Mbunge alilia barabara ili apite kwenda kuomba kura za Rais Samia

Dodoma. Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Angelina Malembeka ameitaka Serikali kuharakisha ujenzi wa barabara katika maeneo mbalimbali nchini, ili kuwawezesha wananchi kufika kwa urahisi na kumuombea kura Rais Samia Suluhu Hassan.

Malembeka ametoa kauli hiyo leo bungeni, Jumatatu, wakati akichangia hotuba ya Waziri Mkuu kuhusu bajeti ya mwaka 2025/26, ambapo Serikali imeomba kuidhinishiwa na Bunge kiasi cha Sh782.08 bilioni.

Amesema kuwa katika kipindi hiki, wanatarajia kuwafikia wananchi ili kuwaomba kura kwa ajili ya Rais, lakini changamoto ya miundombinu, hususan ukosefu wa barabara katika maeneo mengi, inaweza kuwakwamisha kuwafikia wapiga kura waliokusudiwa, ili hatimaye kiongozi huyo apate ushindi wa kishindo ifikapo wakati wa uchaguzi.

“Mheshimiwa mwenyekiti, tunaomba barabara zijengwe ili tupite salama na tuwafikie wananchi tunaowalenga kwa ajili ya kwenda kuwaomba kura za mama, tunataka kura za mama zijae tatizo ni kuwafikia watu,” amesema Mbunge.

Mbunge huyo amesema kazi kubwa imefanyika chini ya Serikali ya awamu ya sita, lakini tatizo la barabara imekuwa ni changamoto inayotia doa.

Mbunge wa Liwale (CCM), Zuberi Kuchauka amelalamikia kitengo cha Maliasili kwa madai kuwa wameshindwa kuwaondoa tembo katika mashamba ya wananchi katika Mkoa wa Lindi.

Kuchauka amesema ziko taarifa kuwa Tembo wakizalia katika eneo moja, huligeuza kuwa ni sehemu ya nyumbani kwako hivyo wananchi wanapata hofu kwani wanyama hao wanazaliana katika mashamba yao.

Amesema mashamba ya wananchi wa Wilaya ya Liwale wanyama hao wamejazana na wanahalibu mazao, lakini hakuna kifuta jacho kinachotolewa na Serikali akisema jambo hilo linawapa hofu.

Related Posts