MAKALA: ALIYEKUWA MRAIBU KWA MIAKA 21, AANZISHA ASASI SEYOLBADA ILI KUIKOMBOA JAMII

Said ameeleza kwamba ,alikabiliwa na changamoto nyingi, kwani alikuwa akishikwa mara kwa mara na polisi , baadae familia iligundua kuwa kajiingiza kwenye matumizi hayo na kuanza kumkera aachane na vitendo hivyo.

“Baadae nilikaa mwenyewe nikajifikiria mbona sijapata faida yeyote toka nianze kutumia dawa hizi baada ya kutumia kipindi kirefu ,sana sana niliathirika kiakili, kimwili na kiuchumi , kwakuwa nilikuwa nauza kila kitu “anafafanua Said.

Said anashukuru kitengo cha kutoa tiba kwa waraibu (Methadone) katika hospital ya Mwananyamala ,ambapo alianza tiba ya methadone 2013-2017 Mwananyamala na 2021 Novemba aliendelea na tiba hiyo hospital ya Tumbi na sasa amemaliza.

NINI ANAFANYA KWASASA

Said anajivunia kuwa Mkurugenzi wa asasi yake aliyoianzisha inayojulikana kama Secure Your Life Benefits Against Drug Addiction ( SEYOLBADA TANZANIA), makao makuu yake yapo Mloganzila, kata ya Kiluvya, wilayani Kisarawe, Mkoani Pwani, ambayo inahusika na kupunguza uhitaji na madhara kwa tabia hatarishi kama biashara, matumizi na utegemezi wa dawa za kulevya zinazosababisha magonjwa ambukizi.

“Nimeanzisha asasi hii ili kulinda recovery yangu na pia kusaidia waraibu wengine baada ya kujua madhara na changamoto nilizopitia kipindi natumia dawa za kulevya “

Said anaelezea kuwa ,lengo kubwa ni kupunguza na kutokomeza biashara na matumizi ya dawa za kulevya .

Vilevile anasema, kazi kubwa wanayoifanya ni kutoa elimu kinga kwa watoto, vijana mashuleni, vyuoni pamoja na elimu tiba kwa waliopata madhara sanjali na jamii kwa ujumla kwenye kupinga biashara na matumizi ya dawa hizo.

Said anaiambia jamii hasa vijana kwamba ,dawa za kulevya ni hatari kwa binadamu kwasababu husababisha magonjwa ya mapafu, kuharibu utindio wa ubongo na magonjwa mengine ambukizi hususan ukimwi, kifua kikuu na homa ya ini, mfano wa madawa hayo ni kokaine, heroin ,bangi na miraa.

Kuna watu wengi walioathiriwa na dawa za kulevya, lakini yanazidi kuenea kwa sababu ni biashara kubwa inayoingiza pesa nyingi.

Anawaomba baadhi ya jamii, kuacha tabia ya kuwatenga na kuwanyanyapaa waraibu kwa kuwaita majina yasiyofaa kama WATEJA ,kwani sio wote wamependa kuingia katika vitendo hivyo.

Kadhalika Said anashukuru Serikali kupitia TAMISEMI, Wizara ya afya, Serikali ya Mkoa wa Pwani, wilaya ya Kisarawe na Mganga Mkuu mkoani Pwani kwa ushirikiano wao hadi kusimama kwa asasi ya SEYOLBADA ,japokuwa bado changa na inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo raslimali fedha na vitendea kazi.

Namuomba Rais Samia Suluhu Hassan, wizara ya afya, Maendeleo ya JAMII, TAMISEMI kupitia mamlaka husika na wadau waziangalie kwa jicho la kipekee asasi changa ikiwemo SEYOLBADA ili kushirikiana kufikia waraibu na jamii kwa kutoa elimu na kupeleka waraibu kwenye tiba ya methadone kwa waraibu.

SERIKALI MKOANI PWANI

Mkuu wa mkoa wa Pwani ,Abubakar Kunenge anaeleza ,mkoa unaendelea na mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa kushirikiana na taasisi na asasi zinazopambana na matumizi ya dawa za kulevya, kufanya doria na kudhibiti mianya na njia zote za panya kupitisha madawa hayo.

Anaeleza ,kupitia operesheni mbalimbali kwa kipindi cha Julai 2023 hadi April 2024, mkoa umefanikiwa kukamata watuhumiwa wa dawa za kulevya 481, ambapo wameshughulikiwa kwa kuwachukulia hatua za kisheria na wengine kufikishwa mahakamani.

