Arusha. Mahakama Kuu Kanda ya Geita imemuachia huru Baraka Shija, aliyekuwa ameshtakiwa kwa kosa la kumuua mkewe, Grace Daudi baada upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha kosa na kuacha mashaka yaliyompa faida mshitakiwa.
Hukumu hiyo ambayo imepatikana katika mtandao wa Mahakama jana, imetolewa Jumanne Juni 25, 2024 na Jaji Kelvin Mhina wa Mahakama hiyo, aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo ya mauaji yaliyotokea Juni 23, 2022, Kijiji cha Nyamhomang’o, Wilaya Geita.
Katika usikilizwaji wa awali, mshtakiwa huyo alikanusha shitaka hilo na maelezo ya kosa hilo yaliyosomwa mahakamani isipokuwa akakubali tu kuwa jina lake na umri wake na pia kuwa Grace Daud alikuwa mkewe, kuwa ndio maelezo pekee sahihi.
Hiyo ikaulazimu upande wa mashtaka kuita mashahidi wake ili kuthibitisha kosa la mauaji ya kukusudia dhidi ya mshtakiwa ambapo mashahidi sita waliitwa na pia vielelezo vinne vilitolewa kortini na kupokelewa kama vielelezo vya kesi hiyo.
Miongoni mwa mashahidi hao, ni Mkuu wa Kituo (OCS) Kituo cha Nyakagwe, Inspekta Kapinga, maofisa wengine wawili wa polisi, Dk Mlakalamu Mataba aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu na Kulwa Daud aliyekuwa dada wa Grace.
Ushahidi wa Jamhuri ulivyokuwa
Katika ushahidi wake akiongozwa na mawakili wa Serikali, Godfrey Odupoy na Kabula Benjamin, shahidi wa tano, Kulwa Daud alieleza kuwa mshtakiwa na mkewe walikuwa wakiishi Kijiji cha Butobela, lakini mkewe baadae aliamua kurudi kwa wazazi.
Shahidi wa tano, aliieleza Mahakama kuwa siku ya tukio alienda nyumbani kwa mshtakiwa na marehemu ambapo alimkuta marehemu na mshtakiwa na alipowasalimia, mshitakiwa hakuitikia, lakini marehemu aliitikia salamu.
Alieleza kuwa marehemu alienda kununua mboga kijijini na alipoondoka tu, huku nyuma mshitakiwa alimuuliza shahidi huyo kama dada yake huyo (marehemu) watarudiana ama la na Mahakama ilinukuu swali hilo kuwa “Kweli huyu tutarudiana”?
Baada ya hapo alimsikia mshtakiwa akiongea kwa simu na rafiki yake akimtaka amletee zana, ambapo baadae mshtakiwa aliondoka nyumbani hapo na kwenda uelekeo aliokuwa amekwenda dada yake.
Hata hivyo, akiwa hapo nyumbani pamoja na mama yake, walisikia kelele za kuomba msaada na walipokimbilia eneo sauti ilipokuwa ikitokea, walimkuta ndugu yao huyo akiwa tayari amekufa ambapo mwili ulichukuliwa na kupelekwa nyumbani.
Shahidi wa kwanza, Inspekta Kapinga, alieleza kwamba walipofika eneo la tukio waliukuta mwili ukiwa na jeraha kichwani na kwa sababu ilikuwa usiku, daktari aliomba ndugu waupeleke mwili nyumbani kwao, na angeufanyia uchunguzi siku inayofuata.
Shahidi huyo alieleza siku iliyofuata, walikwenda kwenye nyumba ambayo mwili huo ulihifadhiwa na daktari akauchunguza na kubaini marehemu alipigwa na kitu kizito au chenye ncha kali na kusababisha fuvu la kichwa kuvunjika na kutokwa na damu nyingi.
Shahidi huyo alidai kuwa mshitakiwa alikamatwa na wananchi wa Kijiji cha Igudeja mkoani Shinyanga na baada ya kufikishwa polisi aliandika maelezo ya onyo na alikiri kutenda kosa hilo la mauaji ya kukusudia.
Mbali na shahidi huyo, shahidi wa sita, Kidaya Makoye aliyekuwa kaimu mtendaji wa kijiji, naye aliandika maelezo ya ungamo (extra judicial statement) ya mshitakiwa, ambayo hata hivyo mshitakiwa alikana kuyaandika.
Daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili huo, alieleza baada ya uchunguzi aligundua majeraha matatu ya kichwa, moja upande wa kulia karibu na sikio, jeraha la pili lilikuwa upande wa kushoto wa kichwa, na la tatu lilikuwa usoni.
Alieleza majeraha hayo yalisababishwa na kitu Kizito na kuwa aligundua kulikuwa na damu kwenye pua na masikio, ambayo ilionyesha kuwa kulikuwa na jeraha la ubongo ambalo lilisababisha damu na sababu ya kifo ilikuwa jeraha kali la kiwewe la ubongo.
Akijitetea mahakamani hapo kwa kuongozwa kutoa ushahidi wake na Wakili Musyangi, alidai kuwa siku ya tukio akiwa anatokea shambani, alipewa taarifa na baba mkwe wake kuwa mkewe alivamiwa na mtu asiyejulikana alipokuwa akitokea shambani, na kuuawa.
