LIGI Kuu Bara imesimama kwa muda, lakini hiyo haina maana uhondo wa soka haupo kwani leo kwenye viwanja viwili tofauti, kuna vita nzito ya timu za ligi hizo zitakazoonyeshana kazi katika mechi za robo fainali za michuano ya Kombe la Shirikisho (FA).
Maafande wa JKT Tanzania waliopo nafasi ya sita katika msimamo wa Ligi Kuu, watavaana na Pamba Jiji wakati Singida Black Stars itakuwa mwenyeji wa Tabora United, kila moja ikipiga hesabu za kutinga nusu fainali za michuano hiyo inayotoa mwakilishi wa nchi katika Kombe la Shirikisho Afrika.
JKT itakuwa mwenyeji wa Pamba kwenye Uwanja wa Meja Isamuhyo, huku ikifika hatua hiyo kwa kuitoa Igunga Utd katika 64 Bora kwa mabao 5-1, kisha ikaing’oa Biashara Utd iliyopo Ligi ya Championship katika hatua ya 32 Bora kwa kuifunga 2-1 na ilipotinga 16 Bora iliiondosha Mbeya Kwanza kwa 3-0.
Kwa upande wa Pamba, ilianza michuano kwa kuichapa Moro Kids iliyopo First League kwa bao 1-0, kisha kuinyoa Kiluvya United katika hatua ya 32 Bora kwa mabao 3-0 na katika 16 Bora iliitambia Mashujaa kwa ushindi wa bao 1-0.
Mara ya mwisho timu hizi zilipokutana katika Ligi Kuu kwenye Uwanja wa Isamuhyo, Desemba 11, mwaka jana zilishindwa kutambiana kwa kutoka suluhu, jambo linalosubiriwa kuona ni ipi itakata tiketi ya kwenda nusu fainali na kuvaana na mshindi wa mechi ya kesho kati ya Yanga na Stand United.
Kocha wa JKT, Ahmad Ally alisema moja ya kazi kubwa alizofanya kwenye uwanja wa mazoezi kabla ya mchezo huo ni jinsi ya kupambana na timu zinazoshambulia zaidi kutokea pembeni, jambo lililompa shida katika mechi mbili za ligi zilizopita.
“Mchezo wetu na Dodoma Jiji na wa mwisho pia dhidi ya Namungo tulipata shida sana, kwa Pamba wanategemea aina hiyo ya ushambuliaji kupitia pembeni hivyo, ni lazima tuweke mikakati mizuri ya kuhakikisha hatuwapatii nafasi,” alisema Ahmad.
Kwa upande wa Fred Felix ‘Minziro’ anayeinoa Pamba Jiji, alisema mchezo wa mtoano siku zote huwa ni mgumu kutokana na mahitaji ya kila timu, hivyo hatotumia mbinu kama alizotumia katika mechi ya mwisho zilipokutana zaidi ya kucheza kwa tahadhari kubwa.
Mbali na mchezo huo, shughuli nyingine ya kuisaka tiketi ya kutinga hatua ya nusu fainali itapigwa kwenye Uwanja wa Liti, mjini Singida kwa wenyeji Singida BS watakaokuwa na kibarua kigumu cha kupambana dhidi ya Kagera Sugar.
Singida ilianza michuano hiyo kwa kuitoa Magnet ya Dar es Salaam kwa kuichapa 2-0, kisha hatua ya 32 Bora ikawatupa nje tena Mabingwa wa Mkoa wa Kagera, Leo Tena kwa mabao 4-0 na katika 16 Bora ikainyoosha KMC kwa bao 1-0.
Kwa upande wa Kagera iliichapa bao 1-0, Rhino Ranges ya Tabora inayoshiriki First League hatua ya 64 bora, ikaitoa Namungo kwa mabao 3-0, kisha 16 bora, ikaichapa Tabora United kwa penalti 5-4, baada ya sare ya kufungana 1-1 katika dakika 90.
Mchezo wa mwisho kati ya timu hizi katika Ligi Kuu, uliopigwa kwenye Uwanja wa Liti, Februari 7, mwaka huu na uliisha kwa sare ya 2-2, japo mechi ya awali Singida ilishinda 1-0, Agosti 24, 2024.
Kaimu kocha mkuu wa Singida, David Ouma alisema wamejipanga vizuri kukabiliana na changamoto iliyokuwa mbele yao, huku kwa upande wa Juma Kaseja wa Kagera akieleza kupoteza michezo miwili mfululizo iliyopita hakujawatoa katika mstari.
Mbabe wa mechi hiyo atakata tiketi ya kuvaana na mshindi wa mchezo uliopigwa jana kati ya Simba na Mbeya City ili kusaka nafasi ya kutinga fainali kuwania ubingwa unaoshikiliwa kwa misimu mitatu sasa na Yanga inatakayoshuka uwanjani kesho kuvaana na Chama la Wana kwenye Uwanja wa KMC.