Dar es Salaam. Kukosekana kipengele kinachoweka ukomo wa muda wa kusaini kanuni za maadili ya uchaguzi, kumeibua mjadala kwa wanasheria, wakihoji sheria ipi inayoeleza chama cha siasa lazima kisaini siku inayopangwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).
Chimbuko la mjadala huo ni hatua ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kutangazwa na INEC kuwa, kimepoteza haki ya kushiriki uchaguzi mkuu na wamarudia kwa miaka mitano, baada ya kususia kusaini kanuni za maadili ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani Aprili 12, mwaka huu.
Katika taarifa yake hiyo, Mkurugenzi wa INEC, Ramadhani Kailima alisema siku hiyo (Aprili 12), ndio iliyokuwa ya mwanzo na mwisho kwa vyama vya siasa na Serikali kusaini kanuni hizo.
“Utiaji saini haufanyiki kwa siku kadhaa, unafanyika kwa siku moja na ni kesho (Aprili 12, 2025). Kusaini maadili ni takwa la kisheria kwa mujibu wa kifungu cha 162 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani, kwa hiyo kesho ndio kusaini na kesho ndio mwanzo na mwisho wa kusaini kanuni za maadili ya uchaguzi,” alisema Kailima.
Kauli hiyo, ndiyo imeibua mjadala kutoka kwa wanasheria, wanaosema sheria ya uchaguzi haikuweka kipengele kinachoonesha ukomo wa chama au wadau husika kusaini kanuni hizo na kwamba INEC imepata wapi hoja hiyo?
Hata hivyo, kinachohojiwa na wataalamu hao, kinajengwa na msingi wa sheria yenyewe katika Ibara ya 162, inayoipa INEC mamlaka ya kuandaa kanuni hizo, kujadiliana na wadau na kuzichapisha katika Gazeti la Serikali.
Ingawa kifungu hicho, kinawataka wadau wanaostahili kutia saini, lakini hakikueleza ni wakati gani kanuni hizo zinapaswa kusainiwa na lini mwisho wa kulitekeleza hilo.
“Kwa madhumuni ya kusimamia uchaguzi wa haki, huru na amani, baada ya kushauriana na vyama vyote vya siasa na Serikali, Tume itaandaa na kuchapisha katika Gazeti la Serikali Kanuni za Maadili ya Uchaguzi zitakazoainisha maadili ya vyama vya siasa, Serikali na Tume wakati wa kampeni za uchaguzi na uchaguzi na utaratibu wa utekelezaji wake,” inaeleza ibara hiyo.
Ibara ya 162(2) inawataja watakaotia saini ambao ni chama cha siasa, kila mgombea kabla hajawasilisha fomu ya uteuzi, Serikali na INEC na zitapaswa kuzingatiwa na wahusika wote waliosaini.
Ibara hiyo 162(3), inaeleza kuwa, “mtu ambaye atakiuka masharti ya kanuni za maadili ya uchaguzi ataadhibiwa kwa mujibu wa kanuni hizo.”
Hata hivyo, alipotafutwa kuzungumzia hilo, Mkurugenzi wa INEC, Ramadhani Kailima simu yake iliita bila majibu.
Hata simu ya Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria wa tume hiyo, Selemani Mtibora nayo haikupokewa na alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi, hakujibu.
Akizungumzia hilo, Wakili Hekima Mwasipu amesema kwa kuwa hakuna kipengele kinachoweka ukomo wa muda, kisheria chama na mdau yeyote husika anaweza kusaini siku yoyote kabla ya kanuni hizo kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali.
“Kama hakuna kipengele kilichoweka ukomo maana yake mdau husika anaweza kusaini siku yoyote. Kwa sababu zinatakiwa zisainiwe ili kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali, maana yake kabla hazijachapishwa zinaweza kusainiwa wakati wowote,” amesema.
Mtazamo huo unashabihiana na uliotolewa na wakili mwingine wa kujitegemea, Dickson Matata aliyesema kuna changamoto ya tafsiri ya kisheria katika ukomo wa muda wa kusaini kanuni hizo za maadili.
Ameeleza changamoto hiyo imetokana na maelezo ya INEC kuwa, Aprili 12, mwaka huu ndio iliyokuwa siku pekee ya kutia saini kanuni hizo.