Katika utetezi wake huo, aliiambia mahakama kuwa akiwa katika kazi yake ya kawaida ya ufyatuaji matofali, alikamatwa na askari polisi wawili aitwaye Paschal na Kilian na mgambo aitwaye Jose Mnyama na kupelekwa Kituo cha Polisi Nyakagwe.
Alidai akiwa kituoni hapo aliandika maelezo na alipokana kutenda kosa hilo hawakumuamini, akawekwa kizuizini ambako alivuliwa nguo na kulazimishwa kusema ukweli ambapo pia alikana kupelekwa kwa mlinzi wa amani na kuandika maelezo.
Hukumu ya Jaji ilivyokuwa
Baada ya Mahakama kusikiliza hoja za pande zote mbili, Jaji alisema ilikuwa na jukumu la la Mahakama kupima kama mshtakiwa ana hatia ama na hilo ni jukumu la upande wa mashitaka kwa mujibu wa sheria kifungu cha 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu.
Jaji alieleza katika kesi hiyo ushahidi uliotolewa hakuna ubishi kuwa Grace alifariki, baada ya kuthibitishwa na mdogo wake aliyemkuta eneo la tukio, pamoja na daktari aliyefanya uchunguzi na ripoti ya uchunguzi wa maiti ambayo pia ilionyesha chanzo cha kifo hicho.
Kuhusu suala la mshtakiwa kumuua mke wake, alieleza kuwa hakuna ushahidi wa moja kwa moja au shahidi wa macho kumuunganisha mshtakiwa na kosa la mauaji.
Jaji alisema kesi ya upande wa mashtaka inatokana na ushahidi wa kimazingira kutoka katika ushahidi uliotolewa na mdogo wa marehemu, kwamba marehemu alipoondoka baada ya hapo, mshtakiwa alikwenda uelekeo wa marehemu.
Alieleza kesi ya mashtaka inategemea ungamo la mshtakiwa kupitia maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa kwanza na maelezo ya ziada ya ungamo kutoka kwa mlinzi wa amani.
Kuhusu ushahidi wa kimazingira, Jaji alisema sheria inayohusiana nayo iko wazi huku akinukuu kesi iliyotolewa uamuzi na Mahakama ya Rufani ikieleza;-.
“Mahakama hii imekuwa ikisisitiza kwamba ushahidi wa kimazingira uelekezwe dhidi ya mtuhumiwa lazima asiwe na uwezo wa kutafsiri zaidi ya moja na lazima ielekeze kwa hitimisho kwamba ni mtuhumiwa ndiye anayehusika na kifo cha marehemu.”
Jaji alisema katika kesi iliyopo mbele yake, hakuna mtu aliyeona kilichotokea wakati mshtakiwa anaondoka kwenye eneo hilo kwa hiyo kutokana na kukosekana kwa ushahidi huo wa muda na kwa kuwa kila mmoja aliondoka kwa wakati wake, kulizua mashaka.
Kulingana na hukumu hiyo, Jaji alisema mashaka yaliyopo juu ya matukio ya siku hiyo ya tukio yanapunguza uwezekano wa mtuhumiwa kuwa mtu wa mwisho kuonekana akiwa na marehemu akiwa bado hai.
Amesema katika ushahidi wa kimazingira wa shahidi wa tano ni dhaifu na unashindwa kubainisha kuwa mshtakiwa ndiye aliyekuwa mtu wa mwisho kujulikana kuwa na marehemu alipokuwa bado hai.
Jaji huyo amesema kuhusu mshtakiwa kukamatwa na wananchi baada ya kudaiwa kukimbia alipotenda kosa hilo,na kwa bahati mbaya, raia hao hawakuitwa ili kuthibitisha kwa nini walimkamata mshtakiwa hivyo kupata ushahidi wao.
“Ni jambo la kawaida kwamba upande wa mashtaka haukulazimika kuitisha idadi fulani ya mashahidi katika kesi hiyo, kwani uaminifu ni muhimu zaidi kuliko idadi na kuwa wananchi hao walikuwa mashahidi muhimu katika kesi hiyo,” amesema Jaji.
Kuhusu maelezo ya onyo, Jaji alieleza ukosefu wa ushahidi wa mwenendo ambao ungeweza kuthibitisha maelezo hayo ya onyo ya mshtakiwa huyo na kuwa ingawa maelezo hayo yalikubaliwa, ukosefu wa ushahidi ulipunguza uzito wake hivyo haustahili sifa yoyote.
Jaji alieleza kutokana na hayo kilichobaki mahakamani hapo ni maelezo ya ungamo aliyoyaandika kwa mlinzi wa amani ambayo katika utetezi, mshtakiwa alikanusha vikali kuhusu maelezo ya onyo anayodaiwa kuyatoa awali.
Baada ya kupitia hoja za pande zote mbili jaji alieleza kuwa kwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha kesi bila kuacha shaka yoyote hivyo mahakama inamuona mshitakiwa hana hatia na kumuachia huru.