NAIBU Waziri Mkuu, Dk. Dotto Biteko amesema vitendo vya mmomonyoko wa maadili vinavyotokea nchini ikiwamo mauaji ya watu wenye ualbino na mapenzi ya jinsia moja ni matokeo ya Watanzania kuuacha utamaduni wao na kuukumbatia wa mataifa mengine. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Biteko ameyasema hayo katika Tamasha la Utamaduni la Bulabo 2024 lililofanyika katika Kata ya Kisesa, Wilaya ya Magu, mkoani Mwanza, lenye kaulimbiu “Tudumishe Mila na Tamaduni zetu, Tushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024”.
Amesema anashangazwa na baadhi ya Watanzania kuyafanya mauaji ya watu wenye ualbino kama sehemu ya utamaduni wao, akisema kuwa imetokana baadhi ya watu kuchukua utamaduni wa mataifa mengine.
“Wakati fulani unajiuliza hivi inakuwaje, mauaji ya watu wenye ualbino yanafanywa kuwa ni utamaduni kwa baadhi ya watu, unajiuliza mapenzi na ndoa za jinsia moja kwa nini zije miongoni mwetu? Ni kwa sababu tumechukua tamaduni za watu wengine na kuzileta miongoni mwetu.
“Utamaduni wetu unatupa heshima na tamasha kama hili linatuwezesha kama nchi kuzingatia utamaduni wetu na kuwawezesha Watanzania kujitambua, kitendo cha kuiga utamaduni wa nchi nyingine bila kupima madhara unaweza kutuharibia na kuondoa heshima yetu,” amesema.
Aidha, Dk. Biteko amesema utambuzi wa makabila miongoni mwa Watanzania ni kwa ajili ya kutaniana na sio kwa ajili ya kubaguana miongoni mwao kutokana na Utamaduni wa Watanzania kuishi kama familia moja na hivyo amehimiza kufanyika kwa matamasha mengi ya utamaduni ili kuenzi mila na kudumisha utamaduni wa Mtanzania.
Katika hatua nyingine, Dk. Biteko amewataka Watanzania kujipanga vema kwa ajili ya kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa pamoja na Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka 2025, “Chagueni viongozi wenye uwezo wa kuwaongoza na kuwaletea maendeleo hata kama hawana fedha na katu msiingie kwenye mtego wa kuchagua viongozi wasio na uwezo kwa kigezo cha fedha” alilisitiza Dk. Biteko.
Awali, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Damas Ndumbaro amesema Serikali kupitia wizara kwa kushirikiana na watemi wa maeneo mbalimbali imepanga kufanya tamasha kubwa zaidi litakalofanyika katika Viwanja vya Majimaji, Songea Mkoani Ruvuma.
Naye, Kiongozi wa Umoja wa Watemi nchini Anthoni, ameishukuru Serikali kwa kuwatambua na kuwawekea mazingira rafiki katika kuendeleza matamasha ambayo yanaendeleza mila na desturi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi yetu, Tamasha la Utamaduni wa Wasukuma limeshirikisha watemi kutoka mikoa saba ambayo ni Mwanza, Kagera, Shinyanga, Geita, Simiyu, Mara na Tabora.