taarifa ya mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Auwsa, Mhandisi Justine Rujomba, amesema katika kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa maji na kukidhi mahitaji, mamlaka hiyo ilifanya utafiti na kubaini eneo linalofaa kwa uchimbaji wa kisima kirefu.
Amesema eneo hilo limeonyesha ufanisi kwa uchimbaji kisima kirefu chenye uwezo wa kuzalisha lita milioni 2.4 za maji kwa siku.
Mhandisi huyo amesema Auwsa inatoa huduma ya maji katika kata tano za wilaya ya Longido ambapo chanzo cha maji hayo ni kutoka Mto Simba, uliopo wilayani Siha na kuwa inazalisha maji lita milioni 1.7 kwa siku, huku mahitaji yakiwa lita milioni 3.8 kwa siku.
“Baada ya kukamilika kwa mradi huu uzalishaji utaongezeka hadi kufikia lita milioni 4.1 kwa siku. Katika mradi huu miongoni mwa shughuli zitakazofanywa ni kufunga miundombinu ya umeme na ujenzi wa kituo cha kusukuma maji katika Kijiji cha Ildonyo,” amesema.
Mkurugenzi huyo ametaja shughuli nyingine ni kujenga bomba la kusafirisha maji, matenki ya kukusanya maji Namanga, Sinya na Oldonyo na kujenga mitandao ya mabomba ya kusambaza maji Kata za Sinya na Namanga.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi hao, Lekule Laizer, amesema akina mama walikuwa wakiteseka kwa muda mrefu kutokana na kukosa huduma hiyo muhimu ya maji karibu na makazi yao.
“Nimekuwa mbunge wa jimbo hili kwa muda mrefu, najua adha ya maji inayokabili wananchi wa Sinya, wametaabika kwa muda mrefu, leo tunapongeza Serikali kwa kufanya kazi kubwa ya kuwakomboa wananchi na kuwatua akina mama ndoo kichwani,” amesema
Naye Laizer Melipa, amesema awali walikuwa wakiteseka na mifugo ilikuwa haiuziki hasa msimu wa kiangazi kwa kukosa maji na malisho, kwani ilikuwa inapungua uzito hivyo wana matumaini na mradi huo.