Kunenge anaeleza, kati ya watuhumiwa hao watuhumiwa 320 wamefikishwa mahakamani,103 kesi zao zimetolewa maamuzi, 134 taratibu za upelelezi zinaendelea bado zinakamilishwa wakati wowote watafikishwa mahakamani.

HALI YA MATUMIZI YA DAWA ZA KULEVYA TANZANIA 2023/2024

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama, mwezi mei, mwaka 2024, ametoa taarifa ya hali ya dawa za kulevya nchini kwa mwaka 2023 ambayo inaelezea mafanikio yaliyopatikana katika vita dhidi ya dawa za kulevya.

Anasema, mwaka 2023, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola vilifanikiwa kukamata jumla ya kilogramu 1,965,340.52 za dawa za kulevya aina ya heroin, cocaine, methamphetamine, bangi, mirungi, skanka na dawa tiba zenye asili ya kulevya na kuwakamata watuhumiwa 10,522.

“Takwimu za mwaka 2023 zinaonyesha mafanikio makubwa, kwani kiasi cha dawa za kulevya kilichokamatwa ni kiasi kikubwa kuliko kiasi kilichokamatwa wakati mwingine wowote nchini.

Kiasi hiki ni karibu mara tatu ya kile kilichokamatwa kuanzia mwaka 2012 hadi 2022, ikiwa ni ishara ya dhamira ya dhati na utashi wa kisiasa wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan kupambana na janga hili” anaeleza Jenista.

Jenista ameeleza, hadi kufikia mwezi disemba 2023, vituo vya tiba saidizi na unasihi kwa waraibu wa dawa za kulevya (MAT Clinics) vilivyohudumia waraibu 15,912 vilifikia 16, na nyumba za upataji nafuu (Sober Houses) na 56 zilizohudumia waraibu 3,488.

“Jumla ya waraibu 903,062 wa dawa za kulevya na vilevi vingine walipata huduma katika hospitali za wilaya, mikoa na rufaa nchini.

Ameeleza kuwa, Serikali imeweka jitihada kubwa katika kuzuia matumizi ya dawa za kulevya nchini kwa kuimarisha elimu na mikakati ya kukabiliana na tatizo hili kupitia vyombo vya habari, mitandao ya kijamii, semina, makongamano, mikutano na dawa za kulevya shuleni na vyuoni.

Aidha anafafanua ,Serikali imetunga Sera ya Taifa ya Kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya ya mwaka 2024 ili kuhakikisha ushiriki wa wadau wote katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya.

Waziri huyo anatoa rai kwa jamii, kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya na kusisitiza kuwa elimu ya kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya inapaswa kuanzia ngazi ya familia ili wasijiingize kwenye makundi hatarishi.

RIPOTI YA DUNIA YA DAWA ZA KULEVYA YA UNODC 2023

Ulimwenguni kote, zaidi ya watu milioni 296 walitumia dawa za kulevya mwaka 2021, ongezeko la asilimia 23 katika miaka 10 iliyopita imeeleza ripoti hiyo ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na kupambana na dawa za kulevya na uhalifu, UNODC.

Takwimu mpya zinaweka makadirio ya kimataifa ya watu wanaojidunga dawa za kulevya kwa mwaka 2021 kuwa milioni 13.2, asilimia 18 juu kuliko ilivyokadiriwa hapo awali.

Ripoti hiyo inaeleza, idadi ya watu wanaougua matatizo ya matumizi ya dawa za kulevya imepanda kufikia watu milioni 39.5, sawa na ongezeko la asilimia 45 katika kipindi cha miaka 10.

Inaelezea, kundi la vijana ndio walio hatarini zaidi kutumia dawa za kulevya na huathiriwa na ugonjwa wa matumizi ya dawa katika maeneo kadhaa ulimwenguni.

Barani Afrika, asilimia 70 ya watu wanaopata matibabu dhidi ya dawa za kulevya wako chini ya umri wa miaka 35.

Tangu mwaka 1989, Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 26 Juni, inaadhimisha siku ya kupambana na biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya duniani.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na kupambana na dawa za kulevya na uhalifu, “United Nations Office on Drugs and Crime, UNODC” inasema, lengo ni kusaidia maboresho ya uelewa mpana zaidi wa mapambano dhidi ya biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya duniani.

Kauli mbiu inayoongoza maadhimisho haya kwa mwaka 2024 ni “kupambana na dawa za kulevya: kuwekeza katika kuzuia kwa maisha bora ya baadaye.” Ni wazi kwamba, matumizi haramu ya dawa za kulevya ni janga linaloiathiri jamii.

Related Posts