Wakulima wa pamba Shinyanga kicheko, kuuza kwa bei ya juu

Kahama. Wakulima wa pamba sasa kunufaika na ongezeko la Sh170 kwa kila kilo baada ya kampuni ya inayonunua zao hilo kuongeza kiasi hicho tofauti na bei elekezi ya Serikali kwa msimu huu.

Bei elekezi ya Serikali ni Sh1,150 kwa kilo moja lakini kampuni ya ununuzi wa zao hilo ya Nida Textile Mills Ltd, imetangaza kununua kilo moja kwa Sh1,320, jambo ambalo limeelezwa na wakulima hao litawasaidia kuinua uchumi wao.

Wakizungumza na gazeti hili leo Ijumaa Juni 28, 2024 baadhi ya wakulima katika kijiji cha Butuyu, halmashauri ya Kishapu Kahama, wameeleza furaha yao wakisema bei hiyo imewapa hamasa kuendelea kulima zaidi ili kupata faida.

“Hii ni faraja kubwa kuongezeka Sh170 sio ndogo, mkulima mwenye pamba nyingi atapata fedha nzuri na kufanyia maendeleo makubwa,” amesema mmoja wa wakulima wa kijiji cha Butuyu, Agnes Mathias.

Mkulima mwingine, Faustine Deusi amesema amelima ekari 12 za pamba, hivyo kwa sasa anaomba kukopeshwa fedha na kampuni hiyo za kuvunia ili atakapovuna na kuuza atakatwa kiasi hicho moja kwa moja.

Meneja mkuu wa kampuni hiyo, Shahid Hameed amesema kila eneo ambalo wananunua pamba wameongeza bei tofauti na iliyotolewa na Serikali, ikiwa ni mchango wao kumuinua mkulima kiuchumi kutokana na msimu huu kuwa na mvua nyingi.

Amesema hatua hiyo itamsaidia mkulima kuongeza uzalishaji kwani atakuwa na uhakika wa kipato kutokana na ongezeko hilo la bei.

Amesema wakulima wengi wamepata elimu ya namna ya kulima kisasa na kuzingatia kanuni bora za kilimo zinazotolewa na maofisa ugani wa kata na kampuni hiyo, akidai sasa wanajipanga kuwapelekea mifuko zaidi ya 500 ya kubebea pamba wakati wa mauzo na uvunaji ili kuondokana na matumizi ya kanga au vitenge.

Naye Ofisa Kilimo wa Kata ya Bunambiyu, John Emmanuel amesema licha ya elimu inayotolewa kulima kisasa lakini mavuno ya msimu huu yamekuwa ya kati kutokana na mvua kubwa iliyovuruga zao hilo.

Kwa mujibu wa Emmanuel, kata hiyo ina wakulima 3,585, kati yao 1,962 wanalima pamba na 1,623 mazao mchanganyiko.

Hata hivyo, ametaja ukosefu wa magunia maalumu ya kuhifadhi pamba kuwa changamoto kwa wakulima hao, badala yake wanatumia kanga au vitenge kubebea na kuhifadhia ambazo zinachangia kuichafua.

Related Posts