Sh7.3 bilioni kukarabati daraja Songwe

Songwe. Serikali imesema inatarajia kuanza  utekelezaji wa ujenzi wa daraja katika barabara ya Mlowo-Kamsamba  ili kuondoa changamoto inayowakabili wananchi baada ya lililokuwapo awali kuathiriwa na mvua za Eli-nino ambapo zaidi ya Sh7.3 bilioni zitatumika.

Hayo yamebainishwa na Meneja wa Wakala wa Barabara (Tanroad) Mkoa wa Songwe,  Suleiman Bishanga wakati wa ziara ya ugeni kutoka Benki ya Dunia uliofika eneo hilo kukagua maendeleo ya mradi huo.

Mhandisi Bishanga amesema mradi huo unatekelezwa kwa fedha za Serikali kutoka Benki ya Dunia zilitolewa kupitia Wizara ya Ujenzi chini ya Waziri Abdallah Ulega.

Amesema mradi huu  unatekelezwa na mkandarasi Abemulo Contractor kwa gharama ya zaidi ya Sh7.3 bilioni, unalenga kuhakikisha daraja lenye urefu wa mita 60 pamoja na maingilio ya mita 500 kila upande linajengwa kwa ubora na kukamilika kwa wakati ambapo hadi sasa, utekelezaji wake umefikia takribani asilimia 15.

Bishanga amebainisha kuwa Benki ya Dunia imeridhishwa na maendeleo ya mradi huo na imepongeza Serikali ya Tanzania kwa usimamizi mzuri wa fedha zinazotolewa, huku wakieleza kuridhika kwao na hatua zilizochukuliwa kuondoa kero ya muda mrefu kwa wananchi wa maeneo hayo.

Amesema kukatika kwa mawasiliano kwenye barabara hiyo kulikuwa kunasababisha wananchi kukaa saa zaidi ya sita kuelekea Mlowo au Kamsamba kwani maji yalikuwa yanajaa na wananchi kushindwa kuvuka vikiwemo vyombo vya usafiri.

Meneja wa Tanroad Mkoa wa Songwe Mhandisi Suleimani Bishanga akitoa maelekea kwa wageni kutoka benki ya Dunia waliotembelea ujenzi wa daraja la Barabara ya Kamsamba_Mlowo

“Mradi huu pia ni sehemu ya maandalizi ya ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami kutoka Mlowo hadi Kamasamba, ambapo kilomita tano zitajengwa kutoka kila upande ambapo Ujenzi huu unatarajiwa kuimarisha biashara, usafirishaji na kuinua uchumi wa wananchi katika maeneo ya Songwe, Rukwa hadi Zambia ,”amesema Mhandisi Bishanga.

Aidha, ametoa rai kwa wananchi kuutunza mradi huo, kuvilinda vifaa na miundombinu inayoendelea kujengwa kwa sababu ni kwa manufaa yao moja kwa moja na kuahidi kuwa Tanroads watausimamia mradi huu, kwa bidii kuhakikisha unakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa ifikapo Novemba 21, 2025 kama ilivyopangwa.

Mkazi wa eneo hilo, Mariamu Mwasawalo amesema walikuwa wanakumbwa na changamoto ya mawasiliano pindi daraja hilo linapokatika kutokana na mvua nyingi kunyesha, hivyo ujenzi wa daraja hilo ukikamilia utawaondolea adha ya kukaa zaidi ya saa sita wakisubiri maji yapungue wavuke.

Related Posts