Biashara zarejea Kariakoo, Wafanyabiashara wataja mwarobaini

Dar es Salaam. Wafanyabiashara wa Kariakoo, jijini hapa wameendelea na shughuli zao baada ya kugoma kwa siku nne kuanzia Jumatatu Juni 24, 2024 huku wakidai mapendekezo ya kupunguzwa kwa faini ya Sh15 milioni hadi Sh4 milioni imebaki kwenye makaratasi.

Mgomo huo ulioanzia Dar es Salaam, ulisambaa mikoa mingine ikiwamo Kigoma, Arusha, Dodoma, Mbeya, Mwanza, Mtwara, Morogoro na Iringa.

Biashara katika maeneo mbalimbali zimeanza kurejea baada ya Serikali ya na Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) kufikia makubaliano ya kumaliza mgomo wa huo kwa kuweka maazimio 15.

Wakizungumza na Mwananchi Digital leo Ijumaa, Juni 28, 2024 wafanyabiashara wamedai mapendekezo yanayozungumzwa na Serikali hayafanyiki kwa vitendo bali ni kwenye makaratasi hivyo ni ngumu kwa wao kuyazingatia.

Jana, Serikali kupitia Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba ilipendekeza kufanyika kwa marekebisho ya sheria ambayo yanashusha faini aliyokuwa akitozwa mfanyabiashara ambaye hajatoa risiti kutoka Sh15 milioni hadi Sh4 milioni. 

Mabadiliko hayo ya ibara ya 87 yanakwenda sambamba na mapendekezo ya marekebisho katika Sheria ya Usimamizi wa Kodi, Sura ya 438 ambayo yamegusa ibara tofauti.

Akizungumza na Mwananchi Digital, baada ya mapendekezo hayo kuwasilishwa bungeni, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara, Martin Mbwana amesema punguzo la faini lililopendekezwa litawapa nafuu kwani ilikuwa ni matarajio yao baada ya kupeleka hoja zao Dodoma.

“Kwetu wafanyabiashara tunapokea kwa mikono miwili faini ya Sh4 milioni kwani ya awali ilikuwa inatuumiza, hilo moja tayari tunasubiri kukamilika kwa mengine,” alisema Mbwana.

Hata hivyo, Zephania Raphael amesema kupunguzwa kwa faini hadi Sh4 milioni sio makusudio ya wafanyabiashara bali itaendelea kuingia kwenye mifuko ya watu binafsi.

“Lengo letu sio masuala ya faini, tunataka kuwe na utaratibu kama wauza mafuta kila kitu kinamalizika bandarini kwa sababu kodi zote zimewekwa sehemu moja sio kwa mgawanyo,” amesema Raphael.

Amedai kilichozungumzwa ni kutengeneza mazingira ya rushwa kwa wakusanya kodi na itaendelea kukaribisha mazungumzo baina ya wakamataji na wafanyabiashara.

Mfanyabiashara mwingine, Jackson John amesema si mara ya kwanza wafanyabiashara kupaza sauti zao kwa malalamiko hayo lakini hakuna kinachofanyika.

“Hata hicho walichopendekeza bungeni bado hakijaanza utekelezaji wake hivyo inakuwa ngumu kusema kama ni ahueni kwetu kwa sababu hata mwaka jana alipokuja Waziri Mkuu, mambo yalitulia lakini tumerudi kulekule,” amesema.

Amesema mapendekezo yao ni kodi zote kuchanganywa na zilipwe katika eneo moja kama ilivyo kwa wafanyabiashara wa mafuta tofauti na sasa.

“Sasa hivi kila mmoja anakuja na kodi yake, huyu anataka hii huyu hii mwisho wa siku mnalipa kodi ya aina moja kwa taasisi mbili inatuumiza hii,” amesema John.

Ritha Sanga ambaye pia ni mfanyabiashara amesema njaa ndiyo inayowafanya kufungua maduka yao lakini bado wanaumizwa na utitiri wa kodi.

“Bado tunaumia ni vile tu hamna namna tuna familia zinatutegemea kodi, ada, ukija huku kamatakamata,” amesema.

Related Posts