Mbeya. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (Tawa) linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kukutwa na vipande 12 vya meno ya tembo katika Wilaya ya Kyela na Mbarali mkoani Mbeya.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga leo Jumanne Aprili 15, 2025 akizungumza na waandishi wa habari amesema kuwa watuhumiwa hao walikamatwa kwa nyakati tofauti kati ya Aprili 3 na 14, 2025.
Kamanda Kuzaga amesema katika tukio la kwanza, Riziki Mapila (55), mkazi wa Lubele Wilaya ya Kyela, alikamatwa na vipande tisa vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilogramu 34.6.
Amesema askari waliokuwa kwenye doria maalumu ya kukabiliana na wahujumu uchumi walimkamata mtuhumiwa katika kitongoji cha Isaki Kata ya Njisi, Tarafa ya Unyakyusa akiwa na vipande tisa vya meno ya tembo. “Askari walipokuwa kwenye doria walimtilia shaka, baada ya kumfuatilia walibaini ndani ya mfuko wa sandarusi alihifadhi meno ya tembo ambayo ni nyara za Serikali ambazo alienda kuficha porini,” amesema Kamanda Kuzaga.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga akionyesha vipande vya meno ya tembo vilivyokamatwa katika Wilaya ya Kyela na Mbarali. Picha na Hawa Mathias
Katika tukio la pili, Kuzaga amemtaja Kennedy Yagawa (37), mkazi wa Itamba akiwa na vipande vitatu vya meno ya tembo bila kibali wakati akitambua fika ni nyara za Serikali.
Amesema Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na askari wa Tawa walimkamata mtuhumiwa katika Kijiji cha Madabaga, kata ya Mapogoro Wilaya ya Mbarali, katika operesheni maalumu zinazoendelea mkoani hapa.
Amesema meno hayo yalikuwa yamehifadhiwa kwenye mfuko wa sandarusi na kisha kufukia ardhini kwenye shamba lililopo kwenye makazi yake.
Kamanda Kuzaga amesema uchunguzi wa awali umebaini watuhumiwa wote wanajihusisha na uhujumu uchumi wa uwindaji haramu wa wanyamapori katika hifadhi za Taifa.
“Watuhumiwa bado wanaendelea kuhojiwa, wakati wowote kuanzia sasa watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili,” amesema Kuzaga.
Akizungumzia tukio hilo, mkazi wa Uyole jijini hapa, Ayubu Samweli ameomba Serikali kuimarisha ulinzi katika maeneo ya hifadhi ili kudhibiti uwindaji haramu na kupoteza rasilimali za Taifa.