Dodoma. Patachimbika bungeni, ndivyo unavyoweza kusema wakati wabunge wakiwa kwenye kipindi cha lala salama, watakapoichambua bajeti ya Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ambayo ni wizara mtambuka inayobeba maeneo mengi ikiwemo afya, elimu na miundombinu.
Bunge hilo la 12 ambalo uhai wake utagota Juni 27, 2025 kwa Rais Samia Suluhu Hassan kulihutubia na kulivunja, kwa sasa wabunge wanajadili hotuba mbalimbali za wizara. Tamisemi ni moja ya wizara ambazo zinatarajia kushuhudia mjadala mkali.
Mjadala huo unatokana na maeneo inayosimamia kama afya, miundombinu hususan ya barabara na elimu yakishikilia kura zao kwa wananchi kutokana na ahadi mbalimbali walizoziwasilisha wakati wakiomba kura mwaka 2020.
Bajeti hiyo ya Waziri Mohamed Mchegerwa anatarajia kuisoma Jumatano ya Aprili 16, 2025 na wabunge wataijadili kwa siku tatu na itahitimishwa Jumanne ya Aprili 22, 2025. Katikati hapo Bunge litasimama kupisha sikukuu ya Pasaka.
Waziri Mchengerwa atawasisha bajeti hiyo baada ya ile ya Ofisi ya Waziri Mkuu itakayohitimishwa Jumanne hii ya Aprili 15, 2025. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliwasilisha bajeti yake Aprili 9, 2025 na inajadiliwa kwa siku tano.
Waziri Mchengerwa atakutana na kibarua cha hoja kama ujenzi wa barabara zilizo chini ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura), ambayo wabunge wamekuwa wakilalamikia inatengewa fedha kidogo lakini hazifiki kwa wakati.
Suala la ujenzi wa barabara limekuwa mwiba kwa mawaziri na katika majibu ambayo Naibu Waziri wa Tamisemi, Zainabu Katimba kwenye maswali ya msingi na nyongeza linachukua nafasi kubwa.
Hata hivyo uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu kwa upande wa wabunge unaongeza joto kwa kuwa wengi ilikuwa ni sehemu ya ahadi zao katika kufungua njia za vijijini, ingawa Serikali ilishatenga Sh5 bilioni kwa kila mbunge ili akafungue barabara anayoona ingesaidia kuunganisha jimbo ambapo tayari fedha hizo zilishaanza kutolewa.
Mchengerwa anasubiriwa katika suala la uhaba wa watumishi maeneo mbalimbali hususan wa afya na elimu ingawa wengi wanaonekana kujazana mjini kwa visingizio vya ugonjwa ama ndoa.
Mfano halisi ni Jiji la Dodoma ambapo watendaji wa mitaa wanaonekana kujaa zaidi hata kuwa na akiba, lakini baadhi ya maeneo ikiwemo wilaya ya Mpwapwa vijiji vingi wanakaimu walimu na vijana wasioajiriwa.
Kwa eneo hilo kipo kilio cha madarasa kwa nafasi za watumishi hasa kada ya ualimu, ambayo wagombea wengi mwaka huu kupitia Chama cha Walimu (CWT) wamekuwa wakitembelea hoja hiyo.
Jambo jingine ni ujenzi wa zahanati na umaliziaji wa maboma ambayo Serikali imekuwa ikitangaza wakati wote kuwa imeshapeleka fedha lakini maeneo mengi bado licha ya wananchi kutumia nguvu zao kuanzisha ujenzi.
Ukarabati wa maboma unachukua nafasi kubwa kwani mwishoni mwa juma mbunge wa Tabora Kaskazini, Almas Maige aliibua hoja hiyo kwenye swali la msingi ambapo wabunge wengi walisimama kutaka kuchangia katika eneo hilo.
Siku mbili za Mchengerwa zitakuwa za moto kwa sababu hii ni bajeti yake ya mwisho katika Bunge la 12 na wabunge wanajiandaa kwenda kwenye uchaguzi jambo linalofanya kila mmoja ajaribu kuonyesha analisemea jimbo lake.
Suala jingine linaloweza kuibuliwa na wabunge ni migogoro baina ya wakuu wa mikoa, wilaya, makatibu tawala wa mikoa na wilaya ama wakurugenzi ambao baadhi hawaelewani na wengine kutumia madaraka yao vibaya dhidi ya wenzao ama wananchi.
Licha ya ukweli kuwa hotuba yake ilikuwa imejaa pongezi na maombi ya kutaka akagombee tena, Waziri Mkuu, Majaliwa anatakiwa kuwaridhisha wabunge kwenye maeneo machache ambayo walitaka majibu.
Hoja tano ambazo ziliibuliwa na wabunge katika hotuba yake ni suala la ajira kwa vijana, utitiri wa mifuko ya uwezeshaji, usalama wa chakula na umri wa kukopesha vijana (wa kiume, mikopo ya asilimia 10) ambao licha ya kuongezwa kutoka mwisho miaka 35 na kuwa 45 lakini wabunge wanataka kusiwe na kikomo.
Mbunge wa Vunjo (CCM), Dk Charles Kimei, alipendekeza iundwe mamlaka kusimamia mifuko ili ijulikane badala ya kubaki ule wa asilimia 10 ya mikopo ya Serikali.
Wabunge waliibua hoja ya utitiri wa mifuko ya uwezeshaji wananchi wakisema kuwa mingine haijulikani hivyo wakapendekeza iundwe timu maalumu kwa ajili ya kuchunguza.
Hoja ya mifuko ya uwezeshwaji ilichukua uzito baada ya Mbunge wa Viti Maalumu, Sylvia Sigula kuliambia Bunge kuwa mifuko ya mikopo ya moja kwa moja ipo 22 na ile ya ruzuku 26, lakini vijana hawaifahamu na hawana mtu wa kuwafahamisha jambo linalowasukumwa kwenda kwenye mikopo yenye masharti magumu.
“Mheshimiwa Spika, mifuko ya mikopo ya vijana ya moja kwa moja ipo 22 na ile ya ruzuku inafikia 26 lakini nani anajua, ni kwa sababu imejificha, tunaomba Serikali iweke mazingira mazuri ya kuitambua na jinsi ya kuwasaidia vijana,” alisema.
Kwenye hoja ya ajira moto uliwaka baada ya Mbunge wa Sumve (CCM), Kasalali Mageni kueleza namna vijana wanavyohangaika kupata ajira na wanaozipata hupitia kitu kinachoitwa ‘koneksheni.’
“Hivi ajira hatujui mfumo wake ukoje, mara nyingi vijana wanahangaika sana zikishatangazwa kila mmoja anaomba msaada na kwa kweli simu za wabunge zimejaa jumbe fupi za kuomba wasaidiwe kupata ajira,” alisema Mageni.
Hoja nyingine ilikuwa na sifa na pongezi kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakimtaka agombee tena ili arudi bungeni Novemba 2025 kwa sababu anatajwa kuwa ni msikivu na mnyenyekevu.
Mbunge wa Bunda, Mwita Getere alisema:“Nenda kagombee na wananchi wa Ruangwa wakulete bungeni, suala la vyeo Mungu ndiye anapanga.”
Kuhusu kugombea bila shaka Waziri Mkuu hatakuwa na majibu zaidi ya kusema atagombea, kwani alishawaambia wapiga kura wake kwamba anaomba mitano mingine ili aendelee kuwasemea.