Mjadala wa siasa kwa sasa ni Chadema kutosaini kanuni za maadili ya uchaguzi, kupoteza sifa ya kushiriki Uchaguzi Mkuu 2025, vilevile migongano ya kisheria kuhusu haki ya chama hicho kushiriki uchaguzi.
Wanasheria wanalumbana kuhusu tafsiri ya kifungu namba 162 (2 na 3). Wengine wanatafsiri na kutoa hitimisho kuwa Chadema ndiyo imetoka. Hawana chao Uchaguzi Mkuu 2025. Wapo wanaojenga hoja kwamba sheria hiyo ni kinyume na Katiba ya Tanzania, kwamba Chadema bado wanayo fursa ya kushiriki.
Swali linakuja; Chadema wao wanasemaje? Mzizi wa yote ni vuguvugu la No Reforms, No Election. Hata kitendo cha Chadema kutokwenda kusaini kanuni za maadili ya uchaguzi, ni utekelezaji wa vuguvugu hilo.
Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, yupo mahabusu, akikabiliwa na kesi ya uhaini. Msingi wa mashitaka dhidi yake ni matamshi yake, kuhusu namna chama chake kitakavyozuia uchaguzi. Msimamo wa Chadema ni kuuzuia Uchaguzi Mkuu 2025 kufanyika.
Sasa, kama Chadema wenyewe hawaitaki haki ya kushiriki Uchaguzi Mkuu 2025, malumbano ya kisheria yanatokea wapi?
Haki ina mantiki ikiwa ambaye anaistahili atakuwa anaitaka. Kama haitaki, kumtetea aipate ni sawa na kumlazimisha nzi azalishe asali.
Dhahiri, Chadema waligoma kuhudhuria shughuli ya kusaini kanuni za maadili ya uchaguzi ili kutuma ujumbe kwamba hawatanii wanaposema “No Reforms, No Election.” Na bila shaka, waliona wangesaini wangeonekana hawayaishi maneno yao.
Ninachoshawishika kujadili ni vuguvugu la No Reforms, No Election, uwezo wa Chadema kulifanikisha na mifano ya kihistoria.
Lini na wapi, wanasiasa wa upinzani na vyama vyao, wamewahi kufanikisha kuzuia uchaguzi kufanyika? Msisitizo wa Lissu ni kuwa malengo hayakuwa kususa uchaguzi, bali kuuzuia.
Kama mpango ulikuwa huo, nini kilitokea mpaka kususia utiaji saini kanuni za maadili ya uchaguzi? Yupo mtu anaweza kutafsiri kwamba Chadema bado hawajajua namna ya kutekeleza vuguvugu walilolianzisha.
Kutosaini kanuni za maadili, kunaweza kusababisha Chadema kupita njia ngumu kufanikisha ajenda yao.
Kufanya mikutano ni haki yao kikatiba, lakini wanaweza kuzuiwa. Vipi polisi wakiwauliza: “Ninyi hamshiriki uchaguzi, mikutano ya nini?” Siasa ni sayansi. Kutosaini kanuni za maadili halikuwa tendo la kisayansi.
Machi 11, 2025, kupitia gazeti la Mwananchi, niliandika makala iliyokuwa na kichwa “No Reforms No Election ni sayansi au utani wa kisiasa?”
Nilichambua ugumu wa Chadema kuitekeleza agenda hiyo kulingana na muda na uwezo wa ushawishi ambao chama hicho kipo nao.
Halafu, napitia kauli ya Mwenyekiti aliyepita wa Chadema, Freeman Mbowe aliyesema ni makosa makubwa kwa chama hicho kususia uchaguzi. Mbowe alisema, CCM wangetamani kuona Chadema inasusia uchaguzi.
Kisha, mawazoni inanijia kauli ya Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi aliyewataka watu wasiilazimishe Chadema kushiriki Uchaguzi Mkuu 2005, kwa sababu chama hicho kinaweza kuwania uchaguzi utakaofuata mwaka 2030 na kuendelea.