“Unasema siku moja wakati sheria haijazungumza ni wakati gani mtu haruhusiwi kusaini na tunafanya mambo kwa kufuata sheria inavyosema sio utashi wa mtu,” ameeleza.
Ameeleza lengo la kanuni hizo ni kutaka vyama au mgombea kuzingatia kanuni za maadili wakati wa uchaguzi, kwa kuwa uchaguzi haujafika na hata wagombea hawajateuliwa, vyama vingeendelea kupewa muda wa kusaini.
“Unawezaje kukata kauli kwamba hakuna namna watu wanaweza kusaini ilhali bado hata uchaguzi wenyewe haujafika,” amesema Matata.
Hata hivyo, amesema hadi sasa bado kilichosainiwa hakijawa kanuni, kwa kuwa hazijatangazwa kwenye Gazeti la Serikali kama inavyohitajika.
Kinyume na hoja hizo, Wakili Sweetbert Nkuba amesema hakuna kipengele kinachoweka ukomo wa muda wa kusaini kanuni za maadili.
Amesema sheria imeipa INEC mamlaka ya kuandaa rasimu ya kanuni kisha kuwashirikisha wadau, kukusanya mapendekezo yao, kujadili kisha wayasaini na iyaweke kwenye Gazeti la Serikali.
“Watu wanatafuta kichaka cha kujificha kwenye sheria kwamba sio lazima usaini siku moja, ilhali wanajua ni lazima zisainiwe ili zitangazwe kwenye Gazeti la Serikali, ukisema hutasaini kwa siku moja zitachapishwa lini gazetini,” amesema.
Kwa mtazamo wake, kama kutakuwa na nafasi ya kusaini kabla hazijatangazwa ni sawa, lakini haiwezekani kujipa muda wa kusaini wakati wowote, ilhali zinatakiwa kuchapishwa.
“Lazima zisainiwe kabla hazijatangazwa kwenye Gazeti la Serikali, huwezi kusema utasaini kesho au siku yoyote, ili zitangazwe lini. INEC ndiye aliyepewa mamlaka ya kusimamia na yeye ndiye atapanga lini watu wakasaini,” ameeleza.
Wakati Nkumba akisema hivyo, mwanasheria John Mallya amesema anavyojua yeye kanuni hizo si lazima zisainiwe mara moja labda kama kuna mabadiliko.
“Ninavyokumbuka fomu hizo zinatakiwa chama kisaini kabla ya uteuzi wa wagombea haujatangazwa. Mwaka 2015 Chadema ilichelewa kusaini, baadaye ikazisaini.
“Huenda utaratibu wa kuzisaini umewekwa mwaka huu, ninachojua daftari lilikuwa linawekwa wazi na muda wowote unasaini,” amesema.
Maoni ya Mallya yanashabihiana na ya mwanasheria Jebra Kambole aliyesema sheria haikuweka ukomo wa muda wa kusaini kanuni za maadili ya uchaguzi, hivyo wakati wowote chama au mgombea anaweza kusaini.
“Hakuna ukomo wa kusaini kanuni za maadili. Chama au mgombea atasaini muda wowote,” amesema na kufafanua kuwa, uchaguzi unasimamiwa na Katiba na siyo kanuni, hivyo hakuna uwezekano wa chama au mgombea kukosa haki ya kushiriki mchakato huo kwa sababu za kikanuni.
Uboreshaji daftari awamu ya pili
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa INEC, Jaji Jacobs Mwambegele ametangaza ngwe ya pili ya uboreshaji daftari la wapigakura, huku akiwaonya mawakala na vyama vya siasa wasiingilie mchakato huo.
“Niwaombe viongozi wa vyama vya siasa na wadau wa uchaguzi kwa jumla kuzingatia sheria za uchaguzi, kanuni za uboreshaji, maelekezo ya Tume na kusimamia miiko na mipaka ya uendeshaji wa shughuli ya uboreshaji wa daftari la kudumu la mpiga kura,” amesema.
Jaji Mwambegele amesema anayehitaji kuweka pingamizi anatakiwa kwenda kwenye kituo cha kuandikisha wapigakura vilivyopo kwenye kila Kata katika halmashauri husika.
Aidha, amesema uboreshaji katika awamu ya pili utafanyika kuanzia Mei mosi na kutamatika Julai 4, 2025.