WAZIRI wa Ujenzi Abdallah Ulega amesema kuwa Serikali itahakikisha inatoa fedha ili kufanikisha utoaji wa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu ili ziwe endelevu na kufikia malengo yale yaliyokusudiwa hasa ya kukuza lugha ya Kiswahili nchini na duniani kwa ujumla.
Akizungumza jana wakati alipomwakilisha Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk. Philip Mpango katika hafla ya utoaji wa tuzo hizo zinazoratibiwa na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), iliyofanyika ukumbi wa The Super Dome Masaki jijini Dar es Salaam
Amesema utoaji wa tuzo hiyo ya uandishi bunifu katika lugha ya Kiswahili ni ishara ya kuendelea kuenzi utamaduni wa hayati Nyerere Afrika na duniani hivyo anaitaka TET kuhakikisha tuzo hiyo inaendelea kuwa endelevu ili kufanikisha malengo yale yaliyokusudiwa.
“Utoaji wa tuzo za uandishi bunifu katika lugha ya Kiswahili ni ishara ya kuedelea kuikuza lugfha hii na utamduni wake Afrika na duniani kwa ujumla, hata hivyo maandiko bunifu yenye tija ni yale yanayoisaidia jamii katika nyanja mbalimbali ikiwemo kijamii, kiuchumi, kisayansi na tekonolojia, nitoe wito kwa watanzania wezangu kuweza kujitokeza kushiriki kwa kuwasilisha miswada yao ili kushindania tuzo hii.
“Niwapongeze sana washindi wa mwaka huu na wote waliowasilisha miswada yao na wale ambao hawatakuwa washindi niwaombe wasikate tamaa ya kuwania tuzo hii, muhimu muendelee kujifunza muandike nini kwa nanini na wakati gani, serikali yetu itaendelea kutoa fedha za kufanikisha utoaji wa tuzo hii ili iwezeshe kufanikisha malengo makuu,” amesema
Hata hivyo , ameiomba TET ambao ndo waratibu, kuhakikisha tuzo hiyo inatolewa kila mwaka ili kufikia malengo yaliyokusudiwa pia ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kujitokeza kwa wingi kuwasilisha kazi zao ili kushiriki tuzo hiyo.
“Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Nyerere aliendeleza lugha ya Kiswahili kwa kuwa mwandishi bunifu wa mashairi na riwaya hivyo jambo hili la Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu ni la heshima kwani linamuenzi Mwalimu pamoja na kazi zake,” amesema
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dk. Aneth Komba amesisitiza kuwa serikali itagharamia uchapishaji na usambazaji shuleni wa nakala za vitabu vitakavyoshinda tuzo hiyo katika nyanja ya riwaya, ushairi, hadithi za watoto na tamthiliya.
Mwenyekiti wa kamati ya Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere, Profesa Penina Mlama amesema kamati imefurahi kuona mwitikio wa waandishi bunifu kushiriki tuzo hizo umekuwa mkubwa kwani jumla ya miswada iliyopokelewa mwaka huu ni 282 ikilinganishwa na 209 iliyopokelewa mwaka jana na 283 ya mwaka wa kwanza zilipoanza tuzo hizo.
Mlama amesema kwamba kati ya miswada 282 iliyowasilishwa mwaka huu, ya ushairi ilikuwa 114, riwaya 46, hadhiti za watoto 77 na tamthiliya ni 45.
“Hata hivyo kwa mwaka huu jumla ya miswada iliyotimiza vigezo vilivyowekwa ilikuwa ni 205 kati ya 282, naendelea kuwasihi sana waandishi bunifu kuzingatia vigezo vilivyowekwa ili kuepuka kuwasilisha kazi ambazo hazijazingatia vigezo, washiriki wa mwaka huu wametoka katika mikoa yote ya Tanzania na miswada minne imetoka kwa watanzania wanaoishi nje ya nchi,” amesema Mlama
Mlama amesema kati ya washiriki wote wa tuzo hiyo wanawake walikuwa 88 sawa na aslimia 32 na kwamba hilo ni ongezeko kutoka washiriki 62 mwaka jana, aidha amesema mwaka huu wanaume ni 194 ikilinganishwa na 155 wa mwaka jana.