Matatani kwa tuhuma za kutoa taarifa za uongo

Unguja. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi linamshikilia Abdallah Ramadhan Mnolwa (24) kutoka Iringa kwa tuhuma za kutoa taarifa za uongo.

Hayo yameelezwa leo, Jumatatu Aprili 14, 2025 na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Abubakar Khamis Ally, alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Madema.

Amesema mtuhumiwa huyo alifika kituo cha Polisi Madema na kutoa taarifa kuwa akiwa Darajani, Wilaya ya Mjini, alilawitiwa na vijana wawili wenye asili ya Kiarabu na kudai kuwa anawafahamu kwa sura.

“Aprili 10, 2025, majira ya saa 3 asubuhi, mtuhumiwa alifika kituo cha Polisi Madema na kutoa taarifa kuwa akiwa huko Darajani, Wilaya ya Mjini, alilawitiwa na vijana wawili wenye asili ya Kiarabu, ambao alidai anawafahamu kwa sura,” amesema Kaimu Kamanda Abubakar.

Amesema kijana huyo alieleza kuwa chanzo cha tukio hilo ni baada ya kutelekezwa na mwenyeji wake, ndipo vijana hao walijitokeza kumpa msaada, lakini mwishowe walimfanyia ukatili huo.

Hivyo, Jeshi la Polisi lilifungua kesi ya kosa la kulawiti na kijana huyo alipelekwa Hospitali ya Mnazi Mmoja kwa ajili ya vipimo, na baada ya uchunguzi wa kitabibu, ilibainika hakuwa ameingiliwa kama alivyodai.

Kaimu Kamanda Abubakar amesema licha ya majibu hayo, mtuhumiwa huyo alisisitiza kukamatwa kwa watuhumiwa wake, huku akipiga simu kwa viongozi mbalimbali kuhusu kutokamatwa kwa watuhumiwa hao na kudai kuwa amekosa ushirikiano kutoka Jeshi la Polisi.

Amesema baada ya mahojiano na mtuhumiwa huyo, ilibainika kuwa taarifa hizo ni za uongo, na mtuhumiwa huyo alishawahi pia kufanya tukio kama hilo Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Hivyo, Jeshi la Polisi limetoa onyo kwa yeyote atakayetoa taarifa zenye kuleta taswira mbaya kwa nchi, kwamba atachukuliwa hatua za kisheria dhidi yake.

Related Posts