WAZIRI MKUU AMPONGEZA RAIS DKT. SAMIA MAFANIKIO MIAKA MINNE

……………………

 ▪️Asema ameimarisha ukusanyaji wa mapato, utekelezaji wa miradi nchini

▪️Asema Miaka minne ya uongozi wake ilani imetekelezwa kwa kiwango kikubwa

▪️Asisitiza ilikuwa ni miaka minne ya kazi na uwajibikaji

 

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amempongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mafanikio yaliyopatikana katika miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita ambapo imeshuhudiwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.

 

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa utekelezaji wa miradi hiyo umetokana na umarishaji wa ukusanyaji wa mapato nchini. “Bila shaka, kila mwananchi ni shahidi wa jambo hili. Hakika Mheshimiwa Rais anastahili pongezi na tunampongeza sana”.

 

“Ninapenda kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza miaka minne ya kuiongoza nchi yetu kwa mafanikio makubwa. Sote ni mashahidi kuwa, katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake, Ilani ya Uchaguzi imetekelezwa kwa kiwango kikubwa.”

 

Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo (Jumanne, Aprili 15, 2025) wakati akiwasilisha hotuba yake ya kuhitimisha hoja ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2025/2026 aliyoiwasilisha Bungeni Jumatano, Aprili 9, 2025.

 

Amesema sambamba na kudumisha hali ya amani, utulivu pamoja na mshikamano wa wananchi, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewezesha utekelezaji wa mipango ya maendeleo pamoja na kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato.

 

 “Mathalan, katika kipindi cha mwezi Julai hadi Machi, mwaka wa fedha 2024/2025, Mamlaka ya Mapato Tanzania imekusanya kiasi cha shilingi trilioni 24.05 sawa na ufanisi wa asilimia 103.62 ya lengo.”

 

Aidha, makusanyo hayo ni ya kiwango cha juu kabisa kufikiwa na TRA kwa kipindi kama hicho tangu kuanzishwa kwake. “Kiasi hicho ni sawa na ongezeko la asilimia 77 ikilinganishwa na kiasi cha shilingi trilioni 13.59 zilizokusanywa katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha 2020/2021.”

 

Mheshimiwa Majaliwa amesema ufanisi uliofikiwa katika makusanyo ni matokeo chanya ya kutekeleza kwa vitendo maagizo na maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha mazingira ya ulipaji kodi.

 

“…Serikali inawapongeza walipakodi nchini kutimiza wajibu wao kwa kulipa kodi stahiki kwa wakati na kuendelea kuunga mkono kizalendo juhudi za Serikali za kuleta maendeleo nchini kwani “Kodi Yetu Ndiyo Maendeleo Yetu”.

 

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwapongeza wafanyakazi wote nchini kwa mchango wao mkubwa katika maendeleo ya Taifa. Vilevile, awapongeza waajiri, viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi na wadau wote kwa kuendelea kuheshimu haki na utu wa wafanyakazi.

Related Posts