Kagera Sugar ilivyomfungulia njia Adebayor

BAADA ya winga wa Singida Black Stars, Victorien Adebayor kufunga bao moja katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Kagera Sugar, mchezaji huyo amesema imetimiza hamu yake ya kucheka na nyavu.

Hilo ni bao la kwanza kwa Adebayor tangu alipojiunga na Singida Black Stars mwanzoni mwa msimu huu akitokea AS GNN ya nchini kwao Niger.

Adebayor alifunga bao hilo katika mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) uliochezwa Jumatatu wiki hii na kuisaidia Singida Black Stars kufuzu nusu fainali ikisubiri kucheza dhidi ya Simba.

“Nimefurahi kufunga bao katika mojawapo ya mashindano muhimu kwa timu yangu, ingawa malengo yangu wakati nakuja kucheza Tanzania bado hayajatimia kwa sababu natamani kufanya vitu vikubwa zaidi,” alisema Adebayor na kuongeza.

“Natamani zaidi kazi yangu iwe na nguvu mbele ya macho ya mashabiki kuliko mimi kuongea sana, hivyo najipa muda wa kuonyesha ninachokimaanisha.”

Adebayor anasisitiza katika mechi zilizosalia za Ligi Kuu na FA hajaona kama kuna maajabu anaweza kuyafanya.

“Sipendi kudanganya ninaweza nikafanya makubwa kwa mechi zilizobaki, ingawa inaweza ikatokea nikafunga kama nilivyofunga ama kutoa asisti.

“Wakati nakuja kucheza Tanzania, malengo yangu makubwa yalikuwa ni kuandika rekodi zenye heshima za kusimuliwa na wengine niliwahi kuwepo katika ligi fulani, lakini hadi sasa mambo yamekuwa magumu,” alisema nyota huyo raia wa Niger.

Adebayor amekuwa hapati nafasi kubwa ya kucheza kwenye kikosi cha Singida Black Stars kutokana na ushindani wa namba uliopo huku nyota kama Jonathan Sowah, Elvis Rupia, Marouf Tchakei na Emmanuel Keyekeh wakiaminiwa zaidi kwenye eneo la mbele kuanzia kiungo hadi ushambuliaji.

Related Posts