HAKUNA VIZIMBA AU MAENEO MENGINE YA KARIAKOO YALIYOGAWIWA AU KUUZWA SOKO LA KARIAKOO – UONGOZI SOKO LA KARIAKOO.

Shirika la
Masoko ya Kariakoo linatoa taarifa kwa umma kwamba kwa sasa hakuna vizimba au
maeneo mengine ya biashara yaliyogawiwa au kuuzwa kwenye soko la Kariakoo kama
walivyodai baadhi ya wafanyabiashara walionukuliwa na vyombo vya habari hivi
karibuni.

Akizungumza
na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Kaimu Meneja Mkuu wa Shirika
hilo
Sigsibert K. Valentine,
alisema  wananchi waepuke vishoka au watu
wengine wanaodai kuwa  vizimba vinauzwa
au kukodishwa kinyume cha taratibu za Serikali.

“Serikali
bado haijaanza kupangisha maeneo ya biashara au vizimba kwenye soko la
Kariakoo. Wananchi wawe watulivu na taarifa rasmi za upangishaji zitatolewa”
alisema Valentine.

Kuhusu zoezi
la uhakiki Valentine alifafanua kuwa halilengi kuwapunguza wafanyabiashara bali
kuweka kumbukumbu sahihi za wafanyabiashara ili ziwekwe kwenye mfumo wa
kidigitali tofauti na ilivyokuwa awali

Kwa sasa Shirika
linaendelea kutekeleza mipango ya Serikali ikiwemo  kukamilisha ujenzi wa soko jipya na ukarabati
wa soko la zamani, kuweka kumbukumbu sahihi za wafanyabiashara waliokuwepo kabla
ya ajali ya moto, kuandaa mpangilio mzuri wa biashara na wafanyabiashara
(market segmentation) na kuratibu maandalizi ya elimu kwa wafanyabiashara kuhusu
mfumo wa TAUSI na   Bima.

Shirika
linatoa shukrani kwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kwa kutoa Shilingi Bilioni 28.03 kutekeleza mradi huu wa kimkakati
ambapo nafasi za biashara 3,500 na ajira zaidi ya 4,000 zitapatikana. Mradi unaendelea vizuri ambapo hadi Juni 2024 umefikia
asilimia 93 na mkandarasi amelipwa zaidi ya Shilingi Bilioni 20. 


 

Related Posts