Simba imesema inawahi Zanzibar siku nne kabla ya mchezo huo wa nusu fainali ya mkondo wa kwanza wa Kombe la Shirikishio Afrika utakaochezwa Aprili 20 mwaka huu kwenye Uwanja wa New Amaan Complex visiwani humo ili kutoa fursa kwa wachezaji kuzoea mazingira na kuwarahisishia kazi ya kupata ushindi.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema kikosi hicho kikiondoka Dar es Salaam saa 3 asubuhi, kitafika Zanzibar saa 5 asubuhi.
Ally amesema baada ya kufika Zanzibar, moja kwa moja maandalizi yataanza kwa ajili ya mchezo huo ambao malengo yao ni kuona wanashinda nyumbani kisha kwenda ugenini kumalizia kazi ya kutinga fainali.
“Kikosi cha Simba kitawasili Zanzibar kesho asubuhi, tumeamua kuja mapema ili kujiandaa na wachezaji waanze kuzoea mazingira ya Zanzibar. Stellenbosch FC bado hawajatupa taarifa kama watakuja moja kwa moja Zanzibar au watapitia Dar es Salaam,” amesema Ally.
Wakati Simba kesho wakienda Zanzibar, leo saa 2 usiku Stellenbosch watakuwa na mchezo wa Ligi Kuu Afrika Kusini dhidi ya AmaZulu FC, kisha baada ya hapo ndiyo wataanza mikakati ya kuja Tanzania kucheza dhidi ya Simba kabla ya kurudiana Aprili 27.

Baada ya kufuzu nusu fainali, Ally amesema malengo yao ni kuona wanatinga fainali na kubeba ubingwa huku wakitaka kupanda zaidi viwango vya klabu vya CAF kufuatia hivi sasa kutoka nafasi ya saba mpaka ya nne.
“Nafasi ya nne Afrika bado sio malengo ya Simba, nusu fainali bado sio malengo, ni sehemu ya mapito. Tunaitaka nafasi ya kwanza Afrika, sio rahisi kumfikia wa kwanza sababu ya alama alizonazo lakini tunaanza na kusogea nafasi ya tatu au ya pili lakini kufikia hilo tunaanza na mchezo wa nusu fainali.
“Tunaenda kucheza mechi hii tukiwa na kauli mbiu inayosema ‘HATUISHII HAPA’, malengo ni kufika fainali ndiyo maana kwa kauli moja tunasema HATUISHII HAPA.”

Mchezo huo ambao umepangwa kuanza kuchezwa saa 10:00 jioni, huku uwanja ukiwa na uwezo wa kuingiza watazamaji 15,885, kutakuwa na viingilio vya aina tatu.
Akitangaza viingilio hivyo, Ally amesema: “Uwanja wa Amaan unaingiza watu 15,885, hivyo tumeweka viingilio kulingana na mahitaji hayo ya mashabiki, tulitamani uwanja ungekuwa na uwezo wa kuingiza mashabiki hata elfu 30 ili ufanane kidogo na ule wa Benjamin Mkapa.
“Hivyo basi, viingilio ni VIP A Sh40,000, VIP B Sh20,000 na Mzunguko Sh10,000. Kuanzia hivi sasa tiketi zinapatikana katika maeneo mbalimbali. Hapa Zanzibar kuna vituo 15 vya kuuzia tiketi hizo, kwa wale wa Dar es Salaam vituo vyote ambavyo vinauza tiketi vitaendelea kuuza kama kawaida.”