NYOTA wawili wakubwa wa timu ya taifa ya Morocco kwa sasa wapo nchini kwa ajili ya mapumziko baada ya kumalizika kwa msimu ulioisha wa 2023/2024.
Wa kwanza ni beki Achraf Hakimi ambaye anacheza soka la kulipwa Ufaransa katika miamba ya soka nchini humo, PSG ambayo imemaliza msimu ikiwa mabingwa, huku Mmorocco huyo akiwa miongoni mwa wachezaji tegemeo wa kikosi cha kwanza.
Mwingine ni kiungo mkabaji Soufyaa Amrabaat ambaye anaitumikia Manchester United ambayo katika msimu uliopita ilifanikiwa kutwaa kombe la FA.
Hawa ni nyota wawili ambao walitoa mchango mkubwa katika kuiwezesha Morocco kutinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la Dunia 2022 katika fainali zilizofanyika Qatar kitendo kilichofanya waanze kufuatiliwa kwa ukaribu na mamilioni ya watu duniani.
Kitendo chao cha kuja hapa nchini kinasaidia kwa kiasi kikubwa kuitangaza Tanzania katika maeneo mbali mbali duniani na hivyo ni neema kwa sekta ya utalii ambayo ni miongoni mwa nyanja zinazochangia kukuza pato la nchi kuleta fedha za kigeni.
Hata hivyo jambo la kushangaza ni kuona wakati wachezaji wa mataifa mengine tena wenye majina na thamani kubwa wanavutiwa na vivutio mbalimbali vilivyopo hapa Tanzania, wachezaji wetu ambao wapo navyo karibu, hawachangamkii fursa ya kwenda kuvitembelea.
Utamaduni wa kwenda kutembelea vivutio vya asılı ambavyo vipo ndani ya nchi yao unaonekana haupo katika maisha ya wachezaji wetu na ndio maana wengi wao hawaonyeshi kutamani kufanya mapumziko yao katika vivutio vyetu
Nadhani mamlaka zinazohusika na utalii na maliasili zinatakiwa kufanya kazi kubwa ya kutoa elimu kwa wachezaji wetu hapa nyumbani ili wawe mabalozi wazuri wa vivutio vyetu.
Wahenga walisema uungwana unaanzia nyumbani hivyo mabalozi wa kwanza wa rasilimali zetu walipaswa kuwa wachezaji wetu wazawa tofauti na hali halisi ya sasa ambapo wengi wamejiweka mbali.