Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi Dkt. Ali Possi akiwasilisha hotuba ya ufunguzi wa mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la TCAA linalofanyika Morogoro
Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la TCAA wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi Dkt. Ali Possi akiwasilisha hotuba ya ufunguzi wa mkutano huo
Watumishi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), wamepongezwa kwa kuendelea kufanya Baraza la Wafanyakazi lenye tija na kuhimizwa kuendelea kuwajibika ili kuwa chachu ya maamuzi makubwa ya kuboresha uboreshwaji wa huduma za Usafiri wa Anga nchini.
Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi Dkt. Ali Possi wakati wa ufunguzi wa Baraza la wafanyakazi la TCAA uliofanyika Aprili 23,2024 mjini Morogoro.
Pia ameongeza kuwa, kufanyika kwa vikao hivyo vya Baraza ni kuimarisha demokrasia mahala pa kazi,na kuwataka wajumbe wa Baraza hilo kurudisha mrejesho kwa watumishi wenzao ambapo pia amewahimiza watumishi wa TCAA kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuendelea kutenda kazi kwa ufanisi.
“Tunatambua umuhimu wa TCAA katika maendeleo ya nchi yetu lakini TCAA inajengwa kuianzia na wewe mtumishi mmoja, nawasihi sana mfanye kazi kwa kushirikiana kila mmoja kwa nafasi yake na inapobidi msaidie mwingine ili kuhakikisha malengo ya taasisi na serikali kwa ujumla yanafikiwa na huduma inatolewa” amesema Dkt. Possi.
Awali akizungumza Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCAA Bw. Daniel Malanga amesema Mamlaka inatekeleza Mradi wa ufungwaji wa mitambo ya Mfumo wa Mawasiliano kwa njia ya Sauti kati ya Rubani na Mwongoza ndege yaani VHF Radio Communication Systems ili kuboresha huduma ya Uongozaji Ndege katika Anga la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hii ikiwa na lengo la kuboresha mawasiliano katika anga la Tanzania.
“Mradi huu unatekelezwa kwa ufadhili wa Serikali kuu kwa fedha za kitanzania bilioni 31.5 ambapo Mamlaka iliandaa mahitaji yaani specification na kutangaza tenda shindanishi ambapo Kampuni ya Jotron AS ya Nchini Norway ilishinda zabuni na kuingia nayo mkataba na utakelezaji ulianza mara moja”
Mkurugenzi Malanga ameongeza kuwa,vingine ni kuendelea kutolewa kwa mafunzo kwa wataalam wa Usafiri wa Anga.
Na pia Bw. Malanga amezitaja baadhi ya changamoto hasa suala la upatikanaji na ucheleweshaji wa upatikanaji wa vibali vya ajira na upandaji wa madaraja kwa Watumishi wa TCAA. Kitendo ambacho kinashusha ari ya watumishi.
Baraza hilo linafanyika kwa siku mbili ambapo mbali na kujadili masuala kadhaa yanayoihusu TCAA wajumbe wamepata nafasi ya kupiga kura na kumchagua mfanyakazi bora wa Mamlaka kwa mwaka huu wa fedha.
Katibu wa Baraza Bw. Didacus Mweya (aliyesimama) akitoa salamu za utangulizi kwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi kwa niaba ya wajumbe wa Baraza
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCAA Bw. Daniel Malanga akiwasilisha hotuba ya Mkurugenzi Mkuu mbele ya Mgeni Rasmi pamoja na Wajumbe wa Baraza
Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la TCAA wakimsikiliza Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCAA Bw. Daniel Malanga
Picha ya Pamoja