Nchimbi aliomba Chadema wawapigie kura wagombea wa CCM ili wasipoteze haki zote, kutopigiwa na kutopiga kura.
Kauli ya Nchimbi inakuonesha kwamba chama chake hakioni hasara yoyote kisiasa kwa Chadema kususa. Alitaka wasibembelezwe.
Baada ya hapo turejee mgogoro wa Tanu mwaka 1958, uliosababishwa na masharti ya kura tatu, yaliyowekwa na Wakoloni, Uingereza. Tanu iligawanyika, waliokuwa na msimamo mkali, walikataa kushiriki uchaguzi. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alisema kutoshiriki ni hasara kubwa kuliko kushiriki. Tanu ilishiriki, ikawa mwanzo wa safari njema ya uhuru.
Mshangao wangu ni chama cha siasa kutoshiriki uchaguzi, wakati mfano ni CUF chini ya Seif Sharif Hamad.
Matokeo ya Uchaguzi Mkuu 2015, yaliyompa ushindi Seif, yalifutwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC). Kuonesha kupinga kilichofanyika, Seif aliiongoza CUF kususia uchaguzi wa marudio ulioitishwa. Uchaguzi wa marudio ulifanyika Machi 20, 2016. Mgombea urais wa CCM, Dk Ali Mohammed Shein, alishinda kwa asilimia 94.1.
Ukiachilia idadi ya wapigakura kujitokeza kidogo, mambo mengine yote yalikuwa chereko kwa CCM. Kilichotokea kwa Seif na Cuf, kilitoa picha kwamba kitendo cha kususa kushiriki uchaguzi, hakikuwa na faida kwake binafsi wala chama. Ni sawa tu na kumsusia fisi bucha au nguruwe shamba la mihogo.
Uamuzi wa kususia uchaguzi una faida tu ya kutaka kuhurumiwa na mataifa ya kigeni na jumuiya za kimataifa, lakini hayajengi chama wala mwanasiasa dhidi ya ushindani wa kisiasa.
Zanzibar mwaka 2016, kwa uamuzi wa Seif, maana yake wafuasi wake wengi hawakupiga kura, hivyo Shein alipata urahisi wa kushinda.
Ilitokea kama ya Angola mwaka 1992. Uchaguzi wa awali Eduardo dos Santos wa MPLA alipata asilimia 49 na Jonas Savimbi wa Unita alipata asilimia 40. Hakuna aliyezidi asilimia 50.
Uchaguzi wa marudio ulipoitishwa Savimbi alisusa kwa madai ya kuibiwa kura. Haikumsaidia, Santos aliendelea kuongoza, Savimbi alirudi msituni. Mwisho aliuawa. Uchaguzi Mkuu 2020, Seif akiwa na ACT-Wazalendo, walishiriki uchaguzi. Hawakupata matokeo makubwa, lakini waliamua kujiunga na Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU).
Seif alisema, wao walishasusa sana bila kupata chochote, kwa hiyo bora kuwemo ndani ili kuchochea mabadiliko.
Kumsusia uchaguzi kiongozi aliye madarakani kwa nchi za Kiafrika ni sawa na kumpa urahisi wa kushinda. Raila Odinga, alisusia uchaguzi wa marudio Kenya, mwaka 2017, kwa hoja ya kutokuwa na imani na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).
Kwa kitendo cha Raila kususia, Uhuru Kenyatta ambaye ndiye alikuwa rais, alitangazwa mshindi kwa kura asilimia 98. Kisha, Raila hakupata chochote, zaidi ya kujiapisha kupitia kiapo cha wakili mtata, Miguna Miguna. Baadaye, Raila alishikana mkono na Uhuru, yakaisha. Uhuru aliongoza kwa amani mpaka alipostaafu kikatiba.
Chadema kutoshiriki uchaguzi, wanampa nafasi Rais Samia Suluhu Hassan na chama chake, CCM, kujipanga kudumisha amani kipindi chote cha kampeni hadi matokeo yatakapotangazwa. Hawana presha ya uchaguzi, maana ushindani utakuwa mdogo dhidi ya vyama vingine.