MAAFANDE wa Tanzania Prisons na Coastal Union wameingia vitani kuiwania saini ya mshambuliaji nyota wa Dodoma Jiji, Anuary Jabir.
Straika huyo wa zamani wa Kagera Sugar aliyewahi kuichezea KAA Gent ya Ubelgiji kwa majaribio, ameziingiza vitani timu hizo, huku ikielezwa mabosi wa Dodoma Jiji wako tayari kumuongezea mkataba mpya.
MASHUJAA imeanza mazungumzo ya kumpa mkataba mpya beki wa kushoto wa timu hiyo, Mpoki Mwakinyuke ili kuendelea naye msimu ujao.
Nyota huyo wa zamani wa Mbeya City, Ruvu Shooting na Ihefu, amekuwa panga pangua wa Mashujaa, hivyo kuwashawishi mabosi wa maafande hao kuzungumza naye ili kumuongezea mkataba.
TIMU mbalimbali zimeonyesha nia ya kuhitaji saini ya aliyekuwa kiungo mkabaji wa Mtibwa Sugar, Juma Nyangi Ganambali kwa msimu ujao.
Miongoni mwa timu zinazohitaji saini ya kiungo huyo ni KMC, Kagera Sugar, Dodoma Jiji na Coastal Union baada ya Mtibwa kushuka daraja kwani hataki kucheza Ligi ya Championship kwa msimu ujao.
KENGOLD, Mashujaa na Pamba Jiji zimeonyesha nia ya kuipata saini ya winga wa Mtibwa Sugar, Kassim Haruna ‘Tiote’ msimu ujao.
Nyota huyo wa zamani wa Polisi Tanzania na Namungo, ni mchezaji huru baada ya mkataba wake na Mtibwa kumalizika huku ikielezwa ameanza kunyatiwa na klabu hizo, huku akiwa hajafanya uamuzi wowote.
VIONGOZI wa Dodoma Jiji wameanza kumfuatilia kipa wa Kagera Sugar raia wa DR Congo, Alain Ngeleka anayetaka kuachana na timu hiyo.
Nyota huyo wa zamani wa Kitayosce kwa sasa Tabora United, inaelezwa hana furaha ya kuendelea kubakia Kagera kwa msimu ujao jambo lililowafanya mabosi wa Dodoma Jiji kuanza mazungumzo naye ili kuipata saini yake.
MSHAMBULIAJI wa Namungo, Ibrahim Ali Mkoko inadaiwa ameingia katika rada za Dodoma Jiji inayomtaka ili kukiboresha kikosi cha timu hiyo.
Taarifa zinasema Mkoko ni chaguo la kocha wa Dodoma Jiji, Mecky Maxime na tayari ameanza mazungumzo na nyota huyo aliyemaliza msimu na mabao mawili ya Ligi Kuu, huku ikielezwa Namungo inahitaji kumbakisha.
KLABU ya Coastal Union imeanza mazungumzo ya kupata saini ya aliyekuwa mshambuliaji wa Mbeya City, Maulid Shaban ambaye yupo huru.
Nyota huyo msimu uliopita akishiriki nao Ligi ya Championship ikimaliza nafasi ya sita na pointi 43, alihusika na mabao 24 kati ya 36 ya kikosi hicho baada ya kufunga 17 na kuasisti saba.