Edison Arantes do Nascimento au Pele (1940-2022) alikuwa mchezaji bora aliyeisaidia Brazil kutwaa kombe la Dunia mara tatu na alikuwa na uwezo wa kuupiga mpira kwa mguu wowote ili kuwazidi ujanja wapinzani wake uwanjani.
Mwaka 1999 alichaguliwa na shirikisho la mpira wa miguu duniani (Fifa) kuwa mchezaji bora wa karne na kwa mujibu wa Fifa alikuwa mfungaji bora wa muda wote kwa kufunga magoli 1281 kati ya mechi 1363 na alikuwa mchezaji ghali.
Nafananisha uchezaji wake na kile ambacho Chama cha Mapinduzi (CCM) kimefanya usiku wa kuamkia leo Aprili 16, 2025 kusogeza mbele uchukuaji wa fomu za kuomba kuteuliwa kugombea nafasi za ubunge, uwakilishi na udiwani uchaguzi mkuu 2025.
Ninasema hivyo kwa sababu uchukuaji fomu wa mapema uliokuwa umetangazwa na chama hicho tawala, ulianza kuathiri ushiriki wa wabunge katika mijadala muhimu ya Bunge, kwa sababu walikuwa mguu moja ndani mguu mmoja nje.
Hakuna asiyefahamu kura za maoni ndani ya CCM safari hii ni kimbembe (ni shughuli pevu) kwa sababu kuu mbili, moja kuna hisia kuwa baadhi ya wabunge na madiwani walibebwa katika kura za maoni na mfumo wa Rais John Magufuli.
Lakini jambo la pili, ni wingi wa watia nia wa nafasi za ubunge na udiwani Tanzania Bara ambao tayari wamekuwa wakifanya purukushani majimboni na kuwanyima usingizi wabunge waliopo madarakani sasa, wanaomaliza kipindi chao Julai 2025.
Awali uchukuaji huo wa fomu ulikuwa umepangwa kufanyika kwa siku 15 kuanzia Mei 1 hadi Mei 15,2025, lakini utaratibu huo ulianza kuleta athari za ushiriki wa wabunge katika vikao vya bajeti hasa ikizingatiwa Bunge linaloendelea ni la bajeti.
Ninaambiwa lengo la kutoa fomu mapema ilikuwa ni kuviwezesha vikao vya ufuatiliaji (vetting) kupata nafasi ya kutosha kupitia mienendo ya watia nia wote na kuwabaini wale waliokiuka Kanuni za Uteuzi wa wagombea toleo la 2021.
Lakini katika taarifa yake iliyotolewa kwa umma usiku wa kuamkia leo Aprili 16,2025, Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Emmanuel Nchimbi, mchakato wa uchukuaji fomu sasa utaanza Juni 28,2025 saa 2:00 asubuhi na kukamilika Julai 2.
Hii ni baada ya mashauriano na wanachama wake, kutafakari na kupima kwa umakini ushauri wao, kikaamua kufanya mabadiliko hayo ya ratiba ya uchukuaji fomu na sasa utafanyika baada Rais Samia Suluhu kufunga Bunge Juni 27, 2025.
Nasema CCM imecheza kama Pele kwa sababu huko majimboni na kwenye kata ni kama ilikuwa “fungulia mbwa” (ruksa) kwani purukushani zilizokuwa zinaendelea zilikuwa zinasababisha mgawanyiko mkubwa kwa viongozi na wanachama.
Kifungu cha 25(2) cha Kanuni za uteuzi wa wagombea uongozi katika vyombo vya Dola Toleo la 2021 kinasema ni mwiko kabisa kwa mgombea kutumia au kuhusisha ukabila, dini, rangi au eneo analoishi au kutoka katika shughuli yoyote ya uchaguzi.
Lakini hali ni tofauti sana katika baadhi ya majimbo ambapo baadhi ya wagombea wanajinadi katika baadhi ya nyumba za ibada kuwa safari hii ni zamu ya kupata Diwani au Mbunge ambaye ni mwislamu au mkristo kinyume na Kanuni hiyo.
Kifungu kidogo cha (3) cha Kanuni hizo kinakataza mgombea yeyote na hapa nadhani hata hawa watia nia, kufanya kampeni za kupakana matope, au ya aina yoyote ile dhidi ya mgombea mwingine na hapa nakusudia walionyesha nia.
