JIWE LA SIKU: Mambo manne kuibeba Simba msimu ujao

VIONGOZI wa Simba wameanza mchakato wa kukisuka upya kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao baada ya kukosa taji la Ligi Kuu Bara kwa misimu mitatu mfululizo na kushuhudia likienda kwa watani wao Yanga ambao nao wameanza kujiimarisha zaidi.

Katika kuthibitisha hilo, tayari Simba imeshatangaza kuachana na wachezaji sita, akiwamo aliyekuwa nahodha wa timu hiyo, John Bocco, Shaaban Idd Chilunda, Saido Ntibazonkiza ‘Saido’, Kennedy Juma, Henock Inonga na Luis Miquissone ambao wote wamepewa mkono wa kwaheri.

Wakati ikitema nyota hao, tayari imemtambulisha aliyekuwa beki wa Coastal Union, Lameck Lawi huku Israel Mwenda, Mzamiru Yassin na Kibu Denis wakiongezewa mikataba mipya ili kuendelea kusalia ndani ya kikosi hicho kwa msimu ujao.

Ili kuleta ushindani kwa msimu ujao, yapo mambo manne ambayo viongozi wa timu hiyo wameyafanya na kuonyesha ni kwa jinsi gani wanataka kurejesha furaha kwa mashabiki wa kikosi hicho cha Msimbazi ambacho kimekuwa kinyonge kwa misimu mitatu mfululizo.

Baada ya kukosa mataji misimu mitatu mfululizo aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo, Salim Abdallah ‘Try Again’ aliamua kujiuzulu kwa maslahi mapana na timu hiyo pamoja na baadhi ya wajumbe wengine waliojiweka pembeni.

Kujiweka pembeni kwa ‘Try Again’ kulimfanya kumuachia rais wa heshima wa Simba na mwekezaji wa klabu hiyo, Mohammed ‘Mo’ Dewji ambaye baada ya kupewa kiti hicho aliteuwa wajumbe wengine huku akimrudisha Salim kuwa kama mjumbe wa bodi.

Kitendo hicho kilitafsiriwa kwa mitazamo tofauti lakini hakuna ubishi kwamba uwepo wa wawili hao ni ishara tosha klabu hiyo inataka kupiga hatua kwani imeshajua ilipoteleza ndio maana ikarudisha baadhi ya wanachama akiwamo, Crescentius Magori.

Kutokana na kuvurunda, viongozi wa timu hiyo walikaa chini na kuamua kuondoa wachezaji wote ambao walionekana kushindwa kubeba uzito wa jezi za wekundu hao, wanachukua mishahara mikubwa ingawa viwango vyao vilikuwa haviridhishi akiwemo, Luis Miquissone.

Hadi sasa inaelezwa Simba tayari imekamilisha usajili wa mastaa wanane wa kigeni ambao wanaingia kuboresha kikosi cha timu hiyo ambayo kwa asilimia kubwa kimevunjwa lengo likiwa ni kuanza upya.

Ni wazi Simba imeamua kusaka wachezaji wapya ambao pia wana umri mdogo tofauti na misimu mitatu nyumba ambayo walijaza mastaa wengi wenye umri mkubwa kama Saido ambaye licha ya kuongwe wake ndani ya kikosi hicho misimu miwili aliyocheza amekuwa kinara wa upachikaji mabao.

Saido msimu wake wa kwanza alifunga mabao 17 akiibuka mfungaji bora sawa na aliyekuwa staa wa Yanga, Fiston Mayele aliyetua Pyramids ya Misri ingawa kuondoka kwa Saido kumezua maswali mengi ya nani atakayevaa viatu vyake msimu ujao.

Kuachana na mastaa hao na kuamua kufanya usajili mpya ni dalili nzuri kwa timu hiyo ili kujenga kikosi kipya ambacho kimezingatia masuala ya umri japo haitokuwa haraka kujipata japo itawasaidia huku mbele kutokana na falsafa yao.

Sio suala geni kwa Simba kuweka kambi nje ya nchi, ni utaratibu ambao wamekuwa wakifanya kila msimu hasa miaka ya hivi karibuni wao ndio wamekuwa wakisafiri mara kwa mara tofauti na watani wao Yanga ambao mafanikio yao yote kwenye misimu mitatu wamekaa kambi jijini Dar es Salaam.

Kitu kipya kwenye suala la kambi msimu huu kwa Simba na ambacho kimeonyesha utofauti ni kuamua kukusanyika wote kwa pamoja tofauti na misimu mitatu nyuma ambapo wachezaji walikuwa wanaenda kwa mafungu.

Msimu huu inaelezwa Simba wameamua kufanya usajili mapema na kuitana haraka Dar es Salaam tayari kwa kujiandaa na safari ya kwenda kujenga kikosi cha ushindani ambao kambi hiyo itakuwa Misri katika mji wa Ismailia ambako walishawahi kwenda.

Kama utakumbuka, msimu wa 2022/2023, timu hiyo ilienda kuweka kambi katika mji huo wa kifahari unaofahamika kwa jina la ‘Little Paris’, ambao ilikuwa ikinolewa na aliyekuwa kocha wa kikosi hicho, Zoran Manojlovic Maki mwenye uraia pacha wa Serbia na Ureno.

Simba kwa misimu ya hivi karibuni imeongozwa na zaidi ya makocha tofauti ambapo msimu ulioisha ilinolewa na watatu ambao wawili walikuwa kigeni na mzawa, Juma Mgunda aliyeiongoza timu hiyo kumaliza msimu ikiwa nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.

Ilianza msimu na Roberto Oliveira ‘Robertinho’ kutokana na matokeo mabaya aliondolewa na nafasi yake ilichukuliwa na Abdelhak Benchikha ambaye pia alishindwa kumaliza msimu na mikoba yake kuchukuliwa na mzawa Mgunda aliyeipeleka timu hiyo Kombe la Shirikisho Afrika.

Sasa inaelezwa uongozi wa timu hiyo umesaka kocha ambaye anaendana na falsafa za timu hiyo ambayo mfumo wake ni timu kucheza soka la kutembeza pasi na sio ‘butua-twende’ ambaye inaelezwa tayari amepatikana na ataungana na timu kwa ajili ya safari ya kwenda Misri.

Inaelezwa kuwa hawajafanya makosa kwenye mchakato wa upatikanaji wake kwani wanataka kocha ambaye atahudumu na timu hiyo kwa muda mrefu ili kuondokana na kasumba ya kutimua timua makocha kama ilivyokuwa miaka ya hivi karibuni kikosini humo.

Related Posts