Dodoma. Mbunge wa Kerwa (CCM), Innocent Bilakwate ameshauri Serikali kushusha bei ya usafiri wa treni ya kisasa ya (SGR) kwa mabehewa ya watu mashuhuri (VIP) ili kuepuka kupata hasara inayotokana baadhi ya viti kwenda bila watu.
Bilakwate ameyasema hayo leo Jumatatu Aprili 14, 2025 wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2025/26.
Mjadala huo ulianza Aprili 9, 2025 baada ya Majaliwa kuomba kuidhinishiwa na Bunge Sh782.08 bilioni kwa ajili ya taasisi yake na Mfuko wa Bunge katika mwaka 2025/26.
Mbunge huyo amesema kukamilika kwa mradi huo wa SGR umerahisisha maisha kwa watu kufika mapema wanapotaka kwenda na kurudi Dodoma.
Hata hivyo, amesema mabehewa ya VIP yakuwa na watu 20 lakini wakati mwingine hata watu 10 , hali hiyo inatokana na gharama kubwa za usafiri ambazo ni Sh150,000.
“Nashauri Serikali kama behewa linalotakiwa kubeba abiria 40 lakini linabeba watu 20, 15 na wakati mwingine hadi 10. kwa nini Serikali isiamue kupunguza nauli kama ni Sh150,000 ikawa Sh70,000,” amesema.
Amesema kwa kufanya hivyo kunaweza kuongeza pato kwa Serikali kuliko kuacha bei kubwa halafu abiria wanakuwa wachache.
Usafiri wa SGR unatolewa na Shirika la Reli Tanzania (TRC) kutoka Dar es salaam- Morogoro hadi Dodoma. Ulizinduliwa Alhamisi ya Agosti 1, 2024 na Rais Samia Suluhu Hassan.
Kwa mujibu wa TRC, bei za VIP zipo za viwango tofauti zikiwemo za Sh120,000 hadi Sh150,000 kwa safari za Dar es Salaam – Dodoma.