Simba yatema wawili wa kigeni

KATIKA kusuka kikosi kipya cha msimu ujao wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL), Simba Queens imeachana na nyota wawili wa kigeni.

Joanitha Ainembabazi

Mabingwa hao mara wa nne wa WPL wameachana na Danai Bhobho raia wa Mzibabwe na Mganda Joanitha Ainembabazi.

Habari kutoka ndani ya Simba zinaeleza kuwa wachezaji hao hawatakuwa sehemu ya kikosi cha msimu ujao kutokana na kuonyesha viwango vya kawaida tangu waliposajiliwa kiasi cha kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara ndani ya kikosi hicho kilichotwaa ubingwa kikiinyang’anya JKT Queens.

Wote wawili walisajiliwa msimu uliopita, lakini wamekuwa wakipata nafasi chache za kucheza kutokana na ushindani waliokutana nao, upande wa Bhobho nafasi yake ilikuwa ikichezwa na Elizabeth Wambui na Joanitha ambaye ameshindwa kuleta ushindani mbele ya Asha Djafar.

Mmoja wa viongozi wa klabu hiyo (jina tunalo), amesema hawana mpango na wachezaji hao msimu ujao kutokana na kile walichofanya.

“Sasa hivi hata Ligi ya Wanawake inaonyeshwa hivyo, tuliwaona na tukawasiliana na walimu wao kwamba kwenye maeneo yao tunahitaji wachezaji wengine na tayari tumewapata,” amesema kiongozi huyo.

Joanitha ambaye anacheza nafasi ya ushambuliaji kwenye mechi 18 amefunga mabao mawili na asisti moja.

Related Posts