.,…………….
RAIS Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya utoaji wa tuzo za wanahabari zinazofahamika kama ‘Samia Kalamu Awards’ zinazohamasisha uandishi wa habari za maendeleo katika nyanja mbalimbali.
Tuzo hizo ambazo zimeandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinatarajiwa kutolewa Aprili 29, mwaka huu katika ukumbi wa Mabeyo Complex jijini Dodoma.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Aprili 15, 2025, Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Dk. Rose Reuben amesema tuzo hizo zimelenga kuhamasisha uandishi wa habari za maendeleo unaojikita katika kufanya uchambuzi na utafiti wa kina, kuongeza maudhui ya ndani, kuzingatia weledi, maadili na uwajibikaji wa kitaaluma.
Amesema tuzo hizo ambazo pia zimelenga kukuza uzalendo na kujenga taswira chanya ya nchi zimetokana na mafunzo yaliyotolewa mwaka jana (2024) ambayo yalilenga kukuza na kuendeleza uandishi wa habari za maendeleo nchini.
“Walengwa wa tuzo hizi ni waandishi wa habari, wachapishaji wa maudhui ya mitandaoni, maafisa habari, watangazaji wa vyombo vya habari ambao walishiriki kwa kutuma kazi zilizorushwa ama kuchapishwa kupitia vyombo yao” amesema Reuben na kuongeza
“Tuzo hizi zimegawanyika katika makundi matatu, kundi la kwanza linahusisha tuzo maalumu za kitaifa ambazo ni pamoja na Tuzo ya Chombo cha habari mahiri kitaifa, Wanahabari Wabobevu, Tuzo ya Ofisa Habari Mahiri wa Serikali, Mwandishi wa habari mahiri kitaifa na Tuzo ya Uandishi wa habari za matumizi ya nishati safi ya kupikia,” amesema
Reuben amesema kundi la pili linajumuisha Tuzo kwa vyombo vya habari ambazo ni Tuzo za Televisheni, vyombo vya habari mtandaoni, redio ya kitaifa, magazeti na redio za kijamii huku kundi la ni tuzo za kisekta ambazo zitatolewa kwa waandishi wa habari waliobobea katika kuandika makala za maendeleo katika sekta mbalimbali.
“Sekta hizo mbalimbali ni pamoja na afya, maji, nishati, mazingira, jinsia, wanawake na makundi maalumu, ujenzi, viwanda na biashara, maliasili na utalii, mifugo na uvuvi, uchumi wa buluu, kilimo, utamaduni, sanaa na michezo, Tehama na ubunifu, ardhi na makazi, madini, fedha na uchumi, vijana, elimu na uwekezaji,” amesema
Aidha amesema tukio hilo litarushwa mubashara kupitia vituo mbalimbali vya televisheni, redio na mitandao ya kijamii ili kuwawezesha wananchi wote waliowapigia kura waandishi na vyombo vya habari kufuatilia matokeo ya utoaji tuzo.
“Washindi watatunukiwa zawadi mbele ya mgeni rasmi kama ishara ya kuthamini na kutambua mchango mkubwa wa vyombo vya habari katika ustawi wa taifa,” amesema Mhandisi Mkuu Mwandamizi Kitengo cha Huduma na Utangazaji TCRA, Jani Kaaya
Naye Mhandisi Mkuu Mwandamizi Kitengo cha Huduma na Utangazaji TCRA, Jani Kaaya amewataka waandishi wa habari nchini kuendelea kuandika habari za maendeleo pamoja na kuwa wazalendo katika taifa huku wakihamasisha matumizi ya teknolojia.
Amesema tuzo hizo za Samia Kalamu Awards zitatoa nafasi kubwa kwa waandishi wa habari kuandaa na kuandika habari zinazozingatia maadili na weledi wa hali ya juu na zenye kuhamasisha watanzania kufahamu mambo makubwa ya kimaendeleo yaliyofanywa nchini.