Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Hamza Johari amemshukuru Rais Samia kwa kuendelea kukilea chama Cha Mawakili wa Serikali kwa miaka mitatu na kusema kuwa ni wajibu wao sasa kukilinda na kuhakikisha kinafikia malengo yake.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameyazungumza hayo leo Aprili 15, 2025 jijini Dodoma wakati wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Mawakili wa Serikali.
Pia, amebainisha kuwa kupitia mkutano huo wameidhinisha Mpango Mkakati wa Chama hicho kitakachoufuata na kutekeleza katika kipindi cha miaka mitano.
“Tumetengeneza Mpango Mkakati tunaokwenda kuutekeleza kwa shauku kubwa pamoja na viongozi wapya watakao chaguliwa katika Uchaguzi unaofanyika leo,” amesema Mhe. Johari.
Amesema hadi kufikia Aprili 9, 2025 idadi ya Mawakili wa Serikali waliojisajiliwa katika Daftari la Mawakili wa Serikali imefikia 3,760 kutoka 2,652 waliosajiliwa wakati wa kuanzishwa kwa Chama hicho.
Naye Mwanasheria Mkuu wa Serikali Zanzibar, Mhe. Dkt. Mwinyi Talib Haji amewaomba Mawakili na Maafisa Sheria wa Serikali kufanya kazi kwa uadilifu na kuzingatia sheria ili kujenga jamii imara na kupunguza mizozo katika jamii.
Aidha, amesema taasisi za sheria ziendelee kushirikiana ili kusaidia wananchi na kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi za kuhudumia jamii na kuleta ustawi kwa mustakabali kwa maendeleo ya nchi.
Kwa upande wake Rais wa Chama cha Mawakili wa Serikali, Amedeus Shayo amesema kuwa Chama chao kimefanikiwa kujenga mfumo wa kielektoniki wa kukusanya ada kwa wanachama pamoja na kuimarisha ushirikiano na taasisi zinazoshughilika na masuala ya sheria za ndani na nje ya nchi.
“ Rais Samia ameendelea kuwa kielelezo kizuri cha haki kupitia Kampeni yake ya Msaada wa Kisheria na Mawakili wanashiriki kutoa huduma za sheria kwa wananchi. Pia, agizo la Rais Samia la Mawakili kuwa walinzi wa uchumi wa nchi kwa kutumia kalamu limeweka msingi wa Chama hiki na umesaidia kuboresha sheria kadhaa mfano Sheria ya Uwekezaji,” amesema Shayo.
Awali Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mstaafu na Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi amemshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia kwa kuzindua Chama hicho mwaka 2022 na kusema “ Chama hiki kama kilivyoanzishwa na malengo yake kitabaki kuwa Chama bora cha kitaaluma kwa sababu Serikali na mawakili walijipanga kuwa nacho na hili ni jeshi la kulinda uchumi wa nchi kwa sheria na kalamu,”
Mkutano huo uliohudhuriwa na Mawakili wa Serikali kutoka katika Wizara, Wakala na Taasisi za Serikali, Mashirika ya umma umeongozwa na Kauli mbiu “ Utawala wa Sheria katika Utekelezaji wa Majukumu ya Serikaki ni Nguzo Muhimu katika Kufikia Malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050”