Wakati kifungu hicho kinazuia kupakana matope, kwenye baadhi ya majimbo wako mawakala, wapambe au “chawa” wa watia nia wamefungua hadi makundi ya Whatsapp mahsusi kwa ajili ya kuwapaka matope wabunge waliopo sasa.
Kifungu kidogo cha (5) cha Kanuni hizo kinasema ni marufuku kwa mwanachama yeyote anayetarajia kugombea au wakala wake kufanya vitendo vinavyoonekana dhahiri ni sehemu ya kampeni kabla ya muda, lakini huko majimboni ni vurugu.
Kanuni hizo zimeandikwa vizuri sana kwani kifungu kidogo cha (6) cha Kanuni hiyo ya 25 kinasema ni marufuku kwa mwanachama yeyote anayetarajia kugombea au wakala wake, kutoa misaada mbalimbali wakati uchaguzi unapokaribia.
Hata hivyo, kanuni hiyo haitamhusu Mbunge, Mwakilishi au Diwani ambaye yupo madarakani wakati huo, kwa kuwa yeye atakuwa bado anao wajibu wa kuhudumia eneo lake la uchaguzi, lakini hali inayoendelea huko majimboni inasikitisha.
Pamoja na Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan kukemea jambo hili katika mkutano mkuu maalum wa CCM uliofanyika Jijini Dodoma Januari 2025, bado wako ambao ni sikio la kufa, wanaendelea kama vile hakuna karipio.
Rais katika karipio lake, alisema wamepokea malalamiko na ushahidi wa picha nyingi sana (pigia msitari neno picha nyingi sana), za watu wanaofanya misafara kwenda majimboni, au vikao vya kujitambulisha na akaonya juu ya hilo.
Wako ambao wanatarajia kugombea wamekuwa wakitoa misaada mbalimbali wengine wamefanya kazi hii tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu 2020, wakiamini wao ndio walistahili kuwa wabunge ila walipokwa nafasi na vikao vya chama.
Kwa hiyo utaratibu wa awali wa CCM wa kutoa fomu mapema hata kabla ya Bunge kuvunjwa, ni kama ulionekana kuruhusu vurugu zaidi majimboni na kwenye kata hali ambayo ilianza kuathiri ufanisi wa utendaji wa wabunge na madiwani.
Mbaya zaidi, wapo watia nia ambao wanapita majimboni na kuwahadaa baadhi ya Makatibu Kata au wapiga kura, kuwa wao wametumwa na Rais Samia au Waziri mkuu au kigogo mkubwa wa Serikali, kuwania nafasi hiyo na atamkingia kifua.
Kampeni hizo za mapema, si kwamba zimewagawa viongozi wa CCM na wanachama katika majimbo yenye rafu hizo, lakini zimeanza kuwagawa hata wapiga kura watarajiwa katika uchaguzi mkuu kutokana kauli zao.
Hali hii ilianza kuwafanya wabunge waliopo katika vikao vya bajeti kujikuta wako njia panda, ama washiriki vikao vya Bunge au watoke kwenda kuzima moto unaowaka majimboni na hii imesababisha hata Bunge kuonekana limepoa.
Ndio maana nasema CCM kwa kusogeza mbele uchukuaji wa fomu hadi Bunge linapokuwa limevunjwa ni kama wamecheza pele na kurudisha akili za wabunge wetu bungeni, badala ya akili muda wote kuwa majimboni kujua nini kinaendelea.
Kamati zile za usalama za CCM zinatakiwa kufanya kazi kweli kweli ili kuhakikisha kuwa majina matatu yatakayorudishwa ni ya wale tu walioheshimu Kanuni, wanaokubalika na wenye sifa za kupeperusha bendera ya Chama cha Mapinduzi.
Kwanini nasema hivyo, kwa sababu hilo lisipofanyika, tutaingiza watu wasio na maadili na watoa rushwa katika vyombo vya Dola, jambo ambalo ni hatari kwani watakwenda kuendeleza vitendo vyao vya ukosefu wa maadili ikiwamo rushwa.
Ndio maana nasema uamuzi huu wa CCM ni kama mchezaji Pele, bila hivyo kungekuwa na athari kubwa kwa wabunge wanaotokana na CCM kufuatilia vikao vya bunge la bajeti na badala yake wangekimbizana majimboni kuzima moto.