Dar es Salaam. Imeelezwa kutokana na baadhi ya watu kukosa ujasiri wa kufanya uamuzi binafsi katika kuzichangamkia fursa, hali hiyo imesababisha walio wengi kuwa masikini.
Hayo yamebainishwa leo Alhamisi, Juni 27, 2024 na wadau mbalimbali katika mdahalo ulioandaliwa na Benki ya CRDB, ilipoungana na wadau wengine kuadhimisha Siku ya Wajasiriamali Duniani (International MSME Day) kwa kuendesha semina kwa wateja wake na baadhi ya wabia wa kimkakati.
Akizungumza kwenye mjadala huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Royal Mark, Johnson Kapira amesema kwa Mtanzania masikini kunatokana na kutokuwa na ujasiri wa kufanya uamuzi binafsi wa kuzichangamkia fursa zilizopo.
Akieleza jinsi alivyoanza ujasiriamali mwanzoni mwa miaka ya 1990 baada ya kuhitimu chuo kikuu, amesema kutokana na changamoto za kupata ajira zilizokuwapo alianzisha kampuni yake na akawa anaomba mikopo ya kufanikisha kazi alizokuwa anazipata na mpaka sasa anakopesheka kiasi kikubwa zaidi.
“Nilianza nikiwa mfanyabiashara mdogo sana. Nilianza biashara mwaka 1995 nikiomba zabuni serikalini na kampuni binafsi. Mtaji ulikuwa changamoto lakini Benki ya CRDB imenikuza kupitia huduma yake ya Purchase Order Agreement. Leo hii naweza kukopa mpaka Sh4 bilioni,” amesema Kapira.
Naye Josephat Kibwanga ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Qualitas amesema:“Mimi ni mteja mkubwa wa Benki ya CRDB. Mikopo yao imeniwezesha kuimarisha huduma katika hospitali yangu na kwa sasa utakuwa muujiza, iwapo mgonjwa atakuja hospitalini kwetu na akaambiwa hakuna dawa. Haya yote yamewezekana kutokana na mikopo inayopatikana kwa wakati kutoka Benki ya CRDB.”
Maneno ya wajasiriamali hao yana akisi kile alichokisema Ofisa Mkuu wake wa Uendeshaji, Bruce Mwile wakati akifungua maadhimisho hayo:“Leo tukiadhimisha siku hii niwahakikishie kuwa Benki yetu ya CRDB itaendelea kuweka mikakati madhubuti ya kuwawezesha wajasiriamali na biashara changa, ndogo na za kati nchini tukiamini kwa kufanya hivyo tunachochea ongezeko la ajira, kuimarisha kipato binafsi na kukuza uchumi wa Taifa letu kwa ujumla wake.
“Ahadi yetu ni kwamba tupo tayari kuwahudumia na kutembea nanyi katika safari yenu ya mafanikio,” amesema.
Hata hivyo, wataalamu wa uchumi nchini wametaja mambo kadhaa, ambayo ni mwiba kwa walio wengi kukosa ujasiri kimaamuzi katika kuzichangamkia fursa hasa za mikopo.
Mtaalamu wa masuala ya uchumi, Oscar Mkude amesema Watanzania wengi wanashindwa kuzichangamkia fursa kutokana na kutokuwa na fedha au rasilimali zitakazowawezesha kupata mikopo.
Mkude amesema ili mjasiriamali akopesheke, lakini awe na uwezo wa kuwa na mtaji, “Benki zetu zinatoa mikopo lakini lazima uwe na mtaji wa kifedha, lakini pia riba yake inakua ngumu asilimia 17 hapo hujaingia kwenye biashara yenyewe ukapata faida ya kuweza kurejesha huu mkopo.”
Mkude ametaja sababu ya pili kuwa ni mazingira ya biashara kwani nyingi zina changamoto.
“Ukianzisha biashara leo atakuja mtaalamu wa Osha mara zimamoto, ushuru, TRA wote hawa wanataka ulipie kodi mbalimbali kwa gharama zake ni wale wenye uwezo ndiyo wanaweza kuendelea na biashara,” amesema Mkude.
Mwile amesema kuwa kipaumbele chao siku zote ni kumhudumia Mtanzania na kuhakikisha anaboresha maisha yake kwa kumpa huduma zinazoendana na kukidhi mahitaji yake.
Ili kukuza ujasiriamali, Mwile amesema Benki ya CRDB inatambua kuwa shughuli zake zikichangia asilimia 27 ya Pato la Taifa na ili itoe mchango wake ipasavyo, kunahitajika huduma na mifumo shirikishi itakayowasaidia wajasiriamali kuyafikia malengo waliyojiwekea.
“Kutokana mikakati tuliyojiwekea, Benki yetu imekuwa kinara katika uwezeshaji wajasiriamali kwani hadi Mei 2024 tulikuwa tumetoa zaidi ya Sh995.346 bilioni kwa zaidi ya wajasiriamali 21,470 katika sekta mbalimbali ikiwamo sekta ya kilimo, ujenzi na makazi, miundombinu, usafirishaji, afya, elimu, nishati, madini, biashara na viwanda, pamoja na uchumi wa buluu ili kuimarisha shughuli zao,” amesema Mwile.
Mwile amesema sekta ya ujasiriamali imekuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi wa mataifa mengi duniani kwa kuchochea ubunifu na uanzishaji biashara mpya, zinazoongeza ajira na kuimarisha kipato cha watu binafsi na jamii kwa ujumla.
“Kwa kuanzisha biashara ndogo na za kati, wajasiriamali huchangia moja kwa moja kwenye ukuaji wa pato la Taifa na kuongeza mapato ya serikali kupitia kodi. Sekta hii pia ina mchango mkubwa katika kuboresha teknolojia na kuongeza ufanisi katika uzalishaji wa bidhaa na huduma, hivyo kufanya uchumi kuwa na ushindani zaidi kimataifa,” amesema Mwile.
Taarifa za Umoja wa Mataifa (UN) zinasema wajasiriamali ni injini muhimu ya kufanikisha utekelezaji wa Maendeleo Endelevu (SDG) kwani kundi hili linachangia asilimia 90 ya biashara zote zilizopo duniani, ambazo hutoa kati ya asilimia 60 mpaka 70 ya ajira zenye staha na kuchangia zaidi ya nusu ya pato la dunia.
Tanzania kuna zaidi ya biashara ndogo za ujasiriamali milioni 3 zinazowapa uhakika wa kipato wamiliki wake.
Ili kumkuza mjasiriamali kuanzia ngazi ya chini, Mwile amesema Taasisi ya CRDB Bank Foundation ambayo ni kampuni tanzu ya Benki ya CRDB inatekeleza programu ya Imbeju inayotoa elimu ya ujasiriamali na fedha kwa wanawake na vijana pamoja na kuwapa mitaji wezeshi inayoanzia Sh100,000.
Hadi sasa tayari programu hiyo imewafikia wajasiriamali zaidi ya 400,000 na kutoa mitaji wezeshi zaidi ya Sh10 bilioni.
Sambamba na maadhimisho hayo, Benki ya CRDB imezindua ‘CRDB Biashara Account’ ambayo ni mahsusi kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo wenye malengo ya kukuza miradi yao, kuongeza idadi ya wateja wanaowahudumia, kukuza mapato yao ili wakue zaidi na kuanzisha kampuni kubwa zitakazohudumia nchi nzima hata nje ya mipaka pia.