CHAMA CHA MAWAKILI WA SERIKALI CHAPIGA HATUA KUBWA KWA ONGEZEKO LA WANACHAMA

Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Doto Biteko akimkabidhi tuzo Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza Johari kwa mchango wake kama mlezi wa Chama cha Mawakili wa serikali kwenye mkutano wa Chama hicho uliofanyika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma Aprili 15, 2025.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza Johari, amesema kuwa Chama cha Mawakili wa Serikali akizungumza katika mkutano mkuu wa mwaka wa Chama cha Mawakili uliomalizika leo Aprili 15, 2025 kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

……………. 

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Dodoma – Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza Johari, amesema kuwa Chama cha Mawakili wa Serikali kimepata mafanikio makubwa, ikiwa ni pamoja na ongezeko la wanachama kutoka zaidi ya 2,000 mwaka 2022 hadi kufikia zaidi ya 3,000 mwaka 2025.

Mhe. Johari aliyasema hayo leo jijini Dodoma wakati akizungumza kwenye Mkutano Mkuu wa Chama cha Mawakili wa Serikali, unaoendelea kufanyika katika jiji hilo.

“Chama hiki kilizinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan mnamo Septemba 29, 2022, na tangu wakati huo kimeleta mafanikio makubwa, hususan katika kuongeza wanachama,” alisema Mhe. Johari.

Aliongeza kuwa moja ya malengo yao ni kukifanya chama hicho kuwa chenye mvuto ili kuwavutia wanachama wa heshima zaidi, kwa kuwa ni chama kikubwa na chenye mchango mkubwa kwa taifa.

Aidha, alieleza kuwa tangu kuzinduliwa, chama hicho kimefanikiwa kupata waraka wa idhini ya malipo ya posho na stahili kwa mawakili wa serikali na maafisa sheria wanaotekeleza majukumu yao katika wizara, idara zinazojitegemea, taasisi za umma, wakala wa serikali, TAMISEMI pamoja na serikali za mitaa.

“Kwa mujibu wa waraka huo, kuanzia Julai 1, 2024, mawakili wa serikali na maafisa sheria watalipwa posho mbalimbali ikiwa ni pamoja na posho ya vazi maalum kwa mawakili na posho ya usaidizi wa pango. Naisukuru sana Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kufanikisha jambo hili,” alisema.

Mhe. Johari alibainisha kuwa chama hicho kimekuwa daraja muhimu kati ya Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Wakala Mkuu wa Serikali na mamlaka nyinginezo, kwa ajili ya kusimamia na kurahisisha upatikanaji wa huduma za kisheria nchini.

Aidha, alieleza kuwa usajili wa wanachama unaofanywa na chama hicho unasaidia kubaini maeneo wanayofanyia kazi ili waweze kushiriki kikamilifu katika utoaji wa huduma za kisheria, sambamba na kudhibiti uwepo wa “mawakili hewa” au vishoka.

Mfumo huo pia unasaidia katika upekuzi wa mikataba, utoaji wa ushauri wa kisheria na kuongeza ufanisi katika utendaji wa majukumu ya kisheria serikalini.

Kwa upande wake,  Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Joram Hongoli Sagini,  akizungunza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi katika mkutano huo Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Doto Biteko alisema kuwa wizara yake inakichukulia chama hicho kwa uzito mkubwa, akisisitiza kuwa serikali ina matarajio makubwa kuona chama hicho kinakuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa.

“Chama hiki kilibatizwa jina na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kuwa ni ‘askari wake wanaotumia kalamu kushinda vita ya kiuchumi’, jambo ambalo linaonyesha imani kubwa aliyonayo kwa chama hiki,” alisema Sagini.

Aidha, alieleza kuwa wizara hiyo inaendelea kusimamia kampeni ya kitaifa ya utoaji wa huduma za kisheria kwa wananchi ijulikanayo kama “Mama Samia Legal Aid”, ambayo imekuwa ikizunguka mikoa mbalimbali nchini. Mpaka sasa, zaidi ya wananchi milioni mbili wamefikiwa na huduma hiyo.

Related Posts