KUNA sababu tano za msingi zilizowafanya mabosi wa Yanga kukaa mezani na nahodha wa timu hiyo, Bakari Mwamnyeto kujadili dili jipya na mwisho wa siku kumpa mkataba wa miaka miwili kuendelea kukipiga Jangwani.
Mwamnyeto aliyetua Yanga Agosti 2020 akitokea Coastal Union, mkataba wake na Yanga ulikuwa unamalizika Juni 30, mwaka huu, hivyo alibakisha takribani siku nne awe huru kabla ya kusaini dili jipya.
Mwananchi linafahamu kwamba, Yanga katika kufanikisha kumpa beki huyo mzawa mkataba mpya wa miaka miwili zimewatoka Sh300 milioni zikiwa ni pesa ya usajili huo.
Hapa kuna sababu tano zilizowafanya Yanga kuendelea kuwa na beki huyo.
Kuhofia kuwaachia Simba mali
Yanga walikaa chini na kufikiria mara mbili kwamba Mwamnyeto akiondoka kisha akatua kwa wapinzani wao hali itakuwaje, jibu walilopata moja kwa moja likawafanya wampe mkataba fasta.
Hilo lilikuja baada ya kuwepo kwa taarifa kwamba endapo Mwamnyeto atashindwana na Yanga katika ishu ya mkataba mpya, basi Simba walikuwa tayari kumchukua. Yanga wakaona siyo kweli, acha tubaki na mali yetu kwani wakiiachia inaweza kuwa pigo kubwa kwao pindi akitua kwa wapinzani.
Kabla ya kusaini mkataba huo, taarifa za ndani zinasema nyota huyo alikuwa na ofa kadha ikiwemo ya nje ya nchi, lakini menejimenti inayomsimamia iliamua kumuachia mwenyewe kufanya uamuzi wapi pa kwenda kwani ndiye mwamuzi wa mwisho.
“Ofa zote zilikuja mezani, lakini maamuzi ya mwisho tumemwachia mchezaji mwenyewe achague wapi atakwenda kuchezea msimu ujao,” alisema mtu wake wa karibu.
Kumkosa mridhi wake
Yanga wameangalia akiondoka Mwamnyeto katika eneo la ulinzi wa kati nani atakuja kuchukua nafasi yake kwa mabeki wazawa waliopo hivi sasa.
Ukiangalia katika timu kubwa za Simba, Yanga na Azam kwa msimu uliopita, Yanga pekee ndiyo ina mabeki wengi wa kati wazawa wanaocheza kikosi cha kwanza, timu zingine zinawatumia wageni au mchanganyiko. Yanga wanaweza kumpanga Job na Bacca ambao wote wazawa huku benchi akikaa Gift Fred kutoka Uganda na Mwamnyeto mwenyewe.
Pale Simba, Henock Inonga na Che Malone Fondoh ndiyo walijenga utawala wao, hawa wote ni raia wa kigeni, wazawa Kennedy Juma na Hussein Kazi walibaki nje kuwaangalia wenzao.
Azam tangu amekuja Mcolombia, Yeison Fuentes, amekuwa na uhakika wa namba kikosi cha kwanza akicheza sambamba na Mkongomani, Yannick Bangala.
Ukienda kuangalia mabeki wa kati wazawa waliopo katika timu zingine wanakutana na Lameck Lawi kutoka Coastal Union ambaye alifanya vizuri msimu uliopita. Huyu amewahiwa na Simba, hivyo Yanga wakakosa chaguo la haraka wakaona wabaki na mali yao.
Uzoefu
Kwa kipindi chote cha misimu minne alichochezea Yanga, Mwamnyeto amekuwa miongoni mwa wazawa waliokuwa wakipata namba chini ya makocha waliomnoa Zlatko Krmpotic, Cedric Kaze, Juma Mwambusi kabla ya kupokewa na Nasreddine Nabi na Miguel Gamondi. Pia hata katika timu ya taifa, Taifa Stars nyota huyo amekuwa akiitumikia mara kwa mara akifanikiwa kwenda Ivory Coast kushiriki michuano ya Afcon 2022.
Hiyo yote inamfanya kuwa miongoni mwa mabeki wazawa wenye uzoefu mkubwa ndani ya uwanja ukizingatia kwamba ni kiongozi wa timu.
Kwa wastani, kimo cha beki wa kati angalau inatakiwa kuwa urefu wa mita 1.80 mpaka 1.88 na kuendelea ili kukabiliana vizuri na washambuliaji ambao nao wastani wao huwa mita 1.86.
Kwa upande wa Mwamnyeto yeye ana urefu wa mita 1.85 hivyo unamfanya kuwa ni beki aliyefuzu viwango kwa upande huo wa kimo.
Licha ya kwamba urefu ni kigezo kikubwa cha beki wa kati, lakini pia bila ya juhudi binafsi katika kuonyesha uwezo ni kazi bure.
Ndani ya Yanga, Bacca mwenye urefu wa mita 1.77 na Job (1.68) ndiyo wamepata muda mwingi wa kucheza msimu uliopita, huku Mwamnyeto akiishia nje, hiyo ilitokana na kushuka kiwango kidogo.
Licha ya kwamba Mwamnyeto ni beki wa kati, lakini ana uwezo wa kubadilika kulingana na hali ya mchezo inavyokwenda.
Msimu wa 2022-23 wakati Yanga inafanikiwa kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, alikuwa sehemu ya waliotengeneza mabao ya timu yake.
Katika mchezo wa robo fainali dhidi ya Rivers United uliochezwa nchini Nigeria ukiwa ni wa marudiano, Yanga ilishinda 2-0 na kufuzu nusu fainali baada ya nyumbani kutoka 0-0.
Mabao hayo yote yalifungwa na Fiston Mayele dakika ya 74 na 81 huku Mwamnyeto akifanikiwa kutoa asisti zote mbili. Kwa kifupi, Yanga ilikwenda nusu fainali Mwamnyeto akiwa sehemu ya wachezaji muhimu wa kupatikana kwa mabao hayo. Msimu huo pia alifunga mabao mawili ligi kuu.
Mbali na hilo, beki huyo pia mara kwa mara anapopata nafasi ya kucheza, amekuwa akienda mbele kuongeza mashambulizi wakati wa upigwaji wa kona au hata faulo kwa wapinzani, kitu hicho kimemfanya awe na mabao matano katika ligi kuu tangu atue Yanga.
Mwamnyeto aliyekitumikia kikosi hicho kwa misimu minne huku mitatu mfululizo ikiwa na mafanikio makubwa kwake na timu akiwa nahodha, sasa anaendelea kuwa sehemu ya timu hiyo ambayo msimu ujao itakuwa na jukumu la kutetea makombe mawili ya Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho (FA).
Beki huyo amekuwa akitengeneza ukuta wa Yanga akishirikiana na mabeki wengine wa kati Ibrahim Hamad ‘Bacca’, Dickson Job na Gift Fred, japokuwa msimu uliopita mara nyingi alikuwa akianzia benchi.
Mwamnyeto tangu atue Yanga Agosti 2020, kikosi hicho kimebeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara tatu mfululizo kama ilivyo kwa Kombe la Shirikisho (FA), mbali na Ngao ya Jamii mara mbili na kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2022-2023, huku msimu uliopita wakitinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza baada ya kupita takribani miaka 25.
Kuhusu ishu za kumuongezea mkataba beki huyo na usajili kwa ujumla ndani ya kikosi cha Yanga, Meneja wa Habari na Mawasiliano klabuni hapo, Ally Kamwe alisema hayo yote yatafahamika Julai Mosi mwaka huu.
“Julai Mosi ndiyo tutatangaza wachezaji walioongezewa mikataba, walioachwa na wapya waliosajiliwa, pia itafahamika kambi yetu itakuwa wapi, hivyo watu wawe na subira.”