Sababu kisayansi matiti ya mwanamke kusinyaa

Dar es Salaam. Kama ulikuwa na fikra kwamba ukinyonyesha mtoto matiti yako yatalala (kusinyaa), yafute mawazo hayo.

Maziwa ya mama ndiyo chakula cha kwanza kwa kila mtoto anayekuja duniani na wataalamu wa afya wanaeleza kuwa ni kinga ya magonjwa mengi kwa mtoto. Hivyo mama anapomnyonyesha mtoto kwa usahihi, inaelezwa kuwa ni moja ya njia sahihi za kuhakikisha mtoto anakuwa mwenye afya na kukua vizuri.

Tafiti zilizofanyika sehemu mbalimbali duniani, zinabainisha kuwa maradhi ya njia ya hewa, kuharisha, maambukizo ya masikio na homa ya uti wa mgongo, hayawashambulii mara kwa mara watoto wanaonyonyeshwa vizuri maziwa ya mama zao katika kipindi cha miezi sita ya kwanza ya umri wao.

Tafiti zinaongeza kusema kuwa hata pale wanapougua maradhi hayo, hali yao huwa si mbaya ikilinganishwa na wale wasionyonya.

Hata hivyo, baadhi ya wanawake hushindwa kuwanyonyesha watoto wao ipasavyo kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo kudai kwamba wakinyonyesha matiti yao husinyaa na kulala, hivyo kupoteza mvuto.

Rahma George, ambaye ni mama wa watoto watatu anasema baadhi ya wanawake hufanya hivyo kutokana na kukosa elimu sahihi, kwani mtu anaweza asinyonyeshe na bado matiti yake yakaharibika mwonekano wake na kulala.

“Kuna mabinti wengi, tena wana umri mdogo hawajaolewa wala kuzaa lakini maziwa yamelala, kufanya hivyo ni ulimbukeni wa baadhi ya wanawake,” anasema.

Neema Ngaya anasema baadhi ya wanawake hufanya hivyo kutokana na kejeli wanazofanyiwa na wenza wao kuwaambia matiti yamelala kama ‘ndala’.

Akijibu hoja, Ishacka Sadick anasema baadhi ya wanaume hufanya hivyo kutokana na kutokubaliana na mabadiliko wanayopitia wenza wao katika kipindi cha ujauzito. Naye Samweli Zacharia anasema wakati mwingine wanaume hutoa kauli hizo kutokana na baadhi ya wanawake wanapokuwa katika kipindi cha unyonyeshaji huacha kujipenda.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa mwaka 2007 na Chuo Kikuu cha Kentucky na kuchapishwa pia katika tovuti ya Science Daily, hakuna uhusiano wowote kati ya kunyonyesha na kuanguka kwa matiti.

Pia utafiti huo ulibainisha sababu mbalimbali zinazochangia matiti ya mwanamke kuanguka, ikiwemo umri, idadi ya mimba ambazo mtu amewahi kupata pamoja na uvutaji wa sigara.

Pia tovuti healthline inabainisha sababu nyingine kuwa ni pamoja na mabadiliko katika uzito, yaani aidha kunenepa au kukonda sana, kufikia ukomo wa hedhi pamoja na vinasaba vya kurithi.

Akizungumza na Mwananchi, daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi, Dk Isaya Mhando anasema kuwa dhana hiyo haina ukweli wowote, kwani wapo wanawake hawanyonyeshi wala hajawahi kuwa na mtoto na matiti yao hulala, pia wapo wanaonyonyesha na bado matiti yake hayaanguki.

Dk Mhando anabainisha sababu mbalimbali za matiti ya mwanamke kuanguka, ikiwemo vinasaba vya urithi, umri na mabadiliko ya uzito.

Anasema moja kati ya mambo ambayo huamua muundo wa matiti ya mwanamke ni pamoja na vinasaba vya kurithi.
Anasema pia huamua uimara wa tishu zinazoshikilia maziwa, huku akiongeza kuwa kama tishu hizo ziko imara matiti ya mwanamke yatakuwa imara, haijalishi ananyonyesha au hanyonyeshi.

“Kwa wale ambao tishu zao ni dhaifu, maziwa huwahi kulala na siyo kwa sababu ya unyonyeshaji wa mtoto,” anasema.

Kwa upande wake, Meneja mradi wa Afya ya Mama na Mtoto na mtaalamu wa lishe kutoka Shirika la World Vision, Dk Daudi Gambo anasema wanawake wanaofanya hivyo wanapaswa kutafakari na kupima urembo wao na faida zinazopatikana kwa mama kunyonyesha kama inavyoshauriwa na wataalamu wa afya.

Dk Gambo anasema unyonyeshaji una faida nyingi kwa mama na pia kwa mtoto, hivyo waachane na nadharia hizo, kwani hazina ukweli wowote.

Anasema maziwa ya mama kwa mtoto huamsha hisia zake na kuimarisha ufahamu saikolojia yake.

Pia kuongeza na kuimarisha kinga ya mtoto, hivyo humsaidia kumuepusha na magonjwa mbalimbali. “Maziwa ya mama yana virutubisho vyote vya muhimu kwa ajili ya ukuaji mzuri wa mtoto, hivyo nawasihi wamama wanaonyonyesha wafanye hivyo kama inavyoshauriwa na daktari kwa ustawi wao.

Pia huimarisha upendo kati ya mama na mtoto, kusaidia kupunguza uzito na kumuepusha na saratani ya matiti.”

Uhusiano kutonyonyesha na saratani

Mkurugenzi wa Kitengo cha Kinga katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), Dk Crispin Kahesa anasema utafiti unaonyesha kunyonyesha kunatoa kinga ya saratani ya matiti.

“Kwa mama asiyenyonyesha hicho kinaweza kuongeza hatari, anaponyonyesha kwa kujibu wa utafiti kuna mpunguzia hatari ya kupata saratani ya titi,” anasema.

Kuhusu kina mama ambao hawanyonyeshi kutokana na sababu mbalimbali za kiafya huwa katika hatari.

“Saratani ya titi inaweza kuwa na mjumuisho wa sababu mbalimbali, ikiwamo hiyo ya kutonyonyesha kwa kina mama wenye watoto wachanga,” anasema Dk Kahesa.

Related Posts