AKILI ZA KIJIWENI: CECAFA ijikite zaidi na wanawake, vijana

KESHO Juni 29 hadi Julai 14 ilikuwa iwe muda wa kuchezwa mashindano ya Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) kwa timu za taifa za wanaume za wakubwa yajulikanayo kama Kombe la Chalenji.

Hata hivyo, Juni 10, Cecafa ilitangaza kufutwa kwa mashindano hayo ili kuwapa wachezaji muda wa kujiandaa na mashindano ya baraza hilo kwa upande wa ngazi ya klabu yajulikanayo kama Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati au Kombe la Kagame.

Mashindano hayo ya Kombe la Kagame yamepangwa kufanyika hapa nchini kuanzia Julai 6 hadi Julai 22 ambapo yatachezwa jijini Dar es Salaam na visiwani Zanzibar.

Kabla hata ya kuanza kwake, mashindano hayo ya Kombe la Kagame yameshaonesha dalili za kupoteza mvuto kutokana na kujitoa kwa baadhi ya timu ambazo zilitegemewa kushiriki.

Pigo kubwa zaidi limekuwa ni kujiondoa mashindanoni kwa Simba, Yanga na Azam FC huku timu hizo zikitoa sababu ya kutoshiriki kuwa ni kupata fursa ya kufanya maandalizi ya msimu ambapo zote zinatarajiwa kuweka kambi zao nje ya nchi.

Juni 13, uongozi wa TP Mazembe nao ulitoa taarifa ya kutopokea mwaliko wa ushiriki wa mashindano hayo jambo ambalo linatishia uwezekano wa timu hiyo kucheza Kombe la Kagame msimu huu.

Kinachoonekana mashindano hayo pamoja na yale ya Chalenji ni ngumu kufanyika katika siku za hivi karibuni kwa vile muda ambao yamepangwa kufanyika unaingiliana na maandalizi ya msimu kwa timu na wachezaji.

Cecafa inaonekana ina nia ya dhati ya kulinda mashindano hayo lakini kiuhalisia nyakati zinayapa ugumu kufanyika na hata yakifanyika hayawezi kuwa na mvuto na msisimko kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Kama kuna uwezekano Cecafa iamue tu kuwekeza nguvu na rasilimali nyingi katika mashindano yake ya wanawake na vijana.

Related